Flora Bahati Lyimo.
Katika
uchunguzi wake, hivi karibuni gazeti hili lilielezwa kuwa kuna habari
ya kashfa nzito inayomtafuna mbunge huyo anayetokea Kanda ya Kaskazini
lakini haikufafanua kwamba inahusu nini.
VYANZO
Baada
ya kutulia na kupekua kwenye vyanzo vyake, Uwazi lilibaini kuwa kashfa
inayomlenga mheshimiwa huyo ni ya ubakaji na tayari imefikishwa
mahakamani huko London nchini Uingereza.
Habari
hiyo ilielezwa ‘kijuujuu’ hivyo gazeti hili likamtafuta Flora ambaye ni
Mtanzania anayetokea mkoani Kilimanjaro ambaye anaishi katika Jiji la
London kikazi.
MAZITO
Alipopatikana
Flora alibanwa kisawasawa ndipo akaibua mazito huku akieleza tukio zima
lilivyofanyika kwa data na vielelezo vya kila aina ikiwemo barua ya
Mahakama ya Crown ya London.
“Ni
kweli mheshimiwa … (anamtaja jina) alinibaka Agosti, mwaka jana. Yeye
na makada wenzake wa chama chake walikuja hapa London kwa ziara ya
kichama na kwa kuwa mimi sina chama nilikwenda kuhudhuria mkutano wao
kwa kuwa nina mtandao wangu (blog) hivyo nilitaka kupata habari za
kuingiza kwa sababu ni za watu wa nyumbani (Tanzania).
MAZOEA YAANZA
Akiendelea
kuweka wazi kisa hicho, Flora anasema: “Nikiwa kwenye mkutano….(jina la
mbunge) alinifuata akaniuliza nimeandika watu wangapi waliohudhuria
mkutano huo, nikamjibu 50 akaniambia niongeze idadi hiyo ili ionekane
mkutano ulikuwa na watu (Watanzania waishio Uingereza) wengi.
“Hapo
ndipo alipoanza kunizoea. Alitaka kunipa kadi ya chama chake
nikakataa, ndipo akadai kwamba mimi nilitumwa kwenye mkutano huo na
balozi na rais kwa ajili ya ushushushu.
KISA KUJISAIDIA HAJA NDOGO
“Mkutano
ulimalizika, sasa nilipokuwa naondoka kurudi nyumbani kwangu, mbunge
huyo na wenzake nao walitoka. Tukiwa njiani wenzake walikwenda
kujisaidia haja ndogo, yeye akaniomba akajisaide nyumbani kwangu,
nilimkubalia. Alipofika ndani, bila kujua kila kitu kinaonekana kwenye
kamera alinibadilikia kama vile adui vitani, ona sasa wema wangu ukawa
umeniponza.
HADI KITANDANI
Alinirukia,
akaniburuza hadi kitandani kwangu. Nilipokuwa mkali na kwa namna
nilivyokuwa nimechanganyikiwa sishikiki ndipo akanivamia maungoni,
akanichania nguo zangu akitaka nimwachie atimize lengo lake la
kuniingilia kimwili kwa nguvu.
“Nilijitahidi
ili asifanikiwe, nikamwambia amekwisha kwani lazima nimwanike ndipo
akanipiga nusu aniue akisisitiza kuwa kama nitauanika uovu wake huo au
kuchukua hatua zozote ataniua.
“Inaniuma sana, kunibaka anibake halafu atishie kuniua, unyama gani huu?”
AITA POLISI
Flora anaendelea kusema:
“Katika
purukushani hiyo, nilipopata mwanya kidogo tu, nikapiga namba ya polisi
999 kuomba msaada. Alipoona hivyo alitoka na kutokomea kusikojulikana.
Polisi walipofika hawakufanikiwa kumkamata.”
UBAKAJI/KUTISHIA KUUA
Flora
alisema polisi walimchukua na kila kitu cha ushahidi zikiwemo nguo zake
hadi kituoni, wakamhoji kwa kumrekodi sauti, wakampa namba ya jalada la
kesi inayosomeka; 4621279/2012-UBAKAJI/KUTISHIA KUUA ambapo hadi leo
mbunge huyo anasakwa na Polisi wa London, akikanyaga tu Uingereza lazima
akamatwe akajibu tuhuma za ubakaji na kutishia kuua.
Flora
akaongeza: “Ukweli ni kwamba hakufanikiwa kukamatwa kwa sababu alikuwa
na passport za kidiplomasia ambazo nyingine hakutumia jina lake halisi.
“Kesho
yake nilisikia alikimbilia Ujerumani, nikawaambia polisi lakini
walikumbana na tatizo lile kwani majina niliyowapa siyo aliyotumia
kuingia Ulaya.
