Naibu
waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani William Burns ambaye
amefanya ziara nchini Misri, amelitaka jeshi la Misri na viongozi wa
serikali ya muda, kuhakikisha kuwa mchakato wa kidemokrasia mnamo
kipindi hiki cha mpito unashirikisha wote. Burns ambaye ndiye afisa wa
kwanza wa ngazi ya juu wa Marekani kuitembelea Misri tangu mapinduzi ya
kijeshi yaliyomwangusha rais Mohamed Morsi, amekanusha shutuma kuwa
Marekani inaegemea upande mmoja katika mzozo wa kisiasa ulioigawa vibaya
nchi ya Misri.
Amefanya
mazungumzo na rais wa mpito Adly Mansour, waziri mkuu mteule Hazem
el-Beblawi, na kamanda mkuu wa majeshi Jenerali Abdel-Fattah el Sisi.
Maszungumzo hayo yalituama juu ya mpango mpya wa kidemokrasia
uliopendekezwa na uongozi wa sasa.
Mpango
huo unataka katiba iliyoandikwa na vyama vya kiislamu chini ya utawala
wa Morsi ifanyiwe mabadiliko, na kisha uchaguzi wa bunge na rais
ufanyike mapema mwaka kesho. Hadi sasa udugu wa kiislamu umekataa
katakata kushiriki katika mchakato wa sasa wa kisiasa, ukisema hautaki
kuhalalisha mapinduzi yaliyomng'oa Morsi madarakani.