Rais Barack Obama wa Marekani.
NDUGU zangu tumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuiona siku hii ya leo, hakika ni mwema kwetu.
Baada
ya kusema hayo leo najadili kuhusu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
kwamba tangu lilipoanzishwa kwa sheria ya Bunge mwaka 1964 halijawahi
kuwa na rekodi ya utendaji kazi wa kujivunia.
Hii
hakuna anayebisha kwani kwa miaka 49, shirika hilo lingekuwa ni mtu
tungesema limekuwa likiishi katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Mbaya
zaidi ni kwamba shirika hili limekuwa likiugua huku ‘madaktari’ wake
yaani wataalamu wanaoliongoza wengine wakiwa wamesomea nje ya nchi
lakini wameshindwa kubaini ugonjwa.
Kwa
miaka yote hiyo 49 hakuna mtu ambaye ameweza kutegua kitendawili
kuhusu faida inayopata serikali yenye asilimia 100 ya umiliki kwa
kuendelea kulikumbatia shirika hilo na matokeo yake ni wananchi kuumia
kwa tozo kubwa ya umeme.
Mwaka jana walipoteuliwa
mawaziri wapya kuiongoza Wizara ya Nishati na Madini, wananchi wengi
walipata matumaini makubwa, kwani Waziri Dk. Sospeter Muhongo na naibu
wake George Simbachawene walionyesha ari kubwa ya kulibadilisha shirika
hilo lililokuwa limeoza kutokana na vitendo vinavyodaiwa kuwa ni vya
rushwa na ufisadi, kuwa shirika lenye ufanisi likiwa na watumishi
wachapakazi wenye ari na uadilifu wa hali ya juu.
Ajabu ni kwamba shirika
limeanza tena mbinu chafu za kujihujumu lenyewe kwa kushindwa kusambaza
umeme kwa visingizio visivyokuwa na vichwa wala miguu. Nimepata
malalamiko ya watu lukuki wakilalamikia kucheleweshewa kupatiwa umeme
sehemu mbalimbali nchini.
Rais Barack Obama wa
Marekani wiki iliyopita alipotembelea Tanzania alitoa ahadi lukuki
lakini ambayo imewafurahisha wengi ni ya kuboresha umeme nchini mwetu na
nyingine saba katika Afrika.
Alitangaza mpango wa
uzalishaji wa umeme wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 7 katika
nchi hizo licha ya kuwa na mpango wa kukinga ukimwi wenye thamani ya
dola bilioni 4.2 pamoja na msaada unaolenga kuimarisha usalama wa
chakula wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 140.
Kubwa ambalo ni dhahiri ni
kwamba Rais Obama, alisema Afrika itajengwa na Waafrika wenyewe na
kwamba nchi kubwa kama Marekani inasaidia kuchochea maendeleo na
kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.
“Hatutaki kusambaza umeme
bali tunafanyakazi kwa karibu na serikali pamoja na wadau muhimu
kuangalia sheria na miongozo itakayosaidia sekta binafsi kuwekeza
zaidi...,” alisema Obama wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari
Ikulu Dar.
Alisema Tanzania pia
itanufaika na mpango wa Marekani wa ‘Power Africa’ ambao umetengewa dola
bilioni saba kwa ajili ya kuufanikisha. Obama hakumung’unya maneno
alisema lengo ni kuibua fursa za uwekezaji na biashara kwa kuhakikisha
nishati ya uhakika inapatikana kwa ajili ya kuendesha viwanda.
Lililowafurahisha watu ni
pale aliposema kuwa mkakati huo unalenga kuwapatia Watanzania na
Waafrika umeme wa uhakika na kwa bei nafuu na wananchi walifurahi
kutokana na nishati hiyo kuwa ghali sana katika nchi yetu.
Ndugu zangu, wananchi
wamelalamika sana kuhusiana na bei ya umeme nchini lakini kilio chao
kimekuwa kama cha samaki katika maji, machozi hayaonekani! Obama baada
ya kuja nchini alikwenda kutembelea mitambo ya Kampuni ya Symbion. Hii
ni mitambo ambayo miaka 4 iliyopita ilipigiwa kelele bungeni kuwa ni
chakavu, Tanesco wakakatazwa kuinunua badala yake kampuni hiyo ya
Kimarekani ikainunua, wakaingia mkataba na Tanesco kuwauzia umeme
unaozalishwa na mitambo hiyohiyo iliyokejeliwa.
Wakati tunasuburi kulipa
takriban shilingi 105 bilioni kwa Dowans baada ya kutubwaga kwenye kesi,
tulishuhudia Obama akienda katika mitambo ile ‘chakavu’ na viongozi wa
serikali yetu! Sisi watu wa kawaida tunajiuliza tena kimoyomoyo,’Si
walisema mitambo hii ni chakavu?’
Naamini bado kitambo kidogo
suala la nchi kuingiza gizani itakuwa ni historia kwani tumeambiwa
kampuni kubwa ya kutengeneza mitambo ya kuzalisha umeme ya GE imetangaza
kuingia ubia na Kampuni ya Symbion kuzalisha umeme nchini na takriban
400MW zitazalishwa kutoka Mtwara na kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Nishati naona ni kipaumbele
kikubwa sana kwenye ziara aliyoifanya Obama nchini. Kwa nchi kama yetu
yenye watu asilimia 21 tu wenye umeme, ni dhahiri kipaumbele hiki
kimeungwa mkono. Hata hivyo, Obama ni lazima asimame kidete kuhakikisha
kuwa kampuni za nchini mwake zinazopata mikataba hapa nchini ziweke wazi
mikataba hiyo na kulipa kodi inavyostahili.
Uwazi wa mikataba na uwezo
wa kupambana na ukwepaji kodi ni muhimu sana katika vita dhidi ya
ufisadi na ubadhirifu, uzalishaji ukianza mapato yao na kilicholipwa kwa
serikali ni vema viwe vinawekwa wazi na hilo naomba Obama mwenyewe
ayasisitize makampuni ya nchini mwake yanayokuja kuwekeza hapa kwetu.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.