UPEPO
mbaya ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unazidi kuvuma, safari hii
wabunge wake wakimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi mawaziri
watatu.Mawaziri
wanaotakiwa kung’olewa ni Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu na Mafunzo ya
Ufundi), Dk. Mathayo David Mathayo (Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi) na Dk.
Fenella Mukangara (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).
Kama Rais
Kikwete atakubali kuwaondoa madarakani mawaziri hao, hii itakuwa mara
ya pili kwake kufanya hivyo. Mara ya kwanza ilikuwa Mei mwaka jana.
Mwaka
jana Rais Kikwete aliamua kuwaengua madarakani baadhi ya mawaziri
waliokuwa wakiandamwa kwa tuhuma mbalimbali, ikiwemo uwajibikaji mbovu.
Miongoni
mwa walioenguliwa mwaka jana ni Dk. Haji Mponda aliyekuwa Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Mustafa Mkulo (Waziri wa Fedha), William Ngeleja
(Nishati na Madini na Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii).
Msimamo
huo wa wabunge wameutoa jana katika kikao baina yao na Rais Kikwete
kilichokuwa kikitathimini mwenendo wa chama na utendaji wa wabunge.
Chanzo
chetu ndani ya kikao hicho kilieleza kuwa baada ya Rais Kikwete kutoa
hotuba ya ufunguzi, baadhi ya wabunge walianza kuchangia, huku wengine
wakishutumiana kwa kuvujisha siri za vikao nje kwa waandishi wa habari.
Wabunge hao walidai kuwa mawaziri hao watatu wamekuwa mzigo kwa Serikali ya CCM kutokana na utendaji wao kutokuwa wa kuridhisha.
Walisema matunda ya uwepo wa mawaziri hao kwenye wizara husika hayaonekeni, hivyo kumtaka Rais Kikwete awang’oe.
Waziri
Kawambwa analaumiwa kwa kuzembea kwenye sekta ya elimu ambayo inazidi
kushuka kiasi cha kuifanya serikali ifute matokeo ya kidato cha nne ya
mwaka jana.
Walisema
kufutwa kwa matokeo hayo ambayo asilimia 60 ya waliofanya mtihani
walipata daraja sifuri, kunadhihirisha uwezo mdogo wa Dk. Kawambwa.
Wakati Kawambwa akibanwa kwa hilo, wenzake Mathayo na Mukangara wanadaiwa kuwepo wizarani bila kuonesha ufanisi wowote.
Wabunge
hao walidai kuwa Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi anayoiongoza Dk.
Mathayo ni nyeti na ilipaswa kuwa ya pili katika kuchangia pato la
taifa baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Walimshambulia
Dk. Mathayo kuwa mzigo kwa wizara hiyo kwani alipokuwepo Dk. Magufuli
(Waziri wa Ujenzi) ilikuwa ikifanya vizuri tofauti na hivi sasa.
“Tusioneane aibu, huyu Mathayo ameshindwa kazi, mwenyekiti muondoe kabla mambo hayajazidi kuwa mabaya,” alisema mbunge mmoja.
JK abariki mchakato wa urais
Mapema
katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho, Rais Kikwete aliruhusu
makundi ya wana-CCM wanaotaka kuwania urais 2015 kuendelea na mchakato
wa kuweka mikakati yao ya kampeni bila chuki.
Kwa
mujibu wa chanzo chetu katika kikao hicho ambacho waandishi
hawakuruhusiwa kuingia, lengo kubwa lilikuwa ni kujadili masuala
mbalimbali ya kitaifa ikiwemo utekelezaji wa ilani ya uchaguzi katika
majimbo ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na ahadi za rais.
Rais
Kikwete aliwataka wana-CCM wenye nia ya kugombea urais kuendelea na
mikakati yao kwa ustaarabu na kuepusha uadui kutokana na wapambe wao
kuwa na kambi zaidi ya moja.
“Tuangalie
makundi ya urais 2015 yasishambuliane kwa kuvunja chama, wenye nia hiyo
ya kugombea waendelee na mikakati yao na si kujenga chuki kwa makundi
mengine.
“Mkumbuke kuwa kambi hizo za urais zinatakiwa kujitizama na wafuasi wao maana wafuasi wengi si wa kuaminika,” alisema Kikwete.
Rais
Kikwete aliwafananisha baadhi ya wapambe na matango pori yanayoota
popote, ambapo alisema wamekuwa na tabia ya kutoa maneno huku na
kupeleka upande wa pili.
Tanzania
Daima ilidokezwa kuwa Kikwete alikuwa na ajenda nne ambazo ni urais
2015, kuwahimiza wabunge kutembelea majimbo yao ya uchaguzi, kurudi
majimboni kwao kusimamia ahadi zao, chama na zile za viongozi wa kitaifa
akiwemo yeye na kuisimamia serikali na kuikosoa bila kuibomoa.
Kwamba Kikwete aliwataka wabunge hao kutumia kauli za staha wanapoikosoa serikali kama ambavyo baadhi wamekuwa wakifanya.
“Mnatakiwa
kuisimamia serikali na kuikosoa bila kuibomoa, lakini kuna baadhi yenu
mmekuwa mnaibomoa serikali kwa jinsi mnavyochangia huko bungeni, hilo si
jambo jema hata kidogo, waachieni wale wenzenu,” alisema.
Katika
hilo, wabunge walionya tabia ya baadhi ya mawaziri wanavyohusiana na
wabunge na wanavyoonekana kwa wananchi, lakini wakaitaka serikali
kutimiza wajibu wake ipasavyo kwa kutoa fedha za bajeti kama
zinavyopitishwa na Bunge.
Pia
ubadhirifu unaofanywa kwenye halmashauri nchini, utendaji mbovu wa
baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa nchini, hivyo wakamtaka rais kukunjua
makucha yake kuondokana na uozo huo.
Kuhusu
kutembelea majimbo, rais alisema kuwa baadhi ya wabunge wameyatelekeza
kwa kutorudi kusikiliza kero za wananchi na kutimiza ahadi zao.
Aliwaonya kuwa kwa tabia hiyo wala wasije kuwaonea donge wale wanachama wengine watakaochaguliwa kuwa wabunge badala yao.
Lugola, Filikunjombe, Mpina wakaangwa
Baada ya
mapumziko ya mchana, kikao hicho kiliendelea kwa wabunge kutoa
madukuduku yao ambapo chanzo chetu kinasema kuwa wabunge watatu
walishambuliwa kwa tabia yao ya kuikosoa serikali kwa kauli nzito.
Wabunge
hao ni Kangi Lugola (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa) na Luhaga Mpina
wa Kisesa ambao hata hivyo wote hawakuhudhuria kikao hicho.
Lugola
amekuwa mwiba mkali wa kuwashambulia mawaziri wa serikali kutokana na
utendaji wao kutoridhisha ambapo hivi karibuni wakati akichangia hotuba
ya bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), alitishia
kuwataja mawaziri na watendaji wanojihusisha na rushwa pamoja na
biashara ya dawa za kulevya.
Filikunjombe
naye amekuwa akipinga kuunga mkono hoja za serikali huku akitumia
maneno makali kama vile ‘serikali kuvaa miwani ya mbao’, kutokuwa sikivu
na mengine kama hayo ambayo inaelezwa kuwa hata Rais Kikwete jana
aliyatolea mfano.
Chanzo
chetu kilieleza kuwa aliyeibua sakata hilo ni mbunge mmoja wa Tabora,
akidai wenzao hao wamekuwa na tabia isiyokoma, na hivyo kupendekeza kuwa
kama wanataka ni heri wakahamia upinzani kuliko kuendelea kuivua nguo
Serikali ya CCM.
Hadi
tunakwenda mitamboni jana, kikao hicho kilikuwa kikiendelea na kwa
mujibu wa ofisa mmoja wa chama, walitarajia kuwa kingemalizika usiku wa
manane.
via tanzania daima