Vikosi
vya usalama vya Kituruki na Kisomali nje ya jengo la ubalozi wa Uturuki
baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kulilipua lango la jengo hilo.
[Majid Ahmed/Sabahi]
l-Shabaab
inatekeleza ahadi yake ya kuendeleza ghasia wakati wa Ramadhani huku
mashambulizi ya mwisho kabisa yakiwa ni kwenye Ubalozi wa Uturuki mjini
Mogadishu mwishoni mwa wiki.
Mara moja
viongozi wa Somalia na Uturuki waliyalaani mashambulizi hayo, na kuapa
kwamba yasingeliitikisa nia yao ya kupambana na ugaidi na kujenga
ushirikiano ambao nchi hizo mbili zimeuunda kwa miaka michache
iliyopita.
Kiasi cha
watu sita waliuawa kwenye mashambulizi hayo, ikiwa ni pamoja na mlinzi
wa Kituruki, raia wawili wa Kisomali na wanamgambo watatu wa al-Shabaab,
mfanyakazi wa ubalozi huo Abdi Mohamed aliiambia Sabahi. Watu tisa
walijeruhiwa, wakiwemo maafisa wanne wa kikosi cha usalama cha Uturuki
waliokuwa kwenye zamu ya kulinda jengo hilo.
Mashambulizi
hayo yalianza pale mlipuaji wa kujitoa mhanga wa al-Shabaab alipolilipua
gari lenye mabomu kwenye lango la kuingilia jengo hilo. Kisha
wapiganaji wawili wenye silaha wa al-Shabaab walijaribu kuingia kwenye
jengo hilo lakini walikabiliwa na vikosi vya usalama vya Uturuki na
kuuawa kabla ya kulifikia jengo, kwa mujibu wa wafanyakazi wa Kisomali
wanaofanya kazi kwenye ubalozi wa Uturuki ambao walizungumza na Sabahi.
Mtu aliyejeruhiwa vibaya akiwekwa ndani ya gari ya wagonjwa muda mfupi baada ya mashambulizi ya bomu. [Majid Ahmed/Sabahi]
Katika jaribio la kuhalalisha mashambulizi hayo, al-Shabaab ilituma
ujumbe kwenye Twitter ikiitaja Uturuki "nchi isiyo ya Kiislamu".
"Waturuki
ni sehemu ya kundi la mataifa yanayoiunga mkono serikali ya kikafiri na
yanayojaribu kukandamiza uanzishwaji wa mfumo wa Sharia ya Kiislamu,"
ulisema ujumbe huo.
Msemaji
wa al-Shabaab, Ali Mohamud Rage, aliapa kwamba kundi hilo la wanamgambo
litaendelea kuwalenga raia wa Uturuki nchini Somalia.
"Mujahidina
wataendeleza mashambulizi yao yanayowalenga maafisa wa serikali ya
Uturuki mjini Mogadishu hadi Uturuki itakapoacha kuingilia mambo ya
ndani ya Somalia," alisema Rage kwenye taarifa iliyotangazwa na Redio
Andalus, inayotumiwa na kundi hilo.
Rage
aliwaelezea wafanyakazi wa huduma za dharura na wanadiplomasia wa
Kituruki nchini Somalia kama makafiri "ambao kwa hakika wamewasababishia
Waislamu, hasa nchini Somalia, matatizo mengi na kupanga njama dhidi
yao."
"Inawezekana
kuwa watu wengi watajiuliza kwa nini watu wa Uturuki, ambao ni
Waislamu, walishambuliwa, lakini tunataka kuwawekea watu wazi kwamba
Uturuki imeutelekeza Uislamu na dini ya Mungu," alisema. "Wameishambulia
nyumba ya Waislamu."
Uvamizi usio wa haki
Shambulio
hilo lilisababisha malalamiko kutoka sehemu kubwa ya viongozi wa
Somalia, Uturuki na wa kimataifa, pamoja na kutoka kwa raia wa Somalia.
"Shambullio
hilo dhidi ya waajiriwa wa Uturuki ambao walikuja Somalia kusaidia
Wasomali haliwezi kuhalalishwa hata kidogo," alisema Mohamed Osman,
ofisa mstaafu kutoka Shirika la Upelelezi na Usalama la Taifa.
"Waajiriwa
wa Uturuki ambao walikuwa walengwa katika shambulio hili la kutisha
siyo tu askari lakini raia ambao wanafanya shaghuli za kihalali za
kibinadamu katika nchi yetu," Osman aliiambia Sabahi. "Wamekuwa
wakifanya kazi usiku na mchana kusaidia watu wa Somalia na kwa hiyo
kitendo hiki cha kutisha sana hakiwezi kuhalalishwa kwa namna yoyote
ile."
"Wasomali
wote wanalaani kitendo hiki kibaya, ambacho kinaonyesha makusudio
mabaya ya magaidi," alisema. "Shambulio hili dhidi ya waajiriwa wa
Uturuki huko Mogadishu linawakilisha shambulio dhidi ya watu wa
Somalia."
Rais wa
Somalia Hassan Sheikh Mohamud alielezea shambulio hili kama "kiitendo
cha uoga wa kukata tamaa na magaidi ambao hawajali lolote kwa ajili ya
amani au utulivu wa Somalia", alisema wakati akitoa rambirambi zake kwa
watu na serikali ya Uturuki.
"Ninalaani
kitendo hiki cha jinai cha ugaidi na serikali yangu na vikosi vya
usalama vitafanya kila kinachowezekana kuwakamata waliopanga na
kuielekeza," Mohamud alisema katika taarifa mara tu baada ya shambulio.
"Lazima
tuendelee kusimama imara dhidi ya wale wanaotafuta kuharibu nchi hii na,
kwa msaada wa kijasiri wa washirika wetu, lazima tuongeze jitihada zetu
mara mbili ili kutoa siku zijazo za amani kwa watu wa Somalia ambao
wanahitaji sana," alisema.
Mohamud
aliusifu msaada wa Uturuki kwa Somalia, akiitaja serikali ya Uturuki
moja kati ya "mshirika anayetumainiwa na kutegemewa wa Somalia".
Uturuki
ilianzisha kampeni kubwa ya kidiplomasia na kibinadamu miaka miwili
iliyopita na imetoa mchango mkubwa katika jitihada za ujenzi mpya katika
Somalia.
Shirika
la ndege la Uturuki lilikuwa shirika la kwanza la kimataifa katika
miongo miwili kufanya safari za mara kwa mara kwenda Mogadishu na kuna
mamia ya wafanyakazi wa misaada wa Uturuki huko Mogadishu.
"Waturuki
wengi wamekuja Somalia kusaidia kujenga tena kwetu," Mohamud alisema.
"Tuna shule mpya na hospitali kwa sababu ya kazi yao ya kipekee."
Hitilafu ya Al-Shabaab
"Kitendo
hiki kinathibitisha tena kinyume cha kile vikundi vya wanamgambo magaidi
vinachodai vinapigania," alisema Omar Foodaadi,mwenye miaka 49,
mchambuzi wa mambo ya siasa huko Mogadishu.
"Al-Shabaab
ingewaeleza wafuasi wake kwamba inaendesha vita vitakatifu dhidi ya
makafiri lakini ukweli ilikuwa inawalenga Waislamu wasio na hatia wakati
wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuwa ilionyesha wazi, kwa mara
nyingine, inapuuza maisha ya binadamu kwa kuwalenga raia wasio na hatia
kutoka katika nchi ya Waislamu," alisema.
"Magaidi
wakati wote wanajaribu kuzuia maendeleo ambayo Somalia inayapata kwa
sababu hawataki kuanzishwa kwa taifa la Somalia," Foodaadi aliiambia
Sabahi. "Ni watu wanaofaidika na vurugu lakini vurugu hazidumu milele."
Watu huko
Mogadishu walionyesha wasiwasi wao kuhusu vitisho na mashambulio ya
mauaji yasiyobagua ya al-Shabaab yanayowaumiza wananchi.
"Nilishtushwa
sana niliposikia habari kuhusu shambulio la mauaji na vitisho ambavyo
al-Shabaab wanafanya dhidi ya mashirika ya kutoa misaada ya Uturuki
ambayo yamekuwa yakitusaidia," Adam Bile, baba wa watoto wanne mwenye
umri wa miaka 56 ambaye anaishi katika kambi kwa ajili ya watu wasiokuwa
na makazi za Tarabuunka huko Mogadishu, aliiambia Sabahi. "Hawa ni
ndugu zetu wa Kiislamu na ninaona hili kama jeraha kwa mahitaji yetu ya
msaada kutoka kwa Waislamu."
Amina
Hirsi, mama wa watoto saba mwenye umri wa miaka 41 anayeishi katika
kambi ya Badbado huko Mogadishu, alihoji azma ya al-Shabaab kulenga
wafanyakazi wa kutoa misaada wa Kituruki na wanadiplomasia.
"Nimechanganyikiwa
kuhusu kama viongozi wa al-Shabaab wamepoteza mwelekeo walipoondolewa
Mogadishu na kuona mabadiliko ya usalama na kurejea kwa upatikanaji wa
misaada kwa watu, au kama hawawezi kuelewa maana ya malengo ya kidini
wanayodai kuyapigania," aliiambia Sabahi.
"Samahani kwamba magaidi wa al-Shabaab waliwashambulia ndugu zetu Waturuki," alisema.
"Lolote
lililotokea, ninaamini tulihisi maumivu yale yale kama ndugu zetu wa
Uturuki walivyohisi," alisema Habiba Dahir, mama wa watoto watatu mwenye
umri wa miaka 35 ambaye anaishi katia kambi ya Badbado.
"Nilitambua
wakati al-Shabaab waliposhambulia ndugu zetu wa Kiislamu kwamba
inathibitisha jinsi al-Shabaab wanavyotaka kuumiza na kumdhuru Muislamu
yeyote anayetaka kutusaidia," aliiambia Sabahi. "Wamepoteza mwelekeo wa
jihad ambayo Mungu alifafanua kwetu katika dini. Ningesema kwa mataifa
ya Kiislamu, yasisimame na kuangalia tu matatizo ambayo al-Shabaab
wanatuumiza nayo, lakini yajaribu kutusaidia."
Mshikamano ni imara baina ya Somalia, Uturuki
Waziri
Mkuu wa Somalia Abdi Farah Shirdon, Waziri wa Mambo ya Ndani Abdikarin
Hussein Gulled, Waziri wa Ulinzi Abdihakin Haji Mohamud Fiqi, Waziri wa
Fedha Mohamud Awil Suleiman na maafisa wengine wa serikali ya Somalia
walitembelea eneo la mlipuko siku ya Jumapili ili kuonesha mshikamano
wao na Uturuki na kulaani shambulio hilo la kujitoa mhanga.
"Tendo
kama hilo la kigaidi lililoshindwa halitaathiri uhusiano baina ya
Somalia na Uturuki na halitarejesha nyuma njia ya mafanikio, ambayo
yamekuwa yakipatikana Somalia yote," Shirdon alisema katika mkutano wa
pamoja kwa waandishi wa habari pamoja na Balozi wa Uturuki Somalia Kani
Torun.
Shirdon
pia alitilia mkazo mshikamano wa watu wa Somalia na serikali yake kwa
familia za wahanga wa Kituruki waliopoteza wapendwa wao kutokana na
shambulio hili.
"Katu
hatutasimamisha juhudi zetu bila ya kuchoka za kuwasaidia watu wa
Somalia ili warejee hali zao baada ya miaka ya misukosuko na miradi
inayoendelea ya maendeleo inayofadhiliwa na Uturuki itamalizwa," Torun
alisema.
Mkurugenzi
Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa Hussein Abdi
Aden alisema serikali imedhamiria kulinda misheni za kigeni zilizoko
Somalia.
"Kuwalenga
waajiriwa wa kiraia kunaonesha ukosefu wa heshima kwa upande wa magaidi
kwa maisha ya binadamu na wanadiplomasia wa kigeni ambao wamekuja
Somalia kuwasaidia watu wetu," aliiambia Sabahi.
"Tendo hili
la kigaidi lina sifa ya kiwango kikubwa cha uoga," alisema. "Magaidi
wanawalenga wafanyakazi wa kiraia wa Uturuki kwa sababu ya jukumu la
Uturuki katika kuwasaidia watu wa Somalia."
Chanzo: sabahionline.com