LEO tungependa kupitia kwenu kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi
wetu wa Uwanja wa kisasa wa mpira katika Jiji la Jangwani kama
itakavyojulikana
Mara ya mwisho tuliongea ama kuonana ilikuwa mwezi wa tatu wakati
Ndugu zetu wa BCEG walipokabizi Concept design ama Usanifu wa awali na
kuanzia sasa tutakuwa tunatoa taarifa za mara kwa mara kuhusu mradi huu.
Wahenga walisema UKICHA KUSEMA HUTATENDA JAMBO lakini pia KUKAA KIMYA
SANA kunajenga hisia mbaya na kutoa nafasi ya upotoshwaji wa habari.
Kwa kifupi napenda kuwakumbusha kuwa Makubalino ya Awali (Memorandum
of Understanding) yalisainiwa 23 Novemba 2012. Pamoja na mengineyo YANGA
inatakiwa:
· Kupata na kuwa na eneo la kutoshereza malengo ya mradi
· Kupata ushauri mzuri, michoro mizuri na mkandarasi mzuri wa mradi
· Kupata na kutenga fedha za kukamilisha usanifu na ujenzi wa mradi
Kwa upande wa BCEG wajibu wao ni kuwa na utaalamu na uzoefu wa
kutosha. BCEG wameandaa na kukabidhi michoro ya usanifu wa awali kukidhi
matakwa ya YANGA. YANGA tunatakiwa kutoa maoni yetu na na kuingia RASMI
mkataba wa ujenzi.
Kutokana na kukua kwa Jiji la Dar es Salaam, na katika hali ya kutaka
klabu iwe na vitega uchumi klabu imeonelea ni vyema kama ingekuwa na
uwanja wa mpira wa karne ya sasa na baadaye ambao pamoja na mambo
mengine utakuwa na mioundombinu ifuatayo:-
1. Uwanja wa mpira wenye viti 40,000
2. Hostel ya wachezaji na football academy ya vijana
3. Viwanja vya mazoezi
4. Uwanja wa kutosha kuegesha magari
5. Hoteli na sehemu ya makazi
6. Ukumbi wa mikutano
7. Sehemu ya maofisi, benki, zahanati (sports clinic)
8. Maduka, supermarket na sinema
9. Sehemu za kubarizi, kupumzikia (Recretional and Open spaces)
Mara baada ya azma yetu kukamilika eneo hili litaitwa “Jangwani City”
na kufanya wakazi wa maeneo ya Jangwani na sehemu za jirani wasiende
maeneo ya mbali kutafuta huduma muhimu za kijamii. Eneo hili litaboresha
mandhari nzima ya Jangwani kwa kukuza mazingira na miundombinu. Hii
itahusu pamoja na mambo mengine ujazaji udongo (tuta kubwa), upandaji
miti, bustani za kubarizi, kuboresha mifereji ya majitaka na kudhibiti
mafuriko ya eneo la Jangwani na hivyo kulipatia sura ya kibiashara na
kitalii.
Ili kukamilisha azma ya kuwa na Jangwani City itakayo kuwa na
miundombinu yote hiyo, Uongozi ulipeleka maombi ya eneo la nyongeza
Manispaa ya Ilala na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
barua zenye kumbukumbu namba YASC/ARDHI/MWK/YM/46/2012 na
YASC/ARDHI/MWK/YM/47/2012 za 12 Desemba 2012, na mpaka sasa bado maombi
yetu hayajajibiwa.
Mwezi wa saba, Wadhamini/Uongozi wa YANGA walimwandikia Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuomba msaada wake kufanikisha maombi ya
nyongeza ya kiwanja yaliyowasilishwa Manispaa ya Ilala na Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Klabu ya Yanga ina kiwanja chenye ukubwa wa hekta 3.59 eneo la
Jangwani. Kiwanja hiki kina hati miliki kwa miaka 99 toka mwaka 1972 na
katika eneo hilo, klabu ilifanikiwa kujenga uwanja wa mpira wa Kaunda na
Jengo la klabu la ghorofa tatu. Jengo hili lilijengwa kwa ufadhili
mkubwa sana wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume (Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi) na michango ya
wanachama na wapenzi wa klabu ambao kila siku wamekuwa wakiamini kuwa
haba na haba hujaza kibaba.
Ndugu Wandishi wa habari kwa kifupi tumefikia hapo, zoezi la kutoa
maoni yetu kuhusu michoro ya usanifu wa awali na kuingia rasmi mkataba
wa ujenzi na BCEG limesimama, likisubiri majibu ya nyongeza la eneo. Ni
matumaini yetu zoezi hili litakamilika hivi karibuni na kuendelea na
mradi.
YANGA DAIMA MBELE NYUMA MWIKO
Dar es Salaam, 30 September 2013
Francis Mponjoli Kifukwe