Aliyekuwa
makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar amesema atagombea urais
katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 dhidi ya Rais Salva Kiir aliyemfuta kazi
mapema wiki hii. Akizungumza katika mkutano wa hadhara jana kwa mara ya
kwanza tangu kufutwa kazi, Machar alisema atawania kupitia chama tawala
na kumpinga Kiir. Machar ameongeza kuwa ili taifa hilo liungane
haliwezi kuvumilia utawala wa kiimla.Rais Kiir alivunjilia mbali baraza
la mawaziri na kumfuta kazi makamu wake siku ya Jumanne kufuatia ripoti
kuwa kuna mzozo wa uongozi ndani ya chama tawala hasa kati ya Kiir na
Machar.
Kiir
amepunguza idadi ya mawaziri kutoka 29 hadi 18. Pia alimsimamisha kazi
katibu mkuu wa chama cha SPLM Pagan Amum akisubiri kukamilika kwa
uchunguzi wa madai ya kudharau mamlaka na kuleta mgawanyiko ndani ya
chama tawala. Machar amesema Kiir ana haki kikatiba kumfuta kazi makamu
wa rais na kulivunja baraza la mawaziri lakini amemshutumu kwa kile
alichokiita pengo la uongozi lilioachwa baada ya hatua hiyo kwa
kushindwa kujaza nafasi zao mara moja.