SERIKALI ya Tanzania imeipa onyo kali nchi ya Rwanda ikiitaka isijaribu
kuota ndoto za kuishambulia kijeshi, vinginevyo itajibu mapigo kwa nguvu
zote na kuhakikisha kuwa imeichakaza.
Kauli hiyo ya kwanza nzito imetolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje ya
Ushirikiano wa Kimataifa kufuatia taarifa ya matamshi makali yanayodaiwa
kutolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda, dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na
kutishia kuishambulia Tanzania.
Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa
wizara hiyo, Mkumbwa Ally, alisema ingawa Serikali ya Tanzania hadi sasa
inajua haina ugomvi wowote na Rwanda, lakini amekiri kuwapo kwa kile
alichokiita ‘kupishana lugha’ kwa Rais Jakaya Kikwete na Paul Kagame.
Mkumbwa alikiri Serikali ya Tanzania kunasa matamshi yanayodaiwa
kutolewa na Rais Kagame katika moja ya hotuba zake aliyoitoa Juni 30,
nchini kwake wakati akihutubia katika hafla moja ya vijana.
Kwa mujibu wa hotuba hiyo, ambayo kwa wiki sasa imesambazwa katika
baadhi ya mitandao ya kijamii, Kagame anadaiwa kusikika akitoa matamshi
ya vitisho dhidi ya Rais Kikwete, kwamba anamsubiri katika wakati aujuao
na kumchapa.
Baadhi ya maneno yanayodaiwa Rais Kagame aliwaambia vijana waliokutana
katika mkutano wao uliojulikana kama ‘Youth Konnect’ na kufadhiliwa na
mke wake, Janet Kagame, yanasema: “Huyu mtu mliyemsikia akiwa upande wa
Interahamwe na FDLR na akashauri majadiliano….majadiliano?”
Aidha, Kagame anadaiwa kusema kuwa hatakuwa tayari kujadili jambo hilo,
isipokuwa atamsubiri Rais Kikwete sehemu muafaka na ‘kumtandika’.
“Sitapoteza muda wangu kumjibu Kikwee, inajulikana maana kuna mahali
hataweza kuvuka…haiwezekani,” alikaririwa akisema Rais Kagame, akilenga
kumtisha Rais Kikwete.
Mbali na Kagame, baadhi ya viongozi kadhaa wa serikali ya Rwanda
wamekuwa wakimshambulia Rais Kikwete wakimpachika majina ya kejeli ya;
“Rais mhurumia magaidi, wauaji wa kimbari, mkorofi na mwenye dharau.”
Mkumbwa hata hivyo alisema Serikali ya Tanzania haina sababu ya kuingia
katika vita na Rwanda, kwa sababu tu ya ushauri alioutoa Rais Kikwete wa
kuitaka ikutane na wapinzani wake wanaoishi ndani ya nchi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), kujadiliana kuhusu amani ya nchi za Maziwa
Makuu.
Alisema msimamo wa Tanzania utabaki kuwa uleule wa kuitaka nchi hiyo
ikubali kukaa meza moja na wapinzani wake, ili kumaliza migogoro
inayoendelea katika nchi hizo za maziwa makuu, ambao unaungwa mkono na
jumuiya ya kimataifa na SADC.
“Unajua mgogoro wa DRC na Rwanda hauwezi kumalizika bila ya nchi hizo
kukaa meza moja na wapinzani wao ili kupata suluhu ya kudumu,” alisema
Mkumbwa.
Aliwataka Watanzania kuwa watulivu na kuendelea na kazi zao kama
kawaida, kwani serikali yao iko makini katika kulinda mipaka yake.
Chanzo cha mzozo
Msuguano baina ya nchi hizi mbili ulianza siku chache tu baada ya
kumalizika kwa kikao cha viongozi wa nchi za Maziwa Makuu na ambacho
kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, chini
ya uenyekiti wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.
Rais Kikwete wakati akimtaarifu Rais Museveni kile walichokuwa
wamekijadili katika kikao hicho kwa vile aliketi kwa muda kwa kuwa
alichelewa kuwasili, alisema ni vema serikali za Rwanda na Uganda
zifungue mlango wa mazungumzo na waasi wao na akaanza kutaja majina ya
vikundi vya uasi vya nchi hiyo vilivyopo nchini DRC.
Habari zinasema kauli ya Rais Kikwete iliungwa mkono na Rais Museveni akisema: “Bila mazungumzo hatutafika popote pale”.
Hata hivyo, matamshi hayo yalijibiwa kwa ukali na serikali ya Rwanda,
kiasi cha kumlazimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, kutoa tamko bungeni.
Kwa kauli yake, Membe alisema serikali ilikuwa imeshangazwa na shutuma
hizo za Rwanda kwani halikuwa jambo baya kutoa ushauri uliolenga kuleta
mapatano na kuepusha umwagaji zaidi wa damu wa wananchi.
Akaongeza kuwa, ilikuwa ni wajibu wa Serikali ya Rwanda kuupokea ama kuukataa, na wala si kutoa maneno ya kejeli na vitisho.
Kauli ya Zitto
Akizungumzia kauli hiyo ya vitisho, mwanasiasa machachari hapa nchini na
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto
Kabwe, alisema ushauri wa Rais Kikwete kwa Rwanda ulikuwa wa busara mno
na akashangaa kuona nchi hiyo jirani ikitoa vitisho, kejeli, dharau na
ukosefu wa adabu kwa Kikwete.
Katika moja ya tamshi lake alilolitoa jana katika mitandano ya kijamii,
Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) alisema Marekani
wanaongea na waasi wa kundi la Taliban, hivyo hakuna dhambi kwa Rwanda
pia kufanya hivyo.
“Pia kama hutaki ushauri si unakataa tu, sasa kuanza kurushiana maneno ya nini tena? Hutaki ushauri basi.
Maneno ya kila siku ya nini? Tangu Kikwete amesema kule Addis, hajasema
tena. Membe (waziri) akajibu Dodoma Tanzania haijasema tena. Kigali
inasema mambo haya kila siku kwa ajili ya nini?
“Taliban na Al Qaeda si wale wale? Wale watoto waliozaliwa mwaka 1994 na
wakimbizi wa Kihutu waliopo Kongo nao ni wauaji? Tufikiri vizuri mambo
haya. Kuna ‘genociders’ wasakwe, wakamatwe wahukumiwe. Kuna watu wana
haki kabisa ya kutaka kushiriki kwenye siasa za Rwanda na wanazuiwa,
wameshika silaha. Hawa lazima wakae meza moja wakubaliane,” alisema
Zitto.
Mwanasiasa huyu alisema kwa sasa serikali za nchi hizo mbili zinatakiwa
kuingia katika vita ya kupambana na kuondoa umasikini wa watu wake na si
vita ya mtutu wa bunduki.
“Busara itumike kwa viongozi ‘neutral’ kama Uhuru Kenyatta kuwaweka
pamoja Kagame na Kikwete wamalize tofauti zao. Haya maneno hayana maana
yoyote,” alisema.
Alisema vita haitamuumiza Rais Kagame wala Rais Kikwete na familia zao,
bali itaumiza wananchi wa kawaida wa mikoa ya Kagera na Kigoma na mikoa
ya mpakani ya Rwanda.
“Vita itaturudisha nyuma sana kwenye juhudi za maendeleo. Vita itazima
harakati za kujenga demokrasia nchini. Busara itumike tu,” alisema
Zitto.
TANZANIA DAIMA