Habari za uhakika zilieleza kuwa hivi
karibuni hali ilikuwa mbaya hadi ndugu kufurika nyumbani kwake Ubungo,
Dar ambapo alikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Jeshi, Lugalo jijini Dar.
Akizungumza na Amani katika mahojiano
maalum, nyumbani kwake Ubungo, Jumanne wiki hii, Dotnata alisema kuwa
awali alipokuwa akiumwa alikwenda katika Hospitali ya TMJ, Dar ambapo
alipimwa na kugundulika kuwa alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo.
Baadaye alipofanyiwa uchunguzi wa kina alionekana moyo haukuwa na tatizo kubwa isipokuwa presha ilikuwa inapanda sana.
HALI YAZIDI KUWA MBAYA
Dotnata aliporuhusiwa kurudi nyumbani akiwa
amepewa matibabu ya kushusha presha, alizidiwa kwa mara nyingine,
akaanza kutapika uchafu wa kijani na bluu.
ATAPIKA DAMU, AKIMBIZWA LUGALO
Haikuishia hapo kwani ilifika wakati akawa anataapika damu ndipo akakimbizwa katika Hospitali ya Lugalo.
Alipofikishwa Lugalo alipimwa tena na kugundulika kuwa figo moja ya kulia ilikuwa imeharibika kutokana na kuathiriwa na sumu.
Pia upande wa kulia wa mwili wake ulikuwa umeungua kwani alikuwa hawezi hata kusogeza mguu wa upande huo.
AONEKANA AMELISHWA SUMU
Hali ilizidi kuwa mbaya ndipo akahamishiwa
tena katika Hospitali ya TMJ ambapo baada ya kufanyiwa kipimo cha ‘Full
Blood Picture (FBP)’, alionekana kuwa amelishwa sumu.
Akashauriwa kupelekwa Hospitali ya Wakorea iliyopo Kariakoo, Dar kwenye wataalam waliobobea kwa kutoa sumu mwilini.
ALILISHWA MIEZI NANE ILIYOPITA
Alipofikishwa huko, daktari aligundua kuwa alilishwa sumu miezi nane iliyopita na ilikuwa ikimtafuna taratibu.
ATOBOLEWA KUTOA SUMU
Baada ya uchunguzi na vipimo vya kina,
Dotnata alitobolewa kwenye mbavu na kuwekewa mirija ambayo ilikuwa
ikichuja sumu yote na kuimwaga nje.
Mirija hiyo aliitumia kwa takribani wiki
nzima kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa huku akiwa haruhusiwi kuonana na mtu
yeyote zaidi ya mumewe, Mohammed Poshi na wachungaji mbalimbali
waliokuwa wakifika kumuombea.
APELEKWA KANISANI
Akiwa anaendelea na matibabu kwa Wakorea,
Dotnata alipelekwa kwa Nabii Flora Peter wa Kanisa la Huduma ya Maombezi
lililopo Salasala, Dar akiwa ametundikiwa ‘dripu’.
Akiwa kanisani hapo, huku akiwa hawezi hata
kutembea, Dotnata aliombewa, akapata nafuu kisha akaanza kutembea na
hapo ndipo hali yake ilipobadilika na kuwa nzuri huku baadhi ya watu wa
karibu wakidai kuwa kama hali itazidi kuwa mbaya itabidi apelekwe nchini
India.
ATAJIWA ALIYEMPA SUMU
Baada ya maombi mazito, Dotnata alifanikiwa
kutajiwa mtu aliyemlisha sumu na kukumbushwa siku na muda aliowekewa
sumu hiyo kwenye juisi.
Alisema aliambiwa jinsi ilivyokuwa kwani aliwekewa sumu kwenye juisi ya embe hivyo akakumbuka kila kitu.
Baada ya kumtambua mbaya wake ambaye ni
rafiki yake wa karibu sana, ilidaiwa kuwa mtu wake huyo alipewa fedha na
kutumwa ili amalize uhai wake na aliyemtuma alidaiwa kuwa hampendi
Dotnata.
Dotnata alidai alishangazwa na jambo hilo kwani iweje mtu huyo awe anatajwa yeye kila siku?
AMWACHIA MUNGU
“Pamoja na kunifanyia hivi, namshukuru Mungu amenirudisha duniani tena nishuhudie ukuu wake.
“Nilikuwa nimeshafika kuzimu, hakika
namuachia Mungu kila kitu, atanilipia kwani sikutarajia mtu niliyekuwa
namuamini kwa muda wa miaka 20 angeweza kuniwekea sumu kwa kulipwa fedha
ambazo zinaweza kuisha na akajutia alichonifanyia,” alisema Dotnata.
HADI SUMU IISHE
Hadi sasa Dotnata bado anatolewa sumu mwilini kwenye hospitali hiyohiyo ya Wakorea na anaendelea vema.