Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Wednesday, June 12, 2013

MAJAJI WATATU KUSIKILIZA KESI YA KIKUNDI CHA UAMSHO..

Kiongozi wa Uamsho, Shekhe Faridi Ahmed.
Mawakili wa Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu ya Zanzibar (Jumiki), Shekhe Faridi Ahmed (41) na wenzake tisa wameiomba Mahakama kufuta taarifa ya kukata rufaa ya Mkurugenzi wa Mashitaka wa Zanzibar (DPP).


Waliomba hayo jana katika Mahakama ya Rufaa Dar es Salaam mbele ya Jopo la majaji Januari Msoffe, Salum Massati na William Mandia, wakati wakisikiliza ombi la  kutaka rufaa dhidi ya uamuzi wa dhamana uliotolewa Machi 11 mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Zanzibar litupwe.
Katika uamuzi huo, Mahakama ilitengua mwenendo wa maombi ya dhamana ya washitakiwa pia ilitupilia mbali maombi ya marejeo ya uamuzi wa Msajili wa Mahakama Kuu uliowanyima dhamana washitakiwa, pamoja na kukataa pingamizi la awali la upande wa mashitaka.
Ombi hilo lilisikilizwa jana bila washitakiwa kufika mahakamani, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama, ambapo kila mtu aliyeingia alikaguliwa na mashine ya ukaguzi.
Wakili wa waleta maombi, Salum Toufiq alidai wameleta ombi hilo kwa kuwa dhamana ni haki kwa washitakiwa na kwa mujibu wa Katibu ya Zanzibar, kesi za jinai zinatakiwa kusilikizwa na kutolewa uamuzi haraka  lakini wanachofanya upande wa mashitaka ni kuchelewesha kesi.
Hata hivyo, mawakili wanaomwakilisha DPP walidai Msajili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, aliyesikiliza maombi ya kwanza ya dhamana ya washitakiwa hao, hakuwa na mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.
Aidha, walidai maombi ya akina Farid si sahihi, kwa kuwa wameyaleta kwa kutumia kifungu cha Kanuni za Mahakama ya Rufaa ambacho kinatumika na Mahakama yenyewe.
Jaji Msoffe alipotaka maelezo kama Msajili aliyesikiliza maombi ya kwanza ya akina Farid alipewa mamlaka na Jaji Mkuu ya kufanya hivyo, mawakili  wa waleta maombi walidai hakuwa nayo. 
Wakili Ramadhan Nassib alidai uamuzi uliotolewa na msajili ulikuwa batili na msajili huyo alichukua kesi bila ya kufuata utaratibu hivyo haikuwa sahihi na kwamba kilichobaki Mahakama Kuu ni hati ya mashitaka dhidi ya washitakiwa tu.
Mbali ya Shekhe Farid, waleta maombi wengine ni Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Mussa, Azan Khalid, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman, Ghalib Ahmada Jum,Abdallah Said na Fikirini Fikirini.
Shekhe Farid na wenzake walifikishwa mahakamani Oktoba 25 mwaka jana na kusomewa mashitaka chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa na Sheria ya Kanuni za Adhabu na hawakuruhusiwa kujibu mashitaka yao.
Aidha walinyimwa dhamana kwa kuwa DPP aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana yao kwa madai kuwa watahatarisha usalama wa nchi. Washitakiwa hawakuridhika na uamuzi huo na kuwasilisha maombi ya marejeo ya uamuzi huo, lakini upande wa mashitaka uliweka pingamizi ukiomba maombi hayo yatupiliwe mbali.
Jaji Abrahamu Mwampashi alitupilia mbali pingamizi hilo la upande wa mashitaka, maombi ya marejeo ya washitakiwa na kubatilisha mwenendo wa maombi ya dhamana kwa Msajili wa Mahakama Kuu.
Credit: audifacejackson blog
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...