JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS
TUME YA UTUMISHI WA UMMA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAKALA NA MAMLAKA ZA SERIKALI ZIMEHIMIZWA KUWEKA MIKAKATI YA KUJIENDESHA KWA FAIDA BILA KUITEGEMEA SERIKALI
Wakala
na Mamlaka za Serikali wamehizwa kuweka mikakati ya kujiendesha kwa
faida, kuwa wabunifu, wakabiliane na changamoto zilizopo na pia
watekeleze majukumu yao kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu
zilizowekwa bila kutegemea fedha kutoka Serikalini. Wametakiwa katika
mipango na malengo yao, vipaumbele vyao viwe ni rasilimali watu,
matumizi bora ya rasilimali fedha na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kwa kufanya hivyo, adhma ya Serikali ya kuzifanya Wakala na Mamlaka
zijitegemee zenyewe itaweza kufikiwa endapo wataongeza uzalishaji na
hatimaye mchango wao kwa Taifa utaonekana kupitia maendeleo
yatakayopatikana.
Hayo
yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma katika Ofisi ya
Rais, Bwana Jovin Kitambi kwa nyakati tofauti jijini Dar es
Salaam wakati akizungumza na Menejimenti na Watumishi wa Wakala wa
Huduma ya Umeme, Mitambo na Huduma za Elekronikia Tanzania (TEMESA),
Mamlaka ya Usafiri na Usalama wa Anga Tanzania (TCAA) na Wakala wa Vyuo
vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA).
“Miongoni
mwa sababu zilizosababisha Mashirika mengi yaliyokuwa yanamilikiwa na
Serikali kufa ni kutokana na kuwepo kwa Menejimenti mbovu zilizokuwa
zimepewa dhamana ya kusimamia mashirika hayo. Hivyo, Serikali iliamua
kuunda Wakala na Mamlaka mbalimbali kwa lengo la kuona zinajiendesha kwa
faida, kwa ufanisi na zinatoa huduma bora. Serikali haitakuwa tayari
kuona Wakala na Mamlaka zilizoanzishwa zinakufa kutokana na Menejimenti
mbovu” amesema Kitambi.
Kitambi
amesema “hivi sasa kumekuwa na ubadhilifu baadhi yenu mnakusanya mapato
mnayachezeachezea kwa kuwa na matumizi mabovu. Simamieni rasilimali
watu, nidhamu na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yenu ili muweze
kuisaidia Serikali na lengo la nyinyi kuwa Wakala na Mamlaka liweze
kuwa na tija. Ni lazima mjiendeshe kwa faida, ufanisi na mnakuwa
wabunifu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo na hatimaye
muweze kutoa mchango wenu kwa kuleta maendeleo ya nchi hasa pale
mtakapoweza kukusanya mapato na kuyaelekeza katika matumizi ya
maendeleo”.
“Wakala
na Mamlaka za Serikali ni Watumishi wa umma hapa nchini, miongoni mwenu
mnalalamikiwa sana na wananchi kwa jinsi mnavyotoa huduma zenu
na maadili ya kazi yamekuwa hayasimamiwi vizuri. Hivyo ni lazima
mbadilike, msifanye kazi kwa mazoea, hakikisheni mnaendesha shughuli
zenu mkiwa watumishi wa umma kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu
zilizopo. Kwa kufanya hivyo, mtakuwa mnatimiza wajibu wenu ipasavyo na
mnaisaidia Serikali. Pia mtakuwa mmeondoa malalamiko mengi ya wananchi
kuhusu utendaji kazi wa watumishi wa umma” amesisitiza bwana Kitambi.
“Ni
aibu sana kwa mtumishi wa umma kupatikana na makosa ya uvunjaji wa
Sheria anapotekeleza majukumu yake kwa kwenda kinyume na maadili ya
msingi. Kuna baadhi ya watumishi wamechukuliwa hatua za kinidhamu kwa
kutenda makosa mbalimbali mfano kudai na kuopokea rushwa, ubadhirifu,
wizi wa mali ya umma, utoro kazini, ubakaji, kudanganya na kuajiliwa
kinyume na sifa na hali hii inaitia doa kubwa Serikali” amesema.
Kitambi
amesema Tume za Utumishi wa Umma zipo karibu nchi zote duniani na
zimeanzishwa kwa lengo la kusimamia uendeshaji wa rasilimali watu katika
utumishi wa umma na kuhakikisha unaleta tija. Amewataka Waajiri,Mamlaka
za Ajira na Nidhamu kuzisimamia Sheria, Maadili na Nidhamu.
“Waajiri
na Watendaji Wakuu mnapaswa mfahamu kuwa rasilimali watu ni muhimu sana
katika maendeleo ya Wakala na Mamlaka zenu. Utumishi wa umma hauongozwi
hivi hivi tu, unaongozwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu, na
tunapozikiuka tunazua malalamiko mengi kwa wananchi. Wasimamieni
watumishi walio chini yenu ipasavyo kwa kuhakikisha kila mtumishi wa
Wakala na Mamlaka anapangiwa majukumu ya kufanya kulingana na taaluma
yake, kunakuwepo na ufuatiliaji, simamieni maadili bila kuona aibu wala
upendeleo, fanyeni kazi kwa misingi iliyowekwa na mkimtendea haki kila
mtumishi. Maana siku hizi kuna malalamiko pia yanatolewa na watumishi
ndani ya Wakala na Mamlaka pale yanapofanywa mambo kienyeji enyeji tu,
matokeo yake ni kupunguza ari kwa watumishi ya kufanya kazi” amesema.
“Waajiri
na Uongozi mzima wa Menejimenti ni lazima maslahi ya watumishi wenu
ikiwemo mishahara yapewe kipaumbele, muwe na mpango wa mafunzo ili
watumishi walio chini yenu waweze kujiendeleza, wapandisheni vyeo
watumishi bila upendeleo, itisheni vikao na watumishi wenu, toeni
maamuzi sahihi kwa wakati, na pia muajiri watumishi kwa kuzingatia
taaluma na sifa. Bila kuyasimamia haya na endapo ikithibitika, Serikali
haitasita kumchukulia hatua Mwajiri au Mtendaji Mkuu yeyote ambae
atakwenda kinyume kwa kutokusimamia Sheria na kutenda haki ipasavyo”
amesisitiza.
Akizungumzia
upande wa waajiri kutokujibu na kutoa ufafanuzi wa kero za wananchi
amesema wananchi wanalalamika wamekuwa wakiandika barua kwa Wakala na
Mamlaka mbalimbali kuhusiana na kero zao lakini wamekuwa hawajibiwi kwa
waajiri kuona kujibu barua si jambo la msingi, amewataka waajiri kujibu
barua kwa wananchi kwa kuzingatia muda waliojiwekea katika mikataba yao
ya huduma kwa wananchi.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Mamlaka ya Usafiri na
Usalama wa Anga Tanzania (TCAA), Bwana Leuben Ruhongole kwa niaba ya
Mtendaji Mkuu amesema, kwa kipindi chote tangu wakiwa Idara ya Usalama
na Usafiri wa Anga baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika mwaka
1977, wamepiga hatua kubwa, mwaka 1999 Serikali iliunda Wakala wa
Usalama wa Anga na kutokana na kuendesha Wakala hiyo kwa faida kupitia
Sheria Namba 10 ya mwaka 2003 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2006
imeweza kuwa Mamlaka kamili kuanzia mwaka 2003.
“Tumefanikiwa
kwa kiasi kikubwa kuiendesha Mamlaka yetu kwa faida na ufanisi mkubwa
kutokana na sisi wenyewe kusimamia majukumu yetu kikamilifu, kwa kufanya
hivyo tumekuwa na makusanyo ya mapato yanayotuwezesha kujiendesha
kupitia tozo mbalimbali tunazotoza ikiwa ni pamoja na kuongoza na kutoa
taarifa za ndege, na pia tunalipwa na ndege husika pale inapokatiza anga
la Tanzania. Tumefanikiwa kujenga jengo la Ofisi yetu linaloitwa
Aviation House lililopo Ukonga Banana kutokana na mapato
yetu. Changamoto kubwa tuliyo nayo sisi kama Mamlaka ni ununuzi wa rada
nyingine mpya ya kuongoza ndege ambayo ni gharama kubwa, kwa sasa
rada iliyopo muda wake umekaribia kumalizika, ambao kwa kawaida muda wa
rada kutumika ni miaka kumi” amesema.
Imetolewa na:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS, TUME YA UTUMISHI WA UMMA
DAR ES SALAAM
25/05/2013