CHAMA
cha Wananchi (CUF) kimesema hakihusiki na vurugu zinazotokea katika
mikoa ya Lindi na Mtwara na kamwe hakitojihusisha na siasa za vurugu.
Taarifa
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Naibu Katibu Mkuu wa CUF,
Julius Mtatiro ilieleza kuwa kwa nyakati tofauti vikao vya mikoa hiyo
vilivyofanyika vimekishutumu chama hicho kuwa kinara wa kuongoza vurugu
katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Alisema
licha ya vikao hivyo kuitaja CUF kuwahamasisha wananchi wawe na misimamo
mikali, lakini ukweli wa jambo hilo unafahamika na kila mtu.
“CUF
haihusiki hata kidogo na misimamo mikali ya wananchi… wananchi ni
waadilifu wanaoipenda nchi yao, na ni watu wazima wasioweza kufundishwa
misimamo na chama cha siasa chenye umri wa miaka 20 kama CUF,” alisema.
Mtatiro
alisema CUF haihusiki na vurugu za wananchi na uvunjifu wa amani katika
wilaya za Masasi, Tandahimba, Liwale, Ruangwa na kwingineko.
Aliongeza
kuwa vurugu za Liwale ziko wazi na chanzo chake ni mfumo mbovu na wa
kiuonevu wa stakabadhi ghalani ambapo wakulima wa korosho waliuza
korosho zao kwa shilingi 1,200 kwa kilo moja na kulipwa sh 600.
Alisema
wakulima hao walijulishwa kuwa malipo ya awamu ya pili wangepewa
shilingi 600 zilizobaki ili kukamilisha 1,200 lakini yalicheleweshwa.
Aliongeza kuwa vurugu za Ruangwa zinafanana na za Liwale ambapo chanzo chake ni wakulima kudhulumiwa fedha zao za korosho.
Mtatiro
alisema CUF haiungi mkono vurugu za wananchi pale wanapodai haki zao
bali wanawasihi wadai kwa njia za amani na ikitokea wakafanya vurugu
serikali iwajibike kwa kuwa yenyewe ndiyo inakuwa imezuia haki zao.
Alibainisha
kuwa CUF inaitaka serikali itatue matatizo mbalimbali kutokana na
vyanzo vya matatizo hayo likiwemo suala la wakulima wa korosho na mazao
mengine kwa kuwa ni kilio cha siku nyingi.
“Mfumo wa
stakabadhi ghalani ufutwe mara moja ili tuwe na soko la ushindani wa
ununuzi wa mazao ya biashara na kumfanya mkulima anufaike. Pia serikali
ishiriki katika kupanga bei ya chini ili kuwalinda wakulima, lakini
isiwalazimishe wakauze wapi na wapi.
“Wafanyabiashara
waruhusiwe kutoka kila kona ya dunia kuja kushindana kununua mazao ya
biashara na si kuchagua wafanyabiashara wachache tu,” alisema.
Kuhusu
gesi, alisema CUF inaamini kuwa Tanzania si Dar ss Salaam pekee, hivyo
serikali lazima ipanue uchumi wa mikoa ya pembezoni na rasilimali gesi
itumike kwa manufaa ya taifa zima.
Aliongeza
kuwa ni vema Mtwara kukajengwa mtambo mkubwa wa kuzalisha umeme na
kuunganisha na gridi ya taifa, viwanda vya mbolea na kemikali, hoteli
kubwa kwa ajili ya utalii wa mikoa ya kusini.
Mtatiro
alibainisha kuwa CUF inawataka viongozi wa kiserikali mkoani Mtwara na
Lindi na wale wa serikali kuu kuitumia vizuri fursa za vikao wanavyokaa
kujadiliana namna ya kumaliza matatizo na umasikini wa wananchi, kuliko
kupoteza muda wakijitungia propaganda za kukishutumu chama hicho.