NYUMA ya
habari ya mfanyabiashara tajiri wa Kariakoo jijini, Costa Shirima (47),
anayedaiwa kujirusha kutoka ghorofa ya tisa katika Hoteli ya Concord
iliyopo Kariakoo Mtaa wa Mchikichini, Dar es Salaam na kufariki dunia,
kuna siri ambayo Ijumaa Wikienda limeelezwa.
Wananchi wakiwa eneo alipodondoka marehemu Costa Shirima.
Habari za
kina kutoka hotelini hapo zilieleza kuwa Shirima alikuwa asafiri kwa
ndege ya saa 10:00 jioni, Ijumaa iliyopita kuelekea nchini China kufuata
bidhaa za maduka yake.
ALIMILIKI MADUKA KADHAA
Uchunguzi
wa Ijumaa Wikienda ulibaini kwamba Shirima ambaye alithibitishwa
kufariki dunia baada ya kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar,
alikuwa akimiliki maduka kadhaa ya urembo wa akina mama yaliyopo jirani
na hoteli hiyo ya Concord.
Taarifa
zaidi zilidai kuwa marehemu mara kwa mara alikuwa akipendelea kula
katika hoteli hiyo na siku ya tukio inadaiwa kuwa aliwaeleza watu kuwa
anapanda juu ya hoteli hiyo kupunga upepo.
Ilidaiwa
kuwa jamaa zake walipomhoji kulikoni kwenda kupunga upepo mchana wote
huo, Shirima alisema kuwa alihisi hewa nzito mahali alipokuwa.
Mwili wa
Costa Shirima baada ya kujirusha kutoka ghorofa ya tisa katika Hoteli ya
Concord iliyopo Kariakoo Mtaa wa Mchikichini, jijini Dar.
MHUDUMU AFICHUA MANENO YA MWISHO
Madai
zaidi yalishushwa na mhudumu mmoja wa hoteli hiyo aliyeomba hifadhi ya
jina kuwa jamaa huyo alipoingia mahali hapo, alitaka kupatiwa chumba cha
kupumzika lakini alipopelekwa kwenye vyumba vya ghorofa ya kwanza
alikataa hadi alipofika ya tisa na kuanza kupunga upepo.
Mhudumu
huyo alidai kuwa alikuwa akimsikia Shirima akiongea peke yake akisema
“Haiwezekani… haiwezekani kabisa…” na baadaye alipokea simu ya kiganjani
ambayo alisikika akibishana na mtu wa upande wa pili.
Kwa kuwa
kila mtu alikuwa na shughuli zake, inadaiwa kuwa ghafla watu
walishtushwa na kishindo na kumuona akiwa chini, akiwa amedondokea gari
dogo aina ya Toyota Corola linalofanya biashara ya teksi ambalo
liliharibika vibaya kutokana na kuangukiwa.
Marehemu
Shirima mbali ya kuwa mfanyabiashara wa muda mrefu Kariakoo, pia alikuwa
akiendelea na ujenzi wa jengo lake la ghorofa maeneo hayo.
Hoteli ya Concord iliyopo Kariakoo Mtaa wa Mchikichini, Dar es Salaam alipokuwa Shirima.
SIRI NYINGINE
Kuna madai
kwamba siku moja nyuma alikuwa akilalamikia taratibu za mikopo katika
mabenki na kwamba kuna watu wa benki walimfuata akawa anajibishana nao.
Madai
mengine ni kwamba inawezekana kuna mtu alikuwa akimtuma kwenda kulipia
bili, kodi ya mapato na vitu mbalimbali, hivyo kuna uwezekano alikuwa
hapeleki sehemu husika hivyo kumweka katika wakati mgumu.
...Shirima baada ya kujirusha kutoka ghorofani.
TARATIBU ZA MAZISHI
Shirima
ameacha mjane na watoto watano, alikuwa akiishi Kimara Suka ambapo
taratibu za mazishi zinafanyika na mwili unatarajiwa kusafirishwa kwenda
Mwika, Moshi kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika kesho Mei saba mwaka
huu.
Kwa mujibu
wa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marieth Minangi, uchunguzi wa
tukio bado unaendelea na taarifa kamili zitatolewa ukikamilika. “Tukio
kweli limetokea na uchunguzi bado unafanyika,” alisema Kamanda Minangi.