“Januari
mwaka huu nilipotaka kurudi nyumbani Kilimanjaro, mahakama ya hapa
(Uingereza) ilinipa barua ambayo nilipofika niliipeleka Kituo Kikuu cha
Polisi Moshi nikafunguliwa faili Namba Mos/RB/17127/12 kwa ajili ya
ulinzi chini ya R.C.O Ramadhan Ng’anza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz.
“Niliwaeleza
kuwa mtu anayetaka kuniua ni mbunge huyo. Kweli waliahidi kunisaidia,
nilipoondoka kurudi London niliwasiliana na polisi Kilimanjaro lakini
niliona kama kuna kitu au mbunge huyo yupo juu ya sheria kwani walikana
kunifahamu.
ASHINDA MAHAKAMANI
“Sitachoka
kutafuta haki na kutetea wanawake wanaobakwa kila siku wanaona aibu
kusema, naamini aibu haipo kwa mbakwaji bali kwa mbakaji, yule ….
(anataka jina) ni mbakaji.
“Nimesharipoti
mashirika mengi ya haki za binadamu ya Uingereza. Kuna siku nilishinda
mahakamani, kule ni yeye tu anasubiriwa atiwe mbaroni akasimame
kizimbani ndipo dunia itajua ninachokisema.”
ASUBIRIWA KIZIMBANI
Flora allisema kama kweli mbunge huyo ni mwanaume aende tena jijini London kama hatasimamishwa kizimbani na kuozea jela.”
Uwazi,
kabla ya kumtafuta Kamanda wa Polisi wa Kilimanjaro, RPC Robert Boaz,
Jumamosi iliyopita lilimtafuta RCO Ng’anza ambaye alisikiliza mkasa
mzima na kudai kuwa hamfahamu Flora lakini alipobanwa alidai yeye siyo
msemaji wa jeshi hilo kisha akakata simu.
KAMANDA WA POLISI
Kwa
upande wake RPC Boaz alisema kuwa kipindi kinachotajwa cha mwezi
Januari yeye alikuwa likizo ndefu na hajawahi kusikia habari kama hiyo
lakini akaahidi kuifuatilia kwa RCO Ng’anza na baadaye arudishe majibu
kwa Uwazi.
Alipotafutwa tena Jumapili iliyopita kwa njia ya simu yake ya mkononi hakupatikana hewani.
SASA NI ZAMU YA MBUNGE
Kama
ilivyo desturi ya Uwazi, Jumamosi hiyohiyo lilimtafuta mbunge
anayetajwa katika aibu hiyo kubwa huku akiwakilisha wananchi wa jimbo
lake ambapo alisomewa kisa kizima kisha akapewa nafasi kuzungumzia au
kufafanua kashfa hiyo ya karne.
Huku
akirekodiwa neno kwa neno, mheshimiwa huyo alisema: “Huyo mwanamke
(akatajiwa jina la Flora Lyimo) simfahamu lakini usikubali kushiriki
kwenye dhambi ya kunichafua kwa sababu ni uongo.
Uwazi: Kwa hiyo mheshimiwa hujawahi kusikia habari hiyo?
Mbunge: Niliisikia, ninaifahamu. Ina karibia miezi nane sasa kwani ameibuka sasa hivi?
Uwazi: Sasa kama hiyo habari ni ya uongo kwa nini usimshitaki?
Mbunge:
Habari hiyo ipo mtandaoni, kama nikisema nishitaki mitandao nitashitaki
mingapi? Mbona …(anautaja mtandao wa kijamii wa Tanzania)
wameshanichafua sana. Nikianza kuhangaika na kesi najua miaka yote
mitano nitakuwa mahakamani badala ya kuendesha harakati jimboni mwangu.
Uwazi: Kama anakusingizia kwa nini wewe?
Mbunge:
Huyo ametumwa na …(jina la mwanasiasa mkubwa nchini) na …(jina la
chama), huko ni kuchafuana kwa sababu kama ni kunikamata, nani asiyejua
jimbo langu, ofisi yangu, nyumbani kwangu na umaarufu wangu? Mwambie aje
sasa hivi anikamate.
TURUDI KWA MLALAMIKAJI
Baada
ya kusikia majibu ya mbunge huyo, Uwazi lilirudi kwa mlalamikaji Flora
na kumweleza alichokijibu mbunge huyo ambapo na yeye alisema:
“Nawatumia
picha wakati akiingia na kutoka kwangu kwani huku kuna kamera za mtaani
zinachukua kila tukio. Unajua lazima abishe kwa sababu ni aibu kubwa
kwake na chama chake.”
KUTOKA UWAZI
Sakati
hili ndiyo tumeanza kulichimba, mambo mengi yataibuka kwa kuwa
tunajiridhisha kwanza na muda wowote tutamwanika mheshimiwa huyo ili
ajitokeze na kuthibitisha kuwa hakufanya kitendo hicho kwani mlalamikaji
ameshasema yake.
NA GLOBAL PUBLISHER