Dar es Salaam. Kuwepo kwa mabanda mengi ya kuonyesha filamu yasiyo na
usimamizi nchini, kumewapa watoto wadogo nafasi ya kuangalia picha za
ngono, huku Serikali ikishindwa kuchukua hatua stahiki ikiwamo kuyafunga
mabanda hayo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumamosi katika mitaa mbalimbali
jijini Dar es Salaam, umebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya mabanda ya
kuonyesha filamu katika makazi ya watu, hivyo kuwapa watoto nafasi ya
kutazama picha zisizofaa kimaadili.
Uchunguzi huo uliofanyika mchana na usiku, umebaini kuwa baadhi ya
wazazi huwapa watoto wao fedha kwenda katika mabanda hayo bila kujua
aina ya filamu wanazokwenda kuangalia, huku wazazi wengine wakiwa hawana
taarifa kuwa watoto wao huingia katika mabanda hayo.
Katika mitaa ya Kigogo na Mburahati, baadhi ya wanawake walikutwa saa
tatu usiku wakiangalia filamu kutoka barani Asia huku wakiwa wamebeba
watoto wadogo. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ilikuwa ikionyesha watu
wakishiriki tendo la ndoa.
Msimamizi wa banda hilo (jina tunalo) alipoulizwa alisema: “Hilo ni picha la Amitabh Bachchan.”
Hata hivyo, baada ya kuiangalia video hiyo kwa muda wa zaidi ya dakika
20, ilibainika kuwa filamu hiyo ilikuwa imechanganywa na filamu nyingine
tofauti na ile iliyotajwa.
Katika banda moja lililojengwa kwa mifuko ya plastiki katika Mtaa wa
Kabojonga, Mtoni Kijichi walionekana wanawake wanne wakiwa wamekaa
sakafuni saa tatu usiku, huku wamewapakata watoto wadogo waliokuwa
wamelala.
Chumba hicho kilikuwa kimejaa watoto wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya
miaka mitano hadi 17. Walikuwa wamekaa kimya, wakifuatilia filamu
iliyotafsiriwa kwa Kiswahili
Kama ilivyokuwa katika mabanda mengine, watoto hao walikuwa wakiangalia
filamu kutoka barani Asia iliyofahamika kwa jina la Train.
Msimamizi wa banda hilo, muda wote alionekana kushika ‘remote control’
kwa ajili ya kusogeza mbele baadhi ya sehemu katika filamu hiyo, ambazo
zinaonyesha utupu kitendo kilichowafanya watazamaji kulalamika.
“Ina scratches nyinyi, hamuoni?” alijibu msimamizi wa banda hilo, lakini
ukweli ni kwamba alikuwa akitaka kusogeza mbele sehemu inaonyesha watu
wakifanya ngono.
Saa nne usiku, katika banda jingine eneo la Mbagala Charambe, watoto
wawili walikutwa wakiangalia filamu kupitia tundu lililopo kwenye moja
ya kona ya banda hilo lililojengwa kwa turubai kuukuu. Ndani ya banda
watu walikuwa wakiangali filamu ya ngono.
Kwa mujibu wa watoto hao, wanafunzi wa shule ya Msingi Majimatitu
(majina tunayo) walifukuzwa kutoka ndani ya banda hilo baada ya kukosa
fedha za kulipia ‘picha’ ya pili baada ya ile ya mwanzo waliyokuwa
wakiangalia kumalizika.
“Mwanzo tulikuwa tunaangalia filamu ya Sarafina, lakini naona sasa
wamebadilisha wameweka picha ya kizungu,” alisema mtoto mmoja.
Mbinu zinazotumika
Ilibainika kuwa wenye mabanda ya kuonyesha filamu hubandika ukutani
matangazo ya filamu zitakazoonyeshwa siku hiyo, lakini huzibadilisha
baadaye na kuweka filamu za ngono.
Katika baadhi ya mabanda ilibainika kuwa huanza kuonyesha mikanda ya
ngono kuanzia saa tatu na saa sita usiku wakati watu wengi wamekwenda
kulala.
Wenye mabanda hayo ya filamu wamebainika pia kutumia majina tofauti yanayotaja mikanda ya ngono.
