MMOJA
wa wafanyabiashara maarufu nchini, Dk Reginald Mengi amesema kwamba
huwezi kutofautisha watoa rushwa wakubwa na mlipuko wa dawa za kulevya,
ambayo kwa sasa yanatikisa nchi.
Dk
mengi ameyasema hayo wakati akizungumza moja ya vikwazo vikubwa vya
uwekezaji nchini katika mazungumzo ya sekta binafsi na umma kwenye
uzinduzi wa taarifa inayozungumzia uwekezaji nchini kwa jinsi unavyoonwa
na viongozi wa wafanyabiashara.
Katika
taarifa hiyo iliyofanyiwa utafiti na Sekta Binafsi kwa ufadhili BEST
AC, Programu iliyopo ofisi ya Waziri Mkuu, rushwa ni mojawapo ya vikwazo
vya uwekezaji nchini.
Ripoti
hiyo “Mitizamo ya viongozi wa biashara juu ya mazingira ya uwekezaji
Tanzania “ ambapo ripoti yake imezinduliwa Julai 11 mwaka huu katika
ukumbi wa Karimjee, changamoto hizo zinatakiwa kufanyiwa kazi mapema na
kwa kasi ili kuinusuru nchi.
Dk
Mengi alisema mfano mzuri wa fedha za rushwa kutumika kuimarisha
uingizaji wa mihadarati nchini au kuitoa ni kukamatwa kwa wasichana
wawili hivi karibuni wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya Sh
bilioni 6.8.
Alisema
mabinti hao hawana uwezo wa kupata fedha za kununulia mzigo wa thamani
hiyo na kusema kwamba kazi hiyo, inawezeshwa na watoa rushwa wakubwa
nchini ambao wanajulikana.
Alisema
taifa hili linasumbuliwa na watoa rushwa wanne wakubwa, ambao alisema
kwamba hatawataja, pamoja na kuulizwa kutakiwa kufanya hivyo na
Mwenyekiti wa kikao cha mazungumzo.
Dk
Mengi alisema kwamba mihadarati hiyo ni tatizo kubwa kwa taifa kwa
sasa, lakini inaweza kuondoka kama hatua za kijasiri za kuwakataa watu
hao zitachukuliwa na wala isiwe kuwepo kwa utashi wa kisiasa pekee
wakati uwajibikaji haupo.
“Taifa likubali kutengana na watoa rushwa wakubwa haraka na mara moja na taifa litaendelea kuishi,” alisema Dk Mengi.
Dk
Mengi alisema yeye ni mmojawapo wa watu wa Tanzania, walioumia katika
rushwa kwani amepoteza miradi miwili mikubwa kwa sababu hiyo.
Hata
hivyo, alisema kwamba Watanzania wenyewe hawapendani na kukaripia
matukio ya rushwa kwani hata alipolalamika kuhusu Hoteli ya Kilimanjaro,
yupo mtu aliyeuliza kwanini Mengi anataka kushika kila kitu.
Dk
Mengi ambaye alisema kwa uchungu juu ya tatizo la rushwa na mihadarati
alisema kwamba mwishoni anayeumia ni mtu wa kawaida hasa masikini.
“Tukiachia
hivi watu hawa watakamata nchi,...taifa litatawaliwa na mtu ambaye
humjui,” alisema Dk Mengi na kuongeza kuwa watu hao watakuwa na uwezo wa
kufanya kila kitu wanachotaka. Alisema Tanzania ikiwa miongoni mwa
mataifa 14 yanayosifika kwa rushwa, wananchi wake ni lazima kuamka na
kushiriki katika vita hiyo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Godfrey Simbeye
alisema kwamba wakati umefika wa kuweka sawa uwekezaji na kutilia
maanani programu ya kitaifa ya maendeleo kwa kushirikisha kikamilifu
sekta binafsi.
Aidha aliitaka Serikali kurejesha mazungumzo kati yake na sekta binafsi, ambayo mara ya mwisho yalifanyika mwaka 2009.
Mazungumzo
hayo kwa kawaida Mwenyekiti wake ni Rais wa nchi. Taarifa hiyo ina
mambo matano ambayo yameelezwa kuwa kikwazo cha uwekezaji.
Mambo
hayo pamoja na rushwa tatizo la upatikanaji wa umeme wa uhakika, kodi
na tozo nyingine, Menejimenti ya Kodi na ugumu wa taasisi za fedha
kuwezesha wajasiriamali.