Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Thursday, July 18, 2013

Bodaboda waibua vurugu Dar

Baadhi ya vijana wanaofanya huduma ya usafiri maarufu kama boda boda wakiwa wamepaki Pikipiki zao.
*********
Vurugu kubwa zilizohusisha madereva wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 100 wa pikipiki, maarufu kama ‘bodaboda’, jana zilizuka katika maeneo ya Ubungo River Side na katika Kituo cha Polisi Magomeni Usalama, jijini Dar es Salaam na kusababisha askari wa Jeshi la Polisi kutumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya.

Vurugu hizo ambazo zilidumu kwa zaidi ya saa moja, kabla ya askari polisi kuzidhibiti, zilisababisha taharuki kubwa miongoni mwa watu mbalimbali, wakiwamo wafanyabiashara, wafanyakazi maofisini, wasafiri na wapita njia katika maeneo hayo.

Madereva hao walizua vurugu hizo wakipinga operesheni iliyoendeshwa na maofisa wa Kampuni ya Yono Auction Mart, ya jijini Dar es Salaam, kuwakamata kwa kosa la kutosajili pikipiki zao kama vyombo vya biashara ya kusafirisha abiria.

Vurugu hizo zilianza katika eneo la Ubungo River Side muda mfupi baada ya maofisa hao wa Yono kuwakamata baadhi ya madereva wa bodaboda.

Hatua hiyo ilipingwa na madereva hao, ambao walijikusanya na kuwa kundi kubwa na kuanza kuwafukuza maofisa wa Yono waliokuwa kwenye gari dogo aina ya Toyota Noah, wakishinikiza kuachiwa kwa wenzao.

Tukio hilo lililotokea majira ya saa 5.00 asubuhi na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara za Mandela na Morogoro, ambao walilazimika kuwapisha madereva hao barabarani.

Mbali na kupiga honi za pikipiki hovyo, madereva hao waliwakimbiza maofisa hao wa Yono, huku baadhi yao wakiwarushia mawe.

Katika vurugu hizo, gari dogo lenye namba za usajili T 307 STL, mali ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) lilivunjwa kioo cha nyuma kwa mawe.

Madereva hao walilikimbiza gari la maofisa wa Yono huku baadhi yao wakilizingira ubavuni na nyuma.

Baada ya kuona wanazidi kufuatwa, maofisa hao ambao idadi yao haikufahamika mara moja, walilazimika kukimbilia katika kituo cha polisi cha Magomeni kunusuru maisha yao.

Hata hivyo, madereva hao wa bodaboda walifika katika kituo hicho na kuendelea kulizingira gari la maofisa hao, huku wakipiga kelele kushinikiza kuachiwa kwa wenzao wakidai kuwa wameonewa.

Kutokana na wingi wao, walikizingira kituo hicho na kusababisha shughuli zake kusimama kwa muda.

Hali hiyo ilizua taharuki kubwa kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo na kusababisha baadhi ya waliokuwa katika kituo cha polisi kukimbia.

Askari polisi walianza kufyatua risasi za moto hewa na kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya madereva hao.

Wakizungunza na NIPASHE, baadhi ya madereva walisema hawakubaliani na utaratibu wa kukamatwa kwa sababu serikali kupitia Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, ilitangaza kufuta kodi kwa usafiri wa pikipiki.

“Tunashangaa hawa watu wa Yono kutukamata wakidai kwamba hatujasajili pikipiki zetu kwa ajili ya biashara wakati serikali ilitangaza bungeni hivi karibuni kwamba, pikipiki zimefutiwa kodi,” alisema Juma Shaban, ambaye ni mmoja wa madereva wa bodaboda.

Mariam Hussein, ambaye ni shuhuda alisema: “Nimekuja sokoni kununua mahitaji, lakini ghafla nikaona kundi kubwa la bodaboda linakuja huku linapiga honi na makelele, zikaenda hapo polisi na muda mfupi yakaanza kupigwa mabomu.”

Aliongeza: “Baada ya kusikia mabomu watu tukaanza kukimbia huku na kule kujiokoa na hata bodaboda wakawa wanahangaika kukimbia kurudi walikotoka, wakigongana wenyewe kwa wenyewe. Na hata wananchi waliokuwa maeneo haya, wote walikuwa wanakimbia na hata wengine wakawa wanadondoka kutokana na msongamano.”

NIPASHE ililitafuta uongozi wa Yono ili kupata maelezo zaidi juu ya operesheni hiyo iliyosemekana kuwa chanzo cha tukio hilo, lakini halikufanikiwa baada ya kuambiwa kuwa uongozi wala msemaji hawakuwapo ofisini.

Licha ya kukosekana ofisini, lakini lilimtafuta msemaji wake kwa njia ya simu ya mkononi ambayo iliita, lakini haikupokelewa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo.

Hata hivyo, alisema hakuna taarifa ya majeruhi na kwamba, watu saba wamekamatwa katika vurugu hizo, pia pikipiki 10 zimekamatwa.


Waziri Mgimwa akiwasilisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 bungeni Juni 13, mwaka huu alisema Sheria ya Usalama Barabarani, SURA, 168; itafanyiwa marekebisho na alipendekeza kuongeza viwango vya ada ya mwaka ya leseni za magari (Annual Motor vehicle Licence Fee).

Viwango hivyo alivitaja kuwa ni gari lenye ujazo wa injini 501cc hadi 1,500cc kutoka Sh. 100,000 hadi Sh.150,000; gari lenye ujazo wa injini 1501.cc hadi 2,500cc kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 200,000; ujazo wa injini zaidi ya 25,01cc kutoka Sh. 200,000 hadi Sh. 250,000.

Katika mabadiliko hayo alisema kuwa magari yenye ujazo wa injini chini ya 501cc hayatatozwa ada ya leseni za magari. Baada ya kusema hayo, alisisitiza kuwa bodabida ahazitatozwa kodi ili vijana watulie wafanye kazi zao.

Maderava wa bodaboda wameibua changamoto kubwa juu ya usalama barabarani, utii wa sheria na ongezeko kubwa la ajali za barabarani.

Mara kadhaa wamekataa kutii amri halali za kuwataka kufuata sheria, kujichukulia sheria mkononi na hata wakati mwingine kuchoma moto magari ya watu wengine na kupopoa mengine kwa mawe, kwa madai ya kugongwa kwa wenzao.





CHANZO: NIPASHE
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...