VIGOGO wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wakiwemo wabunge, wamemjia juu Mkuu wa Mkoa (RC) wa Arusha, Magessa
Mulongo kwa jinsi alivyoshughulikia kesi ya Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (CHADEMA).
Wabunge hao waliliambia gazeti hili mjini
Dodoma kuwa kesi ya uchochezi iliyofunguliwa na serikali dhidi ya Lema
kwa shinikizo la mkuu huyo, itaiathiri kwa kiasi kikubwa CCM.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alisema
kuwa amefuatilia kwa makini chanzo cha kesi ya Lema na hatimaye
kukamatwa na polisi mithili ya gaidi, na kubaini kuwa hulka
“Mimi sitaki kuingilia kesi, lakini
ukiangalia kuanzia ile inayoitwa video ya vurugu za Chuo cha Uhasibu
Arusha na jinsi Mkuu wa Mkoa alivyofika eneo la tukio na kuondoka,
utabaini udhaifu mkubwa wa kiongozi huyo ambao leo unamfanya Lema
aonekane shujaa.
“Leo tunaingia kwenye uchaguzi mdogo wa
madiwani pale Arusha, tunaweza tukashinda, lakini tutafanya kazi ya
ziada kwa sababu tu ya udhaifu wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha,” alisema
Lugola.
Mbunge mwingine
ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema alichokifanya Mulongo ni
sehemu ya tatizo kubwa la viongozi wa serikali kujihusisha na ukereketwa
wa kisiasa.
“Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa kuna kiongozi, tena hakumtaja jina,
kwamba anapendwa kubebwa, alisema mwacheni abebwe. Alisema vile kuwazuia
polisi kukabiliana na watu wanaopenda kumbeba kiongozi huyo.
“Mkuu wa Mkoa
Arusha na wengine wanaokabiliana na wapinzani kwa nguvu kubwa bila
sababu, hii inawaongezea umaarufu,” alisema mbunge huyo kutoka moja ya
majimbo ya kanda ya kati.
Mjumbe mmoja wa
Kamati Kuu (CC) ya CCM ambaye pia hakutaka kutaja jina lake, alilaani
jinsi mkuu wa mkoa huyo alivyojikoroga katika kushughulikia mzozo wa
Chuo cha Uhasibu Arusha.
“Niliposoma
ujumbe wa simu ya mkononi wa Lema ambao alidai umetoka kwa Mkuu wa Mkoa,
nilishangaa sana. Sijui kwanini amefanya vile,” alisema kigogo huyo.
Aprili 24 mwaka
huu, Mulongo aliliamuru Jeshi la Polisi mkoani Arusha kumkamata Lema kwa
madai kuwa aliwachochea wanafunzi wa chuo hicho cha IAA kumzomea na
kumrushia mawe.
Lema alizingirwa
nyumbani kwake na maofisa wa polisi kitengo cha upelelezi na wale wa
doria Ijumaa saa 5.30 usiku kisha kuchukuliwa hadi Kituo Kikuu cha
Polisi kuhojiwa na kuwekwa rumande siku tatu hadi Jumatatu wiki hii
alipofikishwa mahakamani.
Hata hivyo, madai
ya Mulongo kuwa Lema alichochea wanafuzni hao yanakinzana na ushahidi
wa video unaoonesha kuwa mbunge huyo alitumia kila aina ya ushawishi
kuwasihi wasiandamane kufuatia mwenzao Elly Kago (22) kuuawa na watu
wasiojulikana jirani na chuo.
Mapema kabla ya
kukamatwa, Lema aliitisha mkutano na waandishi wa habari akidai
kutishiwa na Mulongo kupitia ujumbe wa maandishi wa simu.
“Umeruka kihunzi
cha kwanza, nitakuonyesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata
na nitakupa kesi ninayotaka mimi,’’ ulisomeka ujumbe huo uliotumwa
kupitia simu namba 0752 960276 ambayo Lema alidai ni ya Mulungo.
Atisha waandishi
Wakati CCM
wakiendelea kumlalamikia Mulongo kwa hatua zake dhidi ya Lema, kiongozi
huyo jana aliwageukia waandishi wa habari wa Arusha akiwataka wawe
makini kipindi hiki, akidai kuwa nao wanatumika na wanasiasa.
Akihutubia katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi, alisema kuwa ikibainika wanatumika nao watafikishwa katika vyombo vya sheria.
“Mimi nilikuwa
Mkuu wa Wilaya Bagamoyo, hivi hivi wakawa hawanielewi na ikafika wakati
wakanielewa kwani kuna miongoni mwao tulitaka kuwafikisha katika sheria,
lakini tukayaacha kwa kuwa sisi ndio walezi,” alisema.
Mulongo aliongeza
kuwa vitu ambavyo vinaandikwa si kweli kabisa, na kwamba wataendelea
kufuatilia kwani baadhi ya waandishi wanashirikiana na wanasiasa
kuwachafua viongozi wa serikali.
Alisema baadhi ya
waandishi mkoani Arusha wamekuwa wakifanya kazi zao kwa ushabiki wa
kisiasa na kuandika mambo ambayo hawana uhakika nayo.
“Unapoingia katika mkakati wa kudhalilisha kiongozi wa serikali unakuwa umeiweka roho yako rehani, kuweni makini,” alisema.
Aidha alivionya
vyama vya wafanyakazi mkoani Arusha kutoruhusu kutumiwa na watu kwa
malengo ya kisiasa na pia waajiri waache kufanya kazi bila kufuata
taratibu na sheria.
TANZANIA DAIMA