Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema), ametaka
Serikali kuhakikisha wajawazito wanaojifungua gerezani watoto wao
wasikae ndani ya gereza.
Akiuliza swali bungeni jana, Nyerere alisema watoto hao siyo wafungwa hivyo kuwaweka gereza ni ukiukaji wa haki za watoto.
“Lini Serikali itaachana na tabia hiyo ya kuwaunganisha watoto na
wafungwa, kwa kuwa hali hiyo ni ukiukaji wa haki za binadamu na ni jambo
la aibu?” Alihoji Nyerere.
Katika swali la msingi, Leticia alitaka kujua Serikali itapoondoa
msongamano magerezani, hasa Gereza la Ngudu ambalo limezidiwa na idadi
kubwa kuliko uwezo wake, hivyo kufanya wafungwa na mahabusu kuishi kwa
tabu.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Silima
alisema wajawazito wanaoingia gerezani ni wahalifu na kwamba, kuna
mazingira ambayo hayaepukiki kutowapeleka gerezani wajawazito hao.
Alisema Serikali ipo kwenye utaratibu wa kuwa na magereza ya watoto,
kuwaepusha kuchanganywa na watu wazima.
Awali, akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Silima alisema Serikali
inatambua matatizo ya msongamano wa wafungwa nchini, hususan Gereza la
Ngudu, wilayani Kwimba, Mkoa Shinyanga.
“Serikali imekuwa ikiyatatua kwa awamu kwa kuyafanyia ukarabati magereza
yaliyopo, kukamilisha na kujenga mapya wilaya ambazo hazina magereza,
lengo ni kuongeza nafasi za kuhifadhi wafungwa magerezani,” alisema.
Kuhusu ucheleweshaji upelelezi, Silima alisema Serikali kupitia Wizara
ya Mambo ya Ndani imeunda Kikosi Kazi kushughulikia msongamano
magerezani, watatoa fursa ya watu kuishi kulingana na idadi ya magereza.
Alisema kikosi hicho kitabainisha vyanzo na sababu za msongamano na
kutoa mapendekezo yake kwa Serikali juu ya hatua za kuchukua.
chanzo:mwananchi