Chama
cha Wananchi (CUF) kimesema kinawasilisha na mawakili wake na asasi za
haki za binadamu kujua hatua za kisheria kuchukua dhidi ya askari wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa madai ya kutekwa na kuteswa
Naibu Mkurugenzi wa CUF Taifa, Shaweji Mketo, na viongozi wengine wa
chama hicho Mkoa wa Mtwara.
Mpango huo
ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wake wa Taifa,
Profesa Ibrahimu Lipumba wakati akiongea na waandishi wa habari.
Prof. Lipumba alisema pia chama hicho kinawasiliana na mawakili hao
kujua hatua za kisheria za kuchukua dhidi ya Jeshi la Polisi kwa madai
ya kuwabambikia kesi viongozi hao ambao kimedai walikamatwa na kupigwa
na askari wa JWTZ katika kambi yao ya Naliendele.
Alisema pia wanawasiliana na asasi za kiraia zinazoshughulikia haki
za binadamu na haki za wanawake kumsaidia kisaikolojia mwanamke
anayedaiwa kubakwa na askari wa JWTZ mkoani humo na kufikishwa
mahakamani.
Lipumba aliwataja viongozi wengine wa CUF waliodaiwa kutekwa na
kuteswa kambini Juni 28, mwaka huu kuwa ni Salum Mohamed ambaye ni
Mwenyekiti wa CUF Mtwara Mjini,Ismail Jamal Mwenyekiti wa CUF Mtwara
vijijini.
Wengine ni Mwenyekiti wa Vijana Mtwara mjini, Ismail Njalu, Katibu wa
CUF Mtwara mjini, Said Kulaga na Kashindye Kalungwana ambaye ni dereva
wa jeshi hilo makao makuu.
Alidai viongozi hao baada ya kutekwa na askari wa JWTZ walivuliwa
nguo zote na kulazwa kifudifudi, kumwagiwa maji ya baridi na kupakwa
chumvi kisha kuanza kupigwa usiku kucha kwa kutumia mikanda ya jeshi,
ngumi, mateke na fimbo maalum za ngozi za wanyama na miti maalum.
Alisema viongozi hao wakiwa njia kurejea Mtwara Mjini wakitokea
Msimbati magari mawili ya jeshi yaliziba barabara baada ya kuliona gari
la CUF na wanajeshi walianza kuwashusha na kuwapiga kisha kuwarusha
kwenye karandinga lao.
Alisema baadaye walipelekwa katika kambi ya Naliendele kabla ya
kuachiwa saa 5:00 usiku na kukabidhiwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mtwara.
“Kwa bahati mbaya Mketo alipigwa sana katika ubavu wake wa kulia
ambao amewahi kufanyiwa operesheni kubwa miezi kadhaa iliyopita,.
Alipoona anapigwa sana eneo hilo akaona awaombe askari wampige maeneo
mengine lakini eneo hilo wamhurumie, kusikia vile askari wale walimgeuza
kwa nguvu na kuanza kumpiga mateke ya nguvu zaidi katika eneo lile hadi
alipoteza fahamu,”alisema.
Alisema Mketo alipozinduka Juni 28, mwaka huu alijikuta ana dripu na hakuelewa ni ya nini na baadaye wanajeshi waliitoa.
Profesa Lipumba alisema tukio la utesaji raia ndani ya kambi ya jeshi
ikiliunganishwa na matukio mengine kama ya utesaji wa Dk.Stephen
Ulimboka , kutekwa nyara kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF),
Absalom Kibanda, kulipuliwa bomu katika mkutano wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) kunadhihirisha hatua za awali za kusambaratika
kwa dola.
Msemaji wa JWTZ, Kapambala Mgawe, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo
zinazoelekezwa kwa askari wa jeshi lake, alisema suala hilo linatiwa
chumvi na wanasiasa kwasababu kiutaratibu anayetekwa ni adui hivyo raia
wa Tanzania hawezi kutekwa na wanajeshi.
Mgawe alisema tuhuma zinazoelekezwa kwa wanajeshi zina lengo la
kutaka kulichafua jeshi hilo ili lisifanye kazi yake kwasababu vipo
vipengele vya kisheria vinavyoruhusu askari wa JWTZ kuliingilia kati
kudumisha amani kunapotokea Jeshi la Polisi limezidiwa.
Alisema katika kipindi hiki ambacho kuna vurugu nyingi zinajitokeza
katika nchini jeshi litakapokuwa linachukua hatua ya kudhibiti yatesemwa
mengi ikiwamo askari kuhusishwa na vitendo vya ubakaji