Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana.Picha na Fidelis Felix
Dodoma. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepinga muundo wa Muungano wa Serikali tatu unaopendekezwa katika rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Chama hicho tawala kimesema bado kinaamini katika muundo wa Serikali mbili.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa
habari mjini Dodoma jana kwamba mapendekezo yaliyowasilishwa mbele ya
Tume hiyo yanabaki kama yalivyo, hivyo msimamo wao ni kuwapo kwa
muungano wenye muundo wa Serikali mbili.
“Mapendekezo ambayo ndiyo msimamo wa chama tulishayawasilisha kwenye
Tume kuwa sisi tunapendekeza mfumo wa Serikali mbili na siyo tatu wala
moja,” alisema Nape alipokuwa akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu
(CC) ya CCM iliyokutana usiku wa kuamkia jana kujadili suala hilo.
Kauli ya Nape inafanana na matamshi ambayo yamewahi kutolewa na baadhi
ya wanasiasa wakongwe ambao ni makada wa CCM wakiwamo, mawaziri wakuu
wastaafu, Frederick Sumaye na John Malecela, Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta na baadhi ya wabunge ambao mara kadhaa
wamekaririwa wakipinga pendekezo la Serikali tatu.
Hata hivyo, Nape alisema matamshi ya viongozi hao yalikuwa ni maoni yao
binafsi na kauli yake ndiyo rasmi ya chama hicho... “Mimi ndiye msemaji
wa chama hiki. Ndiye ninayeeleza msimamo wa chama chetu, yanayozungumzwa
na watu wengine hata kama ni viongozi siyo msimamo wa chama ni maoni
yao binafsi.”
Habari ambazo gazeti hili ilizipata zinasema katika kikao hicho cha CC
kulijitokeza hofu ya suala la wananchi kuwa na mamlaka ya kuwang’oa
wabunge ikiwa hawatatekeleza masilahi yao na kwamba pendekezo hilo lina
upungufu kwani halitafsiri masilahi hayo ni yapi.
Waunda kamati
Nape alisema rasimu iliyotolewa na Tume siyo waraka wa mwisho kwani bado
unatoa fursa kwa Watanzania kuijadili na kutoa maoni yao na kwamba CCM
kitatumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yake kuhusu jambo hilo.
Alisema chama hicho kitawasiliana na wanachama wake zaidi ya 6,000 nchini ili waendelee kutoa maoni yao kuhusu suala hilo.
“Wengi wanadhani rasimu hii ndiyo ya mwisho… hii ni ya mwanzo tu,
itajadiliwa italetwa ya pili na ya tatu, kwa hiyo hatuwezi kusema
kilichoelezwa kwenye tume ndiyo msimamo. Ndiyo maana tumeamua kurejesha
suala hili kwa wanachama wetu liendelee kujadiliwa,” alisema na
kuongeza:
“Kama wanachama wetu wakiamua kuwepo kwa Serikali tatu, hatutachakachua,
tutayachukua na kuyapeleka kama msimamo wetu, lakini tutakubaliana
ikiwa uamuzi utakuwa umewahusisha wanachama wetu katika ngazi zote.”
“Hatuangalii kipengele kimoja tu. Tutapitia vipengele vyote hadi
kuzimaliza kurasa zote zaidi ya 70 zinazoainisha mapendekezo ya Tume ya
Jaji (Joseph) Warioba.”
Alisema wanachama wake wanapaswa kuipitia na kuijadili rasimu hiyo kwa
kuzingatia mapendekezo kilichoyatoa awali wakati wa mchakato wa
kukusanya maoni ya Katiba Mpya.
“Tulitoa maoni yetu na sasa tunaijadili Rasimu ya Katiba Mpya kwa
kuzingatia maoni yetu yale, CCM tunakwenda kwa mujibu wa sheria,”
alisema. Habari kutoka ndani ya CC ya CCM zinasema chama hicho kimeipa
kazi kamati ambayo ilitumika kuandaa mapendekezo yake awali, kupitia
rasimu hiyo na kufanya ulinganisho wa yale ambayo chama hicho
kilipendekeza dhidi ya yale yaliyozingatiwa katika Rasimu ya Katiba
hiyo.
“Kamati itafanya ulinganisho na baada ya hapo tutakwenda kwa wanachama
kuwaeleza ni yapi tulipendekeza kama chama na ni yapi ambayo Tume
imeyazingatia na hapo tutapata mawazo yao ambayo tutayatumia katika
ngazi ya mabaraza ya Katiba,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi