JESHI
la Wananchi Tanzania (JWTZ), limesema limeanza kuwapeleka askari wake
nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) kulinda amani na kuhakikisha
wananyang’anywa silaha zote waasi wa kundi la M23 ili nchi hiyo
itawalike.
Kutokana
na hatua hiyo, JWTZ limesema halitishwi na vitisho vya M23 kutokana na
kujiandaa vizuri kila idara, ikiwa ni lengo la kutaka kuona wananchi wa
DRC wanaishi kwa amani, tofauti na sasa ambako kumekuwa na vitendo vya
kinyama dhidi ya wanawake na watoto wadogo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, wakati wa kutoa tamko
la jeshi hilo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema kamwe
hawatishwi na kundi la M23.
Alisema
wanashangazwa na kitendo M23 kutoa vitisho, wakati askari wanaokwenda
huko wanatoka nhi za Afrika Kusini, Malawi na Tanzania.
“Kwa
nini iwe Tanzania pekee, sisi hatuwezi kutishwa na kikundi cha
wanamgambo 1,000, tunasema tunakwenda kutimiza jukumu la Umoja wa
Mataifa (UN) kuhakikisha DRC inatawalika na silaha zote wananyang’anywa,
“Tanzania
tuna historia kubwa ya kuleta ukombozi na amani ndani ya nchi za
Afrika, zikiwamo Commoro, Afrika Kusini, Liberia, Sudan na Lebanon,
ndiyo maana vikosi vyote vitatu vinaongozwa na Mtanzania, Brigedia
Jenerali James Mwakibolwa.
“Itakumbukwa
Idd Amin Dada, alikuwa anajigamba na kusema anataka kuja kunywa chai
Dar es Salaam, lakini aliishia kuchungulia visiwa vya Ukerewe… majigambo
ya M23 ni ishara ya kuanza kuwa na wasiwasi,” alisema Kanali Mgawe.
Alisema
kikosi kilichoanza kwenda DRC,kinajulikana kama Tanzania Bataria One
–DRC (TANZBATT-1 DRC) na kuongeza kwamba kila baada ya miezi sita
kutafanyika mabadiliko kadri itakavyohitajika.
Alisema
kutokana na vitisho hivyo, bado Tanzania ni salama na itakuwa kuwa
salama na kuwataka Watanzania kuondoa hofu juu ya matukio yanayotokea
hivi sasa.
Alisema
vifaa vya askari, wanaokwenda Kongo vimekamilika na tayari UN
imevifanyia ukaguzi na kuridhia vinakidhi mahitaji katika kuimarisha
ulinzi na usalama.
Kuhusu mzozo wa Tanzania na Malawi, alisema nchi hizo bado zina uhusiano mzuri wa kidiplomasia.
Mapema
wiki hii, Rais Jakaya Kikwete aiwakabidhi askari wa JWTZ bendera mkoani
Pwani, ikiwa ni ishara ya kuanza safari ya kuelekea DRC.
Mtanzania