POLISI saba kutoka wilayani Kasulu, wamepandishwa kizimbani katika 
Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, iliyoanza kikao chake mjini Kigoma leo na 
kusomewa mashitaka ya kuua kwa kukusudia. 
Mbele ya Jaji Sam Rumanyika, askari Polisi hao walidaiwa kuwa Agosti 6, 
2011 walimpiga na kumuua kwa makusudi Festo Stephano, mkulima na mkazi 
wa Kijiji cha Rungwe mpya wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Waliopandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka yao ni pamoja na Baraka 
Hongdi, Koplo Mawazo, Koplo Swahib, Koplo Charles, Koplo Shamsi, Koplo 
Jerry na Koplo Amrani ambao kwa pamoja walikana mashitaka.
Baada ya kukana mashitaka, kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa mashahidi 
wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao, ambapo shahidi wa kwanza
 katika kesi hiyo, Masumbuko Stephano, aliieleza Mahakama kwamba askari 
hao walikusudia kufanya mauaji hayo.
Masumbuko aliieleza Mahakama kwamba siku ya tukio, alikamatwa pamoja na 
marehemu na mgambo wa kijiji, na kuwekwa katika mahabusu ndogo katika 
Ofisi ya Mtendaji wa Kata.
Alidai baada ya kufika, askari hao walianza kuwapiga kwa kutumia vitako 
vya bunduki, fimbo na chupa za bia, hali iliyosababisha wapatwe na 
maumivu makali.
Shahidi huyo alidai kuwa baada ya kupigwa na kukaribia kupoteza fahamu, 
polisi hao waliwavua nguo, wakawafunika na turubai ndani ya gari ambapo 
baadaye walinunua magunia ya mkaa na kuwakandamiza na magunia hayo.
Shahidi wa pili katika kesi hiyo, Andrea Sama, alidai kwamba askari hao 
walikusudia kufanya mauaji siku hiyo, kwani licha ya kutoa kipigo pia 
waliwavua nguo na kuwaingiza miti kwenye sehemu zao za haja kubwa.
“Mheshimiwa Jaji kwa kweli nilishuhudia vitendo vya askari hao kwa macho
 yangu, na nilishindwa kuamini kama jambo hilo linafanyika kwenye ardhi 
ya Tanzania au tuko nchi nyingine, maana unyama uliofanywa na askari 
polisi hao huwezi kudhani kama ni walinzi wa amani katika nchi hii,” 
alidai Sama.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa mfululizo hadi kutolewa hukumu, ambapo 
mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Juvelin Rugaihuruza, alidai kuwa 
upande wa Jamhuri ambao ndiyo mlalamikaji, unatarajia kuwa na mashahidi 
12 na vielelezo viwili.
Washitakiwa hao wanatetewa na Mwanasheria, Method Kabuguzi, kutoka 
Kampuni ya Uwakili ya Kigoma Law Chamber and Advocate ya mjini Kigoma.




