MEYA
wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, amefunguliwa jalada polisi
akidaiwa kutishia kumuua mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (CHADEMA),
katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya
ya Ilemema, Amina Masenza.Matata ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitangiri
aliyevuliwa uanachama wa CHADEMA mwaka jana kutokana na kusababisha
mgogoro ndani ya chama mkoani Mwanza lakini alifungua kesi mahakamani
kupinga uamuzi huo ambapo kesi hiyo bado inaendelea.Hata hivyo katika
hatua ya kushangaza, Septemba mwaka jana, Matata alichaguliwa kwenye
mkutano ambao ulikuwa haukidhi akidi ya wajumbe ambao ni madiwani 14 na
kwa mujibu wa sheria ndio wanaounda halmashauri hiyo mpya iliyomegwa
kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.Akizungumza na waandishi wa
habari juzi jijini hapa, Kiwia alisema Matata alimtishia kumuua Julai
26, mwaka huu, katika kikao hicho na kwamba tayari amefungua jalada
polisi mkoa Mwanza kulalamikia vitisho hivyo.Kiwia alisema kuwa chanzo
cha vitisho hivyo ni msimamo wake wa kumpinga Meya Matata kuongoza kikao
hicho ambapo siku hiyo mbunge huyo alisimama na kumuomba Mkurugenzi wa
Manispaa, Zuberi Mbyana, amteue mwenyekiti wa muda ili aongoze kikao.
Alisema
kuwa alifikia uamuzi huo kutokana na madiwani wa CHADEMA kutomtambua
Matata kama Meya wa Manispaa hiyo wakilalamikia uchaguzi uliomweka
madarakani kuwa ulikuwa batili kwa vile alichaguliwa na madiwani sita wa
CCM na CUF bila kuwepo madiwani wao nane.
“Siku ya
kikao niliomba ateuliwe mwenyekiti wa muda aongoze kikao maana Matata si
Meya wa Ilemela kisheria. Baada ya kusema hivyo, Matata alisimama na
kusema angeliniua. Alirudia kauli yake mara mbili tena mbele ya mkuu wa
wilaya, polisi na wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho,” alisema.
Kiwia
alidai kushangazwa na kitendo cha mkuu wa wilaya ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya pamoja na askari
waliokuwepo kikaoni kunyamazia tukio hilo na kushindwa kumkamata Matata
na kumchukulia hatua.
Alisema
kuwa kwa sasa ana mashaka na usalama wa maisha yake kwani kitendo cha
mkuu wa wilaya kushindwa kumchukulia hatua meya huyo kinatia hofu juu ya
usimamizi wa sheria.
“Kwa
kweli nashindwa kuelewa utendaji wa mkuu huyu wa wilaya, yaani mtu
anasimama mbele yake na kumtishia mtu maisha halafu yeye na askari
wanakaa kimya tu,” alihoji.
Kiwia
aliongeza kuwa baada ya vitisho hivyo, yeye pamoja na madiwani wenzake
wawili wa CHADEMA, Rosemary Brown wa Kata ya Pasiansi na Gradis Kiwia wa
viti maalumu walitoka nje ya kikao huku Matata akitishia kumfukuza
udiwani Brown.
Alipoulizwa
jana kuhusu tuhuma hizo za kutishia kumuua Kiwia, Matata alisema mbunge
huyo asiogope kuuawa maana asipomuua yeye atauawa na wengine endapo
hatapunguza mdomo.
Katika
hatua nyingine, meya huyo anadaiwa kushikiliwa kwa muda na Jeshi la
Polisi Wilaya ya Ilemela juzi kwa tuhuma za uchochezi.
Matata
anadaiwa kuwahamasisha wananchi wa Mhonze kuwapiga mawe maofisa wa jiji
la Mwanza watakapokwenda eneo hilo kugawa viwanja.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, polisi ilimshikilia kwa mahojiano zaidi kuhusu
tuhuma hizo za uchochezi. Matata alikiri kuwaamuru wananchi wa kijiji
cha Mhonze kuwafanya hivyo lakini alikanusha kuhojiwa na polisi badala
yake alisema alikwenda kituoni kwa masuala mengine na si vinginevyo.
“Kweli niliwaapia wawapige mawe watu wa jiji maana watakwendaje kupima na kugawa viwanja eneo lisilo lao.”
Uchaguzi
wa Matata ulikiuka kanuni na sheria za halmashauri. Kwa mujibu wa sheria
ni kwamba akidi ya wajumbe iliyokuwa ikihitajika kwa ajili ya meya
kupigiwa kura ni madiwani tisa badala ya madiwani sita walioshiriki
kwenye uchaguzi huo.
Badala
yake Matata alichaguliwa kuwa meya na madiwani sita pekee, wanne wa CCM
na mmoja wa CUF baada ya madiwani wengine wa CHADEMA kususia mkutano huo
wa uchaguzi.
Matata
alichaguliwa wakati suala lake la kufukuzwa uanachama ndani ya CHADEMA
likiwa bado linangojea uamuzi wa mahakama alikofungua kesi kupinga
uamuzi wa chama chake.Na Tanzania daima