Matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2012, yameendelea kuitikisa
sekta ya elimu nchini baada ya shule kufunguliwa jana bila kutangazwa
kwa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.
Kwa
kawaida, wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo
vya ualimu, hutangazwa mapema ili kutoa fursa kwa wanafunzi na shule
husika kufanya maandalizi ya mahitaji.
Lakini
tofauti na ilivyozoeleka, wanafunzi wa kidato cha sita walianza masomo
yao jana huku wale wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya
ualimu wakiwa hawajatangazwa.
Mkanganyiko
huo pia unazigusa shule za sekondari za binafsi kwani baadhi
zilishachukua wanafunzi wa kidato cha tano na nyingine ziliahirishwa
kufunguliwa jana kutokana na kutokuwa na wanafunzi hao.
Hali hiyo
imewaacha njia panda baadhi ya wakuu wa shule ambao waliwaambia
waandishi wetu kwa nyakati tofauti kwamba wanasubiri maelekezo ya Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu suala hilo, huku wengine
wakitishia kufunga shule hizo na kuzigeuza kuwa vyuo vya taaluma
nyingine.
Akitangaza
matokeo mapya ya kidato cha nne Mei mwaka huu, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa aliahidi kwamba majina ya
watakaojiunga na kidato cha tano yangetangazwa mapema ili wapate muda wa
kujiandaa na kuripoti kwenye shule husika mapema kadri
itakavyowezekana.
Jana,
Dk Kawambwa hakupatikana kuzungumzia suala hilo na msemaji wa Wizara
hiyo, Bunyanzu Ntambi alisema suala la kutangaza majina hayo lipo kwenye
ngazi za uamuzi. NA MWANANCHI
“Sababu hasa siwezi kujua, lakini kwa kuwa matokeo yenyewe
yalichelewa kutangazwa ni rahisi hata mchakato wa kutangaza
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano uchelewe,” alisema Bunyanzu.
Wakuu wa shule
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Morogoro, Thomas Chihwalo alisema: “Ninachosubiri ni maelekezo ya wizara, nini kifanyike.”
Mkuu wa Sekondari ya Azania, Dar es Salaam, Benard Ngoyaye
alipoulizwa alisema: “Nenda kwa Ofisa Elimu wa Wilaya, yeye anafahamu
kwa nini majina yamechelewa kufika wakati walikwishachaguliwa.”
Mkuu wa Shule ya Sekondari Arusha, Christopher Malamusha alisema
walitarajia wizara ingetangaza majina hayo mapema lakini hadi jana
walikuwa hawajapokea taarifa zozote.
Mkuu wa Sekondari ya Tambaza aliyejitambulisha kwa jina moja, Zuberi
naye alisema wanasubiri maelekezo ya Ofisa Elimu Wilaya ya Ilala.
Hata hivyo,
Ofisa Elimu ya Sekondari wa Manispaa ya Ilala, Germana Mng’aho alisema
asingeweza kuzungumzia suala hilo na kwamba mhusika mkuu ni Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ilboru, Arusha, Julius Shula alisema
hata majina ya wanafunzi wanaojiunga na shule yao hawayafahamu.
Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani, Dar es Salaam,
alisema kwa kawaida wanafunzi wa kidato cha tano huripoti shuleni wiki
mbili kabla ya wale wa kidato cha sita kitu ambacho mwaka huu kimekuwa
tofauti.
Msaidizi wa Mkuu wa Shule ya Sekondari Bwiru Wavulana ya Mwanza,
Malongo Charles alisema wanasubiri wanafunzi watakaopelekwa na Serikali.
Hata hivyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Moshi, Fanuel Angalo alisema anaamini wizara husika itatangaza wiki hii.
“Ni jambo jipya kidogo limetokea lakini tunaamini Waziri atatoa
tangazo lake wiki hii halafu wanafunzi hao wa kidato cha tano waripoti
shuleni wiki ijayo,” alisema Angalo.
Mkoani Tanga, walimu katika Shule za Sekondari za Tanga Ufundi,
Gallanos na Usagara kwa nyakati tofauti, waliilalamikia wizara kwa
kuwachelewa kuwapelekea wanafunzi wa kidato cha tano na kusema kuwa hiyo
imevuruga utaratibu wa ufundishaji.
Hakuna athari
Baadhi ya
wadau wa elimu walisema kilichotokea si kigeni kwani kimepata kutokea
miaka ya nyuma na mihula ilirekebishwa na kwenda sawa na wenzao ambao
walikuwa wameanza masomo.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Ushauri wa HakiElimu, Nyanda Shuli
alisema kubadilika kwa muhula wa kuanza masomo si jambo kubwa ambalo
linaweza kuathiri elimu na kwamba anaamini wizara itakuwa imetoa
mwongozo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Kitila
Mkumbo alisema si mara ya kwanza kwa muhula wa masomo kubadilika kwani
imewahi kutokea siku za nyuma na marekebisho yakafanywa ili kufidia muda
ambao wanafunzi wanakuwa wamepishana na wenzao.
“Sidhani kama ni jambo kubwa sana ambalo linaweza kuathiri chochote
katika masuala ya elimu, la msingi ni kuhakikisha kuwa waliochelewa
kuanza masomo wanapata muda wa kumaliza mtaala (mtalaa) wa masomo kama
inavyotakiwa.”
Kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Juni 29, mwaka huu, wakuu wa shule
za sekondari za Serikali walikutana katika Chuo cha Ufundi, Arusha
kupitia majina ya waliochaguliwa na kuiachia kamati ya kukamilisha kazi
hiyo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema tatizo kubwa
lilikuwa ni idadi ya wanafunzi kuwa ndogo ikilinganishwa na nafasi za
kidato cha tano kutokana na kufeli kwa wanafunzi wengi katika matokeo ya
kidato cha nne, 2012.
Hata baada ya matokeo hayo kufanyiwa marekebisho, idadi ya wenye sifa za kuchaguliwa ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.
Mara nyingi, wanafunzi walio katika nafasi kubwa ya kuchaguliwa
kujiunga na masomo ya kidato cha tano ni wale waliofaulu kwa daraja la
kwanza mpaka la tatu.
Kwa sasa shule za Serikali zenye kidato cha tano zina uwezo wa kuchukua wanafunzi 45,000 kwa wakati mmoja.
Baada ya matokeo ya kidato cha nne kurekebishwa, wanafunzi waliofaulu
kwa daraja la kwanza mpaka la tatu ni 35,349; daraja la kwanza ni
3,242, daraja la pili ni 10,355 na daraja la tatu ni 21,752.
Ikiwa wanafunzi hao wote watachaguliwa kujiunga na kidato cha tano,
bado shule hizo zitakuwa na upungufu wa zaidi ya wanafunzi 9,000.
Upungufu huo hautakuwa na athari kwa shule hizo pekee, bali hata kwa
vyuo vya ualimu na vile vya kati ambavyo hupokea wanafunzi waliohitimu
kidato cha nne na kufaulu.
Mwaka jana, wanafunzi 31,516 walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule 201 za Serikali.
Idadi hiyo ni karibu asilimia 60 ya shule 495 ambazo kwa mujibu wa
takwimu za Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), zilifanya mitihani ya
kidato cha sita mwaka huu. Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa idadi ya
watahiniwa wa shule waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 43,231.
Kwa maana hiyo, ikiwa shule za Serikali zitachagua idadi sawa na ile
ya mwaka jana, (31,516) kwa ajili ya kujiunga na kidato cha tano, shule
binafsi 294 zitalazimika kugawana wanafunzi 3,833 watakaobaki.
Shaka ya wadau
Kutokana
na idadi ya wanafunzi wanaofaulu mtihani wa kidato cha nne kuendelea
kushuka kila mwaka, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo
Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema asilimia 70 ya
shule zenye kidato cha tano zimefungwa ama kupunguza idadi ya wanafunzi.
Mringo alisema matokeo ya hali hiyo yanaonekana kwenye yale ya kidato
cha sita yaliyotangazwa Mei 31, mwaka huu ambayo baadhi shule kongwe
zilizokuwa zinafanya vizuri miaka ya nyuma, zilishika nafasi za mwisho
akisema hali hiyo imekuwapo kwa miaka minne mfululizo.
“Shule za private (binafsi) asilimia 70 ama wamefunga au wamepunguza
udahili wa wanafunzi, kwa ufupi wameanza kujitoa kwenye hii bishara ya
shule, shule kama ya Green Acres na St. Mary’s kushika nafasi za mwisho
ni kiashirio cha kuwa walishaanza kujitoa kwenye hiyo biashara,”
alisema.
Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya Raida, Profesa Ruth Meena alisema
wameamua kutochukua tena wanafunzi wa kidato cha tano kuanzia sasa na
baada ya walio kidato cha sita kuhitimu, wanafikiria kuifanya taasisi
hiyo kuwa chuo.
Meneja wa shule hiyo, Anneth Meena alisema: “Kila mwaka idadi ya
ufaulu inashuka na wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano
wanakosekana, sisi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu walikuwa ni
ishirini na kitu na wanaoingia kidato cha sita sasa hivi ni 21.”
Alisema wakati hali ikiwa hivyo miundombinu ya shule hiyo yenye
kidato cha tano na sita pekee ina uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya
400.
Hofu vyuo vikuu
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala
alisema kwa jinsi hali ilivyo siku zijazo kutakuwa na upungufu mkubwa wa
wanafunzi wenye sifa za kwenda vyuo vikuu.
Alisema kutokana na matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012, alitegemea
kuona bajeti ya elimu kwa mwaka 2013/14 inajielekeza kutatua matatizo
yanayojulikana na yale yatakayoainishwa na Tume ya Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, kitu ambacho hakijafanyika.
“Nilitegemea resources (rasilimali) nyingi zingeelekezwa kwenye
kutatua matatizo ya elimu yanayojulikana na yale yasiyojulikana, lakini
bajeti ya elimu ni ndogo kama miaka mingine, wakati ya Kenya ikiwa ni
asilimia 18 na Uganda ikikaribiana na hiyo kwetu ni asilimia 10,”
alisema na kuongeza:
Msemaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Edward Mkaku alisema
kufeli kwa wanafunzi wengi ngazi za shule siyo sababu ya kufanya vyuo
hivyo vifungwe kwani taasisi hizo zina kazi kuu tatu ambazo ni
kufundisha, kufanya utafiti na kushauri.
Alisema pia kuwa, TCU imeanzisha programu mbalimbali ikiwa ni pamoja
na kuruhusu hata watu walioishia darasa la saba na kufanya kazi muda
mrefu kwenye maeneo mbalimbali kujiunga na vyuo vikuu.
“Kuna mtu alimaliza darasa la saba na akaenda kusoma cheti cha
sheria, huyu mtu kafanya kazi kama karani wa Mahakama ya hakimu mkazi
kwa miaka minane, huyu mtu ukimwingiza kusoma sheria na mwanafunzi
aliyetoka kidato cha sita lazima afanye vizuri zaidi,” alisema.