Kanuni ya 37 (1), inasomeka: “… ili ibara au
Rasimu iweze kupitishwa itahitaji kuungwa mkono na wingi wa theluthi
mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili toka Zanzibar”.
Taarifa zisizo rasmi zinasema ili kuwezesha
kupatikana kwa theluthi mbili kutoka upande wa Tanzania Visiwani CCM
walikuwa wakihitaji kupata kura 16 ikilinganishwa na idadi yao ya sasa
ya wanaounga mkono.
Kamati ya Uongozi
Harakati zinazofanywa na Sitta zimekuja saa chache
tangu kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu,
ambacho habari zinasema kilimwelekeza kiongozi huyo kufanya jitihada za
kutatua mgogoro uliopo.
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis
Hamad alisema kikao cha Kamati ya Uongozi hakikufikia uamuzi kuhusiana
na wajumbe wanaounda Ukawa kutoka bungeni kwa sababu hawajapata taarifa
ya nini kilichowafanya waondoke.
“Hakuna cha kushika hapa, hatukujua kwa nini
walitoka bungeni lakini Mwenyekiti (Sitta) alikuwa akiwatafuta ili kujua
sababu za kutoka kwao bungeni,” alisema Hamad na kuongeza: “Mwenyekiti
anawatafuta na tulikubaliana wakipatikana atatuita ili tuzungumze,”
alisema Hamad.
Hamad alimnukuu Sitta kuwa milango iko wazi kwa
Ukawa kwa mazungumzo. Pia alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda yuko tayari
kuzungumza nao ili kufikia mwafaka kuhusiana na tatizo ambalo
limewafanya kutoka bungeni.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho aliliambia gazeti
hili kuwa: “Kimsingi tulikubaliana wote katika kikao kwamba bila wenzetu
hatuwezi kupata Katiba Mpya, kwa hiyo tulimwomba mwenyekiti (Sitta)
awatafute viongozi wa Ukawa ili afahamu msimamo na mwelekeo wao na
ikiwezekana waanze mazungumzo.”
Mjumbe huyo aliongeza: “Tulishauri pia kwamba
Mwenyekiti awafahamishe wakubwa walioko serikalini kuona jinsi gani
wanaweza kuwatafuta wenzao ili watafute mwafaka, maana hali tuliyofikia
ni mbaya.”
Alisema ilishauriwa kwamba zitafutwe njia za
kumhusisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Zanzibar, Seif Sharif Hamad kama hatua ya kushawishi upande wa Ukawa
kulegeza msimamo wao.
Mjumbe mwingine alisema katika kikao hicho
yalitolewa mapendekezo kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ifanyiwe
marekebisho ili kuruhusu kufanyika kuwa kura ya maoni kwa sura mbili; ya
kwanza na ya sita za Rasimu ya Katiba, lakini wazo hilo lilipingwa.
“Hilo wazo lilitolewa sawa, lakini lilionekana
kama halitafaa kwa sababu kimsingi hata kura zikipigwa baina ya serikali
mbili na tatu, matokeo ya Zanzibar yanafahamika, kwa hiyo tuliona jambo
la msingi ni kufanyika kwa mazungumzo,” alifafanua mjumbe huyo.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi