Dawa za
kulevya ni janga la taifa katika nchi yetu na sijaona mikakati yoyote
ikifanywa na vyombo vya dola kwa kushirikiana na wananchi wema
kuhakikisha tatizo hili linakuwa historia nchini mwetu.
Wakati
umefika wa kila Mtanzania kutambua ubaya wa dawa hizi katika jamii na
wahusika kama vile polisi, mahakimu, majaji, waendesha mashitaka na
wananchi kuhakikisha wanaohusika na uingizaji, usambazaji na
utengenezaji kama wapo nchini, wanafichuliwa na kufikishwa katika vyombo
vya sheria.
Kila idara kati ya hizo nilizozitaja, ikilegea inakuwa kama wametoa mwanya kwa dawa hizo kutapakaa nchini na kuathiri watumiaji.
Nakumbuka maadhimisho ya kitaifa ya ‘Siku ya Kupiga Vita Dawa za
Kulevya Duniani’ yaliyofanyika mwezi uliopita, Waziri Mkuu Mizengo Pinda
alitangaza kwamba tatizo la dawa hizo ni janga la kitaifa hivi sasa.
Akasema kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika
biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba,
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa
kwa kujihusisha na dawa hizo.
Pia alisema katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi
za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, kuharibu taswira ya nchi na
kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu
wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
Anasema mwaka huu pekee kumekuwa na ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya
katika eneo la kimataifa la Bahari ya Hindi karibu na nchini .
Ni wazi kuwa kauli hiyo ya Pinda inathibitisha dhahiri kuwa taifa
linakabiliwa na changamoto kubwa ya kudhibiti tatizo la dawa za kulevya.
Ninachosema ni kwamba vita bado ni ngumu kutokana na wanaoendesha
biashara ya dawa hizo kuwa na fedha za kutoa rushwa kwa lengo la kuzuia
kukamatwa.
Kutokana na hali hiyo, hivi sasa biashara hiyo inaendelea kusambaa na
kwamba, tayari imeshabisha hodi hadi shuleni, kwa wasanii, wanamuziki na
hata kwa wachezaji wa michezo mbalimbali.
Nilishituka Waziri Mkuu Pinda aliposema kuwa hivi sasa mikate, maandazi
na askrimu zinazouzwa kwenye shule za msingi, zinawekwa dawa za
kulevya.
Akabainisha kuwa vitendo hivyo vinafanya vijana wengi wa shule za msingi
na hata sekondari kuwa na tabia za ajabu, ikiwamo kuingia darasani
wakiwa na kiatu kimoja mguuni, mkufu wenye nyembe na kidani chenye
nyembe kifuani.
Natoa wito kwa kusema vita dhidi ya matumizi na biashara haramu ya dawa
za kulevya inahitaji ushirikiano wa hali ya juu kwa Watanzania wote bila
kujali itikadi.
Polisi wafanye kazi yao, mahakama nayo ifanye kazi yake sawasawa kwani
kuna taarifa kuwa kesi za dawa za kulevya nchini ni chache sana
zinazoisha; Nyingi zipo mahakanani, zinakwamishwa na nini?
Dunia nzima inapiga marufuku dawa za kulevya kwa sababu huchangia makosa
mengi kutendwa kama vile wizi, uporaji, ukabaji na hata ujambazi na
watumiaji kuharibikiwa akili, hivyo kupoteza nguvu kazi ya taifa.
Kwa hiyo vita dhidi yake ni wajibu wa kila mtu.
Cha kusikitisha na kuhuzunisha ni kwamba, mara zote vinapotajwa vikwazo
vinavyokwamisha vita dhidi ya dawa za kulevya, kiini hasa cha tatizo
huwa hakiguswi kabisa!
Kiini hicho si kingine, bali ni unafiki, wanakamatwa watu wadogowadogo
sana na mapapa hawapo, asili ya matumizi ya dawa za kulevya haisemwi!
Kwamba ni unywaji wa pombe.
Kabla ya dawa za kulevya hazijagunduliwa, wanywaji walikuwa wakinywa pombe ya kawaida.
Pombe ya kawaida ilipoonekana inachelewesha lengo la mnywaji,
ikatengenezwa gongo, na kadhalika. Pombe kali ilipoonekana inachelewesha
lengo, ndiyo sasa zikavumbuliwa dawa za kulevya. Lengo likiwa lilelile,
kuharakisha kulewa. Huo ndiyo ukweli, ambao watu hawataki kuusema.
Baadaye watu wakaunda usemi kuhalalisha ulevi eti kuna kuna pombe haramu na pombe halali!
Tujiulize, lengo la mnywaji wa gongo lina tofauti gani na lile la
mnywaji wa wiski? Tunajua kuwa pamoja na manufaa ya kiuchumi yaliyomo
kwenye biashara ya pombe, madhara yake (pombe) ni makubwa sana kwa jamii
na moja ni hili la vijana kutumia dawa za kulevya. Kwa kuwa kuna ugumu
wa kuzuia na kupiga vita unywaji wa pombe, vita dhidi ya dawa za kulevya
kamwe haitafanikiwa.
Haitafanikiwa pia kama wenye mamlaka au jamaa zao wataendelea kuwa
sehemu ya dawa za kulevya, pia ikiwa vyombo vinavyohusika na mapambano
vitakabiliwa na tatizo la rushwa.
Wito
ninaoutoa ni kwamba, kesi zilizopo mahakamani zishughulikiwe na
ikiwezekana Rais Jakaya Kikwete aunde mahakama maalum ya kushughulikia
watuhumiwa wa dawa za kulevya ili kesi zisiwe zinachewa sana kama ilivyo
sasa.