Baadhi ya majina hayo ni ‘Pilau’, ‘Blue’, ‘Kuchikuchi Hotae’, ‘Yale mambo yetu’ na ‘Picha la ukweli’.
Katika banda moja huko Tandika, haruhusiwi mtu asiyefahamika kuingia
ndani ya banda hilo. Jitihada za kujua nini kilichokuwa kikiendelea
katika banda hilo zilifanikiwa baada ya kumtumia binti mmoja (jina
tunalo) mwenyeji wa eneo hilo, aliyetuthibitishia kuwa filamu iliyokuwa
ikitazamwa ndani ilikuwa ni ya ngono.
Uchunguzi ulibaini pia kwamba mabanda mengi yanayoonyeshsa filamu
mitaani hayana leseni, huku baadhi yao leseni zake zikiwa zimeisha muda
wake.
Kilichobainika kuhusu watoto
Baadhi ya watoto waliohojiwa, wengi wakiwa ni wanafunzi wa shule za
msingi, walisema wameshaona zaidi ya mara moja filamu za watu wakifanya
ngono katika mabanda ya kuonyesha filamu hizo.
“Tuliona kwa (analitaja banda la kuonyesha filamu) watu walikuwa
wakifanya ngono bafuni, baadaye wakaenda chumbani,” alisema mtoto (jina
tunalihifadhi) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya
Msingi Mabibo, Kinondoni.
Mtoto mwingine wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Tumaini, Ilala,
alisema aliwahi kufukuzwa kutoka kwenye banda ambalo watu walikuwa
wakiangalia filamu za ngono.
“Mwanzo tulikuwa tunaangalia ‘muvi’ ya Kanumba, ilipoisha wakaweka ya
kizungu…wakati inaanza niliona watu hawana nguo nikaanza kucheka
wakanifukuza wakasema nitoke mimi bado mdogo,” alisema mtoto huyo wa
miaka 13.
Maoni ya wazazi
Wazazi walioonyesha kukerwa na tatizo hilo, waliilalamikia Serikali kwa
kushindwa kuyafunga mabanda ya filamu na kusema ni vyema kama litatumika
Jeshi la Polisi kuyafunga na ikibidi kuyabomoa kabisa.
“Siku hizi watoto nyumbani wanafanya mambo ya ajabu, ukiwauliza
mmejifunza wapi wanakwambia tulikuwa tunaangalia mkanda wa video,
…tumechoka, bora wayavunje kabisa mabanda hayo,” alisema Voida Sanga
mkazi wa Sinza Kijiweni.
Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God (TAG) Kimara, Festo Segesela
alisema kuwa hali imekuwa mbaya katika baadhi ya mitaa kwa kuwa kuna
wasichana wadogo wanaokwenda kuangalia mikanda ya ngono, huku wakiwa
wamebeba watoto mgongoni.
“Kwa kweli hali ni mbaya…, kizazi chetu kinaangimia, wengine ni mabinti
wadogo kabisa wanakwenda kuangalia hiyo mikanda ya ngono wakiwa na
watoto mgongoni,” alisema Segesela.
Akifafanua, Segesela alisema kuwa hali imefika ilipo sasa kutokana na
viongozi wa Serikali kuingiza siasa katika mambo yanayohitaji
kuchukuliwa hatua za haraka.
“Kuna baadhi ya viongozi wanashindwa kuchukua hatua kwa sababu tu wanaogopa kunyimwa kura, hii ni hatari kwa kweli,” alisema Segesela
“Kuna baadhi ya viongozi wanashindwa kuchukua hatua kwa sababu tu wanaogopa kunyimwa kura, hii ni hatari kwa kweli,” alisema Segesela
Hata hivyo, baadhi ya wazazi waliunga mkono kuwepo kwa mabanda ya
kuonyesha filamu kwa kile walichosema kuwa watoto wao hutumia muda wa
jioni kuangalia video badala ya kwenda mitaani kuzurura.
“Ni bora nikampa mwanangu shilingi mia, aende kuangalia video kuliko
aende kucheza mitaani ambako hata sielewi atakutana na nani,” alisema
Vicky Tarimo mkazi wa Mwananyamala Kisiwani
Wazazi wengine waliwarushia lawama wazazi wenzao kwa kushindwa
kuwaangalia watoto wao, kwa madai kuwa baadhi ya watoto wamekuwa
wakitumia siku nzima katika mabanda ya filamu hizo, huku wazazi wao
wakiwa hawana taarifa ya kitu kinachoendelea
“Mzazi hajui mtoto wake yuko wapi siku nzima, amepata fedha wapi ya
kuangalia hiyo mikanda? Hata kama ni shilingi mia kila mkanda, lazima
ujue amepata wapi,” alisema Elias Naftari mkazi wa Kigogo
Mwenyekiti wa Bazara Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mtaa wa
Twangoma Temeke, Darwesh Kinicha alisema iwapo hali itaachwa iendelee
ilivyo sasa maadili ya jamii yatavurugika na kubaki na kizazi kisicho na
mwelekeo.
Akitoa mfano, Kinicha alisema mtoto wake ambaye ana miaka saba tayari
ameshaanza kuonyesha dalili zinazoashiria kuwa ameshajifunza mambo
yasiyofaa.
“Mimi mwenyewe mtoto wangu yupo darasa la saba anazungumza mambo hayo
hayo; …kutokana na vitendo anavyofanya na wenzake, nimeamua kumpeleka
madrasa, akitoka huko namfungia ndani sitaki aende kucheza kokote,”
alisema Kinicha.
Aliongeza: “Nimeamua kununua TV awe anaangalia channel ya Baby TV, lakini ni wazazi wangapi wanaoweza kufanya hivi?,” alihoji Chinicha.
Aliongeza: “Nimeamua kununua TV awe anaangalia channel ya Baby TV, lakini ni wazazi wangapi wanaoweza kufanya hivi?,” alihoji Chinicha.
Kwa mujibu wa Chinicha, vitendo vya watoto kuangalia filamu za ngono
vimezidi zaidi katika maeneo ya ‘uswahilini’ ambako filamu hizo
huonyeshwa kwenye mabanda yaliyosehemu za wazi na yanayofahamika na
viongozi wa eneo husika.
“Hili jambo halihitaji uchunguzi wala kuundwa tume, huku kwetu
uswahilini hali ni mbaya kuliko maeneo ya Mikocheni na Mbezi Beach,”
alisema Chinicha.
Maoni ya Ofisa Habari wa Wilaya ya Temeke
Kwa kujibu wa Ofisa Habari wa Wilaya ya Temeke, Joyce Nsumba, wanazo
taarifa za watoto kuangalia filamu za ngono kwenye mabanda mitaani kwa
muda mrefu na kwamba watendaji wa mitaa ndiyo waliopewa jukumu la
kusimamia mabanda hayo na kuhakikisha yanafungwa.
Nsumba alisema kuwa madiwani walilijadili tatizo hilo kwenye Mkutano
Mkuu wa mwaka na kukubaliana kuwa kila kiongozi wa mtaa ahakikishe
mabanda hayo yanafungwa.
“Hiyo ni kero ambayo inafahamika hata madiwani walijadili, tatizo ni
nguvu ya soda inatumika, tuna mpango tuwashirikishe polisi watusaidie
kuwakamata wote wanaoendelea na vitendo hivyo,” alisema Nsumba.
Hata hivyo, baadhi ya watendaji katika halmashauri, ambao hawakutaka
majina yao kuandikwa gazetini kwa madai kuwa wao siyo wasemaji wa
halmashuri, walisema kuwa mpango wa kuyafunga mabanda ya filamu huenda
usifanikiwe kwa kuwa kuna baadhi ya madiwani wanamiliki mabanda hayo.
“Wapo baadhi ya waheshimiwa madiwani ambao wamekuwa wakitutishia
tunapotaka kwenda kuyafunga mabanda hayo kwa sababu nao wanamiliki
mabanda,” kilisema chanjo chetu.
Kamanda Kova ahaidi kuchukua hatua
Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema kuwa vitendo
vinavyofanywa na wenye mabanda ya kuonyesha filamu ni kosa na
havikubaliki, huku akiahidi kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua
za kisheria wahusika wote.
“Vitendo wanavyofanya havikubaliki, tutawajulisha makamanda wote wachukue hatua haraka,” alisema Kova.
chanzo:mwananchi