STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 16.7.2013
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed
Shein, pamoja na wananchi wa Zanzibar wamepata mshtuko na huzuni kubwa
kwa vifo vya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi wa Watanzania walioshambuliwa
na kuuawa wakati walipokuwa wakilinda amani katika eneo la Darfur,
nchini Sudan.
Dk.
Shein ameelezea kusikitishwa kwake na vifo hivyo na kueleza kuwa
inasikitisha zaidi kuwa wanajeshi hao wamekufa wakiwa katika kazi ya
kulinda amani nchini humo na kueleza kuwa wao ni mashujaa na wamekufa
kishujaa.
Hayo
yalielezwa katika salamu zake za rambi rambi alizotuma Dk. Shein kwa
Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananachi wa Tanzania, Jenerali Davis Adolf
Mwamunyange pamoja na wanajeshi wote, pia, salamu hizo zilitoa pole kwa
familia za wafiwa.
Aidha,
salamu hizo alizozituma Dk. Shein zilieleza kuwa huu ni msiba wa Taifa
lote na wananchi wote wa Zanzibar wanaungana pamoja katika kuomboleza
msiba huo.
“Tunatoa
pole na tunamuomba MwenyeziMungu aziweke pahala pema peponi roho za
mashujaa hao, vile vile tunawatakia nafuu ya haraka majeruhi wote wa
tukio hilo”.
Alisisitiza
Dk. Shein “ Mwenyezi Mungu akupeni moyo wa subira na ustahamilivu
katika kipindi hiki cha msiba mkubwa”. zilieleza salamu hizo za
rambirambi
Dk.
Shein pamoja na wananchi wa Zanzibar wanaungana na Watanzania wenzao
kuwaombea wale wote walioumia katika tukio hilo ili waweze kupona kwa
haraka na kuendelea na majukumu yao ya ulinzi wa amani.
Vijana saba wa Jeshi la Wananachi wa Tanzania waliuawa baada ya kushambuliwa na waasi wa Sudan na wengine walijeruhiwa.
Wanajeshi
hao wa Tanzania waliopoteza maisha yao pamoja na wale walioumia
walikuwa ni sehemu ya askari 37 na ofisa mmoja ambao walikuwa
wanasindikiza msafara wa waangalizi wa kijeshi katika eneo la Darfur.
Katika
suala la ulinzi wa amani katika eneo hilo la Darfur, Wanajeshi kutoka
Tanzania wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya ulinzi tokea pale Tanzania
ilipoanza kuchangia walinzi katika eneo hilo mnamo mwaka 2007, ambapo
vijana hao waliouawa ni miongoni mwa vijana waliokwenda nchini humo
Februari mwaka huu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar