- Akihutubia mkutano huo, Rais Kikwete alimtaka Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii kuzungumza mgogoro huo na alipopanda jukwaani alisema miradi iliyopangwa kutekelezwa na Manispaa ya Bukoba chini ya meya huyo haiko wazi, inawaumiza wananchi na ina harufu ya ufisadi.
Bukoba. Rais Jakaya Kikwete
amewaagiza Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM), Balozi Khamis Kagasheki na Meya
wa Manispaa hiyo, Anatory Aman kumaliza mara moja mgogoro wa ardhi
uliodumu kwa muda mrefu kwenye manispaa hiyo ukiwahusisha.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo alipokuwa
akihitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Kagera kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Akihutubia mkutano huo, Rais Kikwete alimtaka
Balozi Kagasheki ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii kuzungumza
mgogoro huo na alipopanda jukwaani alisema miradi iliyopangwa
kutekelezwa na Manispaa ya Bukoba chini ya meya huyo haiko wazi,
inawaumiza wananchi na ina harufu ya ufisadi.
Alisema kulikuwa na mgawo wa viwanja vilivyokuwa
vitolewe kwa wananchi na walikuwa wamelipia fedha kwa ajili hiyo, lakini
havikuwahi kutolewa. Alisema kuna viwanja 5,000 lakini havijatolewa
mpaka sasa.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema haoni sababu ya
wawili hao kuendelea kulumbana na kusema kinachotakiwa ni kukaa pamoja
kupima viwanja vilivyopo na utaratibu wa kugawa uendelee.
“Ugawaji viwanja uendelee, kila mwenye kustahili
apewe na ambaye hakuridhika ana nafasi ya kukata rufani... hakuna sababu
ya kuendelea kulumbana,” alisema Rais.
Mgogoro kati ya Meya Amani na Balozi Kagasheki,
ulianza baada ya Manispaa ya Bukoba kuanza kutekeleza miradi mbalimbali
ikiwamo ya ujenzi wa soko la kisasa, kituo cha mabasi na upimaji wa
viwanja 5,000.
Mapema Machi mwaka huu, CCM, kupitia kwa Katibu
wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kilitolea tamko mgogoro huo na
kusema hauna tija na badala yake, unarudisha nyuma jitihada za
kuimarisha chama.
Nnauye, aliwataka wakazi wa Manispaa ya Bukoba kuendelea na shughuli zao zikiwamo za miradi ya maendeleo.
Atembelea mpaka wa Tanzania na Rwanda
Akihutubia umati wa wanaCCM, Rais Kikwete alirejea
hotuba yake ya Siku ya Mashujaa kuhusu atakayeigusa Tanzania: “Watu
hawakunielewa, wapo walioanza kufikiria sasa naanza vita, nilichokisema
ni kwamba atakayetuchokoza hatutamwacha.
“Siwezi kuagiza jeshi kuvamia nchi, jeshi letu ni
kwa ajili ya ulinzi wa amani ya taifa letu, kwa wananchi na mipaka.
Sitaruhusu hilo, sasa kama kuna mtu anafikiria vingine, shauri yake.”
Juzi Rais Kikwete alitembelea mpaka wa Tanzania na Rwanda kuona shughuli mbalimbali zinazoendelea katika mpaka huo.
Rais Kikwete alisimama kwa muda ili kukagua ujenzi
wa kituo cha kuhudumia shughuli za mpakani kati ya Tanzania na Rwanda
eneo la Rusumo, ambacho kukamilika kwake kutapunguza tatizo la
kuchelewesha usafirishaji wa mizigo na usafiri wa abiria kati ya nchi
hizo mbili.
Alielezwa kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa
kituo hicho ambacho kitafanya kazi kwa saa 24, kitapitisha magari kati
ya 400 na 500 kwa siku.
Awali, Rais Kikwete alizindua Kivuko cha Mv Ruvuvu
kitakachokuwa kikifanya kazi kwenye Mto Ruvuvu katika eneo la Rusumo
pamoja na mradi wa kusambaza umeme katika vijiji 12 vya Wilaya ya
Karagwe katika Kijiji cha Nyakayanja, Nyaishozi.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi