Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi ,Zanzibar.
Jeshi
la Polisi Zanzibar limefanikiwa kuwakamata watu watatu wanaosadikiwa
kujihusisha na vitendo vya uhalifu wakiwa na bastola moja ambayo ilikuwa
imefichwa katika shamba la migomba ikiwa imechimbiwa chini ya ardhi
kwenye kopo la rangi.
Akizungumza
na waandishi wa habari Kamishna wa Polisi Zanzibar Mussa Alli Mussa
alisema watu hao walikamatwa kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema na
ndipo walipowakamata na katika mahojiano ya awali watuhumiwa hao
walikiri kuwa na bastola wanayoimiliki isivyo halali.
Kamanda
Mussa, aliwataja watu hao kuwa ni Alli Mwanasai (40) mkazi wa Mbagala
Dar es Salaam, Mohamed Said Mohamed (32) na Miraji Mohamed Rashid (40)
wote wakazi wa Bububu Kigamboni Zanzibar ambapo mpaka hivi sasa
wanaendelea kuhojiwa.
“Kutokana
na kukamatwa kwa bastola hii, tunaendelea kuwahoji watu hawa kwa kina
zaidi ili kubaini kama matumizi ya silaha hii ilihusika katika matukio
mbalimbali yaliyojitokeza hapa Zanzibar yakiwemo tukio la kuuwawa kwa
Padri Mushi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda ”Alisema Kamishna
Mussa.
Aidha,
Kamishna Mussa alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili kujua
washirika wao wengine, wakiwemo watu wanaowafadhili kwa kuwapa taarifa
zinazowawezesha kufanya uhalifu, watu wanaowapa usafiri kukamilisha
uhalifu huo na watu wanaowafdhili kwa pesa ili kutekeleza uhalifu huo.
Kamishna
Mussa amewahakikishia wananchi kwamba kutokana na juhudi kubwa za Jeshi
hilo wahalifu wote watakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Aidha,
ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wanaowashuku
kuhusika na vitendo vya uhalifu hasa katika kipindi hiki cha mwezi
mtukufu wa Ramadhani ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo
vya sheria.
Alisema
kuwa uzoefu unaonyesha kuwa katika kipindi cha mwezi mtukufu wa
Ramadhani baadhi ya makosa ya jinai huongezeka ikiwemo ajali za
barabarani , wizi wa kuvunja nyumba usiku, vipando kuibiwa pamoja na
wizi katika vituo vya mafuta hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini katika
kipindi hiki na kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi pindi
wanapobaini viashiria vyovyote vya kihalifu, taarifa hizo zitalisaidia
Jeshi la Polisi kudhibiti viashiria hivyo kabla uhalifu haujatendeka.