*RB yake yazua utata, Polisi washikwa kigugumizi
JIMEIBUKA
hofu ya kuwepo mpango mahususi unaoratibiwa na Serikali kufichua njama
za kigaidi, ambazo zinadaiwa kutekelezwa na baadhi ya viongozi wa
kisiasa wanaoheshimika katika jamii, MTANZANIA Jumapili
limebaini.Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa,
kukamatwa kwa mtuhumiwa namba mbili katika kesi ya ugaidi iliyofunguliwa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ludovick Joseph, ni utekelezaji wa
mpango huo.
Imedaiwa
kuwa, kuna utata mkubwa wa usahihi wa taarifa za tukio la Ludovick
kutekwa na watu ambao hawajafahamika hadi sasa na hata taarifa za
kutekwa kwake alizodai kuzifikisha katika kituo kidogo cha polisi
Kigogo, nazo zina utata.
Kwa
mujibu wa wapasha habari wetu, taarifa za kutekwa kwa Ludovick na
kunyang’anywa vitu vyake vyote alivyokuwa navyo, zikiwemo nguo alizokuwa
amevaa na hata madai kuwa aliripoti tukio hilo katika kituo cha Polisi
Kigogo siyo za kweli, bali zimetengenezwa ili kufanikisha mpango huo.
Ludovick
alidai kutekwa usiku wa Jumanne ya Machi 5, mwaka huu, akiwa eneo la
Sinza ambako alisema alitoa taarifa zake katika Kituo cha Polisi cha
Kigogo na kufunguliwa RB yenye namba KIG/RB/318/2013.
Taarifa
ya kutekwa kwake aliiandika mtandaoni na ilisomeka hivi; ‘Leo usiku,
yapata saa tano na nusu, niliachana na Maggid Mjengwa maeneo ya
Shekilango tukitokea Rose Garden. Yeye alielekea hotelini alikofikia
sehemu fulani Kariakoo nami nikasubiri kigari kuelekea nyumbani kwangu.
Hapo
Shekilango, magari yalichelewa kidogo, pembeni ilipaki bajaji ikiwa na
watu wawili na dereva ndipo wakaniambia twende tuchangie mia tano tu
kwenda Ubungo Mataa, nikakaa katikati ya hao jamaa.
Ghafla
wakakata kona na kuanza kuelekea Mabibo huku wakiulizana kama wako
kamili na mwingine kujibu yuko kamili. Nikajua tayari niko mikononi mwa
majambazi na sikujua wako kamili namna gani, kwa hiyo nikaamua kuwa
mtulivu.
Tulipofika
relini karibu na Mabibo wakanipokonya begi lakini, hawakulifungua.
Ndani yake kulikuwa na laptop, toshiba kubwa na chaji yake, kamera ndogo
ya digital na USB yake, modem ya zantel na card reader. Tulipofika
maeneo ya Loyola Sekondari, nikawasihi wanishushe ili nirudi mwenyewe,
wakaniambia safari ile inaishia Jangwani.
Nikaingiwa
na wasiwasi mkubwa na nia yao hasa, maana wameshanipokonya begi kwa
nini wasiniachie? Lakini niliendelea kuwa mtulivu ili kutowaprovoke.
Tulipovuka
Kigogo mwisho kwenye giza karibu na msikiti, wakasimama pembeni ya
barabara na kuniamuru kushuka, nikashuka na kuanza kuwadai begi langu,
ndipo mmoja akasema wamekuwa wastaarabu mimi naanza kuwadharau. Ghafla
akanivuta kwa nguvu kunirudisha kwenye kibajaji akamwambia mwenzie
wanisachi kama nina vitu vingine, wakanisachi na kuchukua pesa, nilikuwa
na elfu 35 na simu mbili ndogo za nokia moja yenye line mbili.
Kisha
mmoja akatoa ‘order’ nivuliwe nguo. Nikavuliwa viatu, T-shirt na
suruali nikabaki na nguo za ndani pekee. Wakanishusha na kuniacha hapo.
Kurudi
nyuma kama hatua kumi tu ndipo kituo kidogo cha polisi Kigogo nikaanza
kutoa maelezo hapo kwa zaidi kama ya saa mbili nikiwa uchi na nguo za
ndani tu. Nikiwa hapo nikasikia polisi wakiwasiliana juu ya tukio la
kupigwa vibaya Absalom Kibanda, kwenye redio calls.
Ilikuwa
yapata saa nane, baada ya kuchukuliwa maelezo polisi walinipatia gari
nikaelekea hotelini kwa Maggid, ambaye saa kumi aliamshwa na
kunichukulia chumba hapo nikapumzika. Ameniazima nguo zake ndizo nimevaa
bado hadi sasa naelekea kituo cha Polisi Magomeni kwenda kupewa
mpelelezi wa kesi yangu. Namba ya kesi yangu Kigogo ni KIG/RB/318/2013,
wizi kutoka maungoni.’
Wakati
Ludovick akiwa ametoa maelezo hayo kwa jamii kupitia mitandao ya
kijamii, polisi wameshindwa kuthibitisha taarifa za kutekwa, kuporwa na
kupokea taarifa yake aliyodai kuitoa kituo kidogo cha polisi Kigogo.
Polisi
katika kituo kidogo cha Kigogo waliohojiwa na MTANZANIA Jumapili
kuhusiana na taarifa za Ludovick, walionekana kurushiana mpira
kuzizungumzia.
Askari
aliyekutwa kituoni hapo alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema taarifa
za matukio mbalimbali hufunguliwa hapo, lakini huhamishiwa Kituo cha
Polisi cha Magomeni kutokana na udogo wa kituo hicho, hivyo kumtaka
Mwandishi kufuatilia suala hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni.
Gazeti
hili lilipofika Kituo cha Polisi Magomeni, kