MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, imesema haina uwezo wa kusikiliza kesi
ya ugaidi inayowakabili makada watano wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema). Makada hao wanakabiliwa na shitaka la ugaidi,
ambapo Juni 24, mwaka huu, waliachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya
Igunga, kisha na wakakamatwa kwa tuhuma za kummwagia tindikali kada wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Tesha, katika uchaguzi mdogo wa Jimbo
la Igunga, Mkoa wa Tabora, uliofanyika mwaka 2011.
Katika
kesi hiyo, watuhumiwa ni Evodius Justunian (30), mkazi wa Bukoba, Oscar
Kaijage, mkazi wa Shinyanga, Seif Magesa wa jijini Mwanza na Rajabu
Daniel, mkazi wa Dodoma.
Watuhumiwa hao, walipokamatwa walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya
Igunga, kabla ya Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo
kukamatwa na kuunganishwa kwenye kesi hiyo.
Akitoa
uamuzi huo jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Tabora, Issa Magoli, alisema mahakama hiyo haina uwezo kisheria wa
kusikiliza shauri hilo ambapo aliliahirisha hadi Julai 22, mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Magoli, aliwashauri mawakili wa upande wa
utetezi, kuwasilisha hoja zao Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kuwa huko
ndiko kunakoweza kupatiwa ufumbuzi wa kisheria wa shauri hilo.
Katika shauri hilo, washitakiwa hao walifunguliwa kesi mbili katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tabora, baada ya kesi ya awali ya
kudhuru mwili kwa tindikali kufutwa na kufunguliwa kesi ya ugaidi dhidi
ya makada hao wa Chadema.
Awali, katika shauri hilo yalizuka mabishano ya kisheria kati ya
mawakili wa upande wa utetezi, wakiongozwa na Peter Kibata na Profesa
Safari, huku upande wa Serikali ukiongozwa na Wakili Juma Masanja na
Edifonce Mkandala.
Wakati wa mabishano hayo, mawakili wa upande wa utetezi waliomba
Mahakama ifute kesi hiyo, kwa kile walichosema kuwa ni batili kutokana
na baadhi ya vifungu vya sheria kukiukwa, huku mahakama hiyo ikiwa haina
uwezo wa kuisikiliza isipokuwa Mahakama Kuu peke yake.
Mawakili hao walisema kuwa, washitakiwa walikamatwa sehemu tofauti,
hivyo kesi zao zilipaswa kusikilizwa katika maeneo waliyokamatiwa badala
ya kusikilizwa katika eneo moja.
Ulinzi mahakamani
Kabla ya washtakiwa hao kufikishwa mahakamani, Jeshi la Polisi mkoa hapa
liliimarisha ulinzi katika eneo la mahakama ambapo ilipotimu saa 4
asubuhi, walifikishwa wakiwa katika gari la Polisi lenye namba za
usajili PT 1816, huku wakiongozwa na askari wa kutuliza ghasia FFU.
Chanzo - Mtanzania