Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Friday, June 14, 2013

UTARATIBU WA UTOAJI LESENI ZA USAFIRISHAJI WA ABIRIA KWA MAGARI YANAYOBEBA ABIRIA KUANZIA 7 HADI 14


Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) inapenda kuufahamisha  umma  kuwa kuanzia tarehe 1 Juni, 2013, SUMATRA ilianza kutoa leseni za kusafirisha abiria kwa magari yenye uwezo wa kubeba abiria kuanzia 7 hadi 14.

Hatua hii imefikiwa na SUMATRA ili kuimarisha udhibiti katika sekta hii  ya usafiri ambapo huduma ya usafirishaji abiria kwa kutumia mabasi madogo yanayobeba abiria kuanzia 7 hadi 14 yanatoa huduma bora, salama na yanakidhi viwango. Aidha hatua hii imekusudiwa kusaidia wamiliki kufanya biashara ya usafirishaji kwa weledi na ufanisi zaidi na mdhibiti kuwasimamia watoa huduma hao na hivyo kuimarisha shughuli za udhibiti ili kuwa na usafiri bora na salama kwa wananchi wa Tanzania.


Ili kufanikisha utoaji leseni kwa ajili ya usafirishaji wa abiria, wamiliki wa magari hayo ambayo yanajumuisha magari aina ya NOAH   wameelekezwa kuzingatia yafuatayo:

1) Magari husika yawe na madirisha ya kufunguka na kufunga kwa ajili ya kuingiza hewa ya kutosha.
 
2) Mlango wa abiria uwe upande wa kushoto tu na endapo gari lina mlango upande wa kulia, mlango huo uzibwe  moja kwa moja kwa ajili ya usalama kama ilivyobainishwa katika Kanuni za SUMATRA za Viwango vya Ufundi, Usalama  na Ubora wa Huduma  wa Magari ya Abiria, 2008. 

3)   Magari hayo yawe na sehemu maalumu ya watu kupita wakati wa dharura tofauti na mlango wa kuingilia abiria. 

4)   Magari hayo yataruhusiwa kutoa huduma ya usafirishaji abiria kwenye maeneo yenye upungufu wa huduma  za usafiri na kwa umbali usiozidi kilometa hamsini (50) . 

5)Magari hayo hayatapewa leseni kutoa huduma kwenye majiji ambayo Mamlaka tayari imeshachukua hatua za kukataza matumizi ya magari ya uwezo huo kwa ajili ya kuondoa msongamano.

6) Magari yatakayopata leseni ya kusafirisha abiria yatapaswa kupakwa rangi maalum kwa ajili ya utambulisho wa gari la abiria na utambuzi wa njia kama itakavyoelekezwa na SUMATRA.

7)Magari yatakayopewa leseni ya kusafirisha abiria yatapaswa kutumia nauli zilizopitishwa na kutangazwa na SUMATRA.

SUMATRA itatoa leseni ya usafirishaji wa abiria baada ya mmiliki wa gari husika kukamilisha matakwa yote yaliyotolewa hapo juu.

Tungependa wananchi na wadau kwa ujumla waelewe kwamba, leseni ni nyenzo muhimu ya udhibiti.
Faida za leseni ya usafirishaji ni pamoja na:

1. Leseni humsaidia Mdhibiti kama SUMATRA kuwa na taarifa sahihi za watoa huduma ikiwa ni pamoja na anuani zao hivyo kuweza kuwafikia kiurahisi katika masuala kama vile mafunzo n.k.
 
2.Leseni humsaidia Mdhibiti kuweka utaratibu muafaka wa utoaji huduma kwa kuhakikisha unakuwa salama na bora.
 
3.Leseni husaidia katika kubaini upatikanaji wa huduma katika maeneo mbalimbali.
 
4.Leseni ni utambulisho na hivyo humsaidia mtoa huduma kutoa huduma bila bughudha.
 
5.Leseni husaidia umma kuwatambua watoa huduma halali na hivyo kuwatumia.
 
6.Leseni husaidia katika masuala ya fidia za bima.
 
7.Leseni ni uthibitisho kwamba chombo cha usafiri ni salama na kinafaa kwa kutoa huduma ya usafiri. 

Hivyo tunatoa wito kwa watoa huduma kukata leseni ya usafirishaji ili waweze kufaidika na faida zilizotajwa hapo juu.

SUMATRA imekuwa ikifanya kazi karibu sana na Jeshi la Polisi kama msimamizi mkuu wa utekelezaji wa Sheria hapa nchini. Pale ambapo taarifa za Polisi zinapothibitisha ukiukwaji wa sheria, hatua za kisheria huchukuliwa na mdhibiti (SUMATRA).

Kutokana na hali hii tunapenda kuwafahamisha wamiliki wa mabasi madogo ya abiria 7 hadi 14 na umma kwa ujumla kuwa SUMATRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani watafanya ukaguzi kwa magari yote yasiyo na leseni za usafirishaji ili kuhakikisha mabasi yote yanayotoa huduma ya usafiri kwa umma yana leseni halali ya usafirishaji abiria na kufuata Sheria, Kanuni na Masharti yote yaliyobainishwa katika leseni hiyo.

Ni vyema wamiliki wa vyombo vya usafiri hususan wa mabasi madogo kuzingatia na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo kwa ajili ya maslahi ya muda mrefu na yenye tija kwao kama watoa huduma na kwa sekta ya usafirishaji abiria hapa nchini.

Kwa kushirikiana tunaweza kuwa na usafiri bora na salama!

 Imetolewa na:
Meneja Mawasiliano
SUMATRA
Juni, 2013
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...