Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Friday, April 26, 2013

Wabunge CCM ‘washikana uchawi’ Bajeti ya Maji

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe (wa pili kushoto), Naibu Waziri wa Maji, Dk Binilith Mahenge (kushoto) na Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere baada kuahirishwa kwa kikao cha Bunge, Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi  
 
Dodoma. Saa chache baada ya Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2013/14 kutupwa na Bunge jana, wabunge wa CCM wameshikana uchawi huku wakitaka kuwatosa wenzao wanaowatuhumu kusababisha kadhia hiyo.

Wabunge wa CCM walikutana katika kikao cha dharura kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kujadili hatua ya Bunge kukataa bajeti hiyo kwa maelezo kwamba haina suluhisho la kuwaondolea wananchi matatizo ya maji.

Kelele za wabunge wa CCM na wale wa upinzani zilimlazimisha Spika wa Bunge, Anne Makinda kuiondoa bungeni na kuitaka Serikali ikajipange upya na kuiwasilisha Jumatatu.
Baada ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge jana mchana, wabunge wa CCM walikutana na habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema wabunge Kangi Lugola (Mwibara) na Deo Filikunjombe (Ludewa) walishambuliwa kutokana na kile kilichodaiwa kwamba wamekuwa wakiidhalilisha Serikali ya CCM bungeni.

Habari zinadai kwamba waliowashambulia wabunge hao ni wenzao, Saidi Nkumba (Sikonge) na Livingstone Lusinde (Mtera) ambao kwa nyakati tofauti walitamka kwamba hawaisaidii Serikali na kwamba bora wakahamia upinzani kuliko kuendelea kukichafua chama hicho.
“Kimsingi jamaa walibanwa sana walitaka Filikunjombe na Lugola wafukuzwe uanachama kwa sababu wanaishambulia sana CCM bungeni,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo kingine kilisema kuwa wabunge hao walipata utetezi wa wabunge wawili, Beatrice Shellukindo (Kilindi) na Peter Serukamba (Kigoma Mjini) ambao walikaririwa wakisema kwa nyakati tofauti kwamba Lugola na Filikunjombe hawajakosea chochote kwani wanaeleza hali halisi ilivyo.

Baada ya mjadala huo, Pinda alikaririwa akimwelekeza Katibu wa Wabunge wa CCM, Janister Mhagama kumwandikia barua Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuhusu suala hilo ili liwe ajenda katika mkutano baina ya wabunge wa CCM na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ambao unatarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Habari zinadai kuwa hoja ya kutupwa wa Bajeti ya Maji haikujadiliwa hata kidogo, kwani baada ya Pinda kuwaarifu wabunge kuhusu kilichotokea bungeni, wabunge hao wa CCM katika kikao hicho cha ndani walianza kumsaka mchawi kutoka miongoni mwao.

Akiiondoa bajeti hiyo jana mchana, Spika Makinda aliitaka Kamati ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge pamoja na Wizara ya Fedha na Wizara ya Maji kukutana kuiangalia upya na kutafuta jinsi ya kupata fedha za kuongeza kisha iwasilishwe Jumatatu ijayo.

Hatua ya Makinda ilikuja baada ya mashambulizi makali ya kuikataa hivyo kusema haoni sababu za hoja hiyo kuendelea kujadiliwa, kwani tayari ilikuwa imelalamikiwa na wabunge wengi kutoka pande zote.

“Mapema leo Mheshimiwa Mwigulu Nchemba aliomba mwongozo wangu, lakini na mimi nasema toka jana hadi leo hii naona hoja za wabunge kuhusu jambo hili hakuna anayeunga mkono,” alisema Makinda na kuongeza:

“Pamoja na shutuma nyingi kuhusu Kamati ya Bajeti niliyounda na kumteua Mheshimiwa (Andrew) Chenge kuwa mwenyekiti, sasa naagiza kamati hiyo ikutane na Wizara na Serikali ili watafute jinsi ya kupunguza tatizo hili na walete majibu hapa siku ya Jumatatu, hivyo naahirisha shughuli za Bunge hadi Jumatatu asubuhi.”

Makinda alilalamikiwa kwamba aliunda kamati hiyo kinyume cha kanuni za Bunge lakini jana alisema alifanya hivyo kwa kutumia Kifungu cha 5 cha Kanuni za Bunge ambazo zinampa mamlaka ya kufanya hivyo.


Katika hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara ya Maji, iliyosomwa juzi na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, Serikali iliomba Sh398 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji 2013/14.

Dalili za kuondolewa kwa hotuba hiyo zilianza mapema jana, baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe kumuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda iwapo hakuona sababu za msingi za kuondoa hoja hiyo ili wahusika wakae na kuifumua upya?

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, maji ni uhai na maji ni muhimu kwa mustakabali wa maisha ya mwanadamu, mjadala wa hotuba ya maji unaonekana kuwa ni mkali zaidi na wengi hawakubaliani na bajeti hii. Je, Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwa nini Serikali isiondoe hoja hii ili wahusika wakakae na kuichambua upya?” aliuliza.

Akijibu swali hilo, Pinda alikiri kuwa Bajeti hiyo ilikuwa na mvutano mkali kutoka kwa wabunge, lakini akasisitiza kuwa Serikali inaweza kutazama namna ya kuongeza fedha kupitia mafungu mengine (OC) ili kujazia.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Nchemba aliomba mwongozo wa Spika kuhusu jambo hilo akitaka Serikali kukubaliana na hoja yake kwamba bajeti ya maji isiendelee kujadiliwa, kwani ilipaswa kufanyiwa marekebisho na kuandaliwa upya ili kupunguza tatizo la ukosefu wa maji kwa wananchi.

Licha ya wabunge hao, tangu juzi mjadala huo ulipoanza, wabunge wote walikuwa wakipiga kelele kuipinga wakisema haikuwa na suluhisho la kweli.

Nje ya ukumbi

Wakizungumzia uamuzi wa Spika, baadhi ya wabunge walisema ulikuwa sahihi kwani isingewezekana ikapitishwa kwa kuwa ilishaonekana kutokukidhi matarajio yao.
Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alirejea kauli yake aliyotoa wakati akichangia ndani ya Bunge kuwa lazima viongozi wa Serikali wanyimwe maji ya kunywa pindi wanapokwenda katika ziara zao ili waone uchungu wa kukosekana kwa maji.

Alisema Spika alitumia hekima kwa kuondoa mezani hoja hiyo ambayo alisema kwa vyovyote isingepitishwa na wabunge akiwamo kwani alishatangaza hadharani kutoiunga mkono.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alipongeza uamuzi wa Spika lakini akaitahadharisha Serikali “Isije ikarudi na majibu ya danganya toto kama ilivyofanya mwaka jana katika Wizara ya Nishati.”

Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu alisema Bajeti hiyo inapaswa kuongezwa hadi kufikia Sh1 trilioni ili walau iweze kukidhi mahitaji ya maji nchi nzima.



MWANANCHI
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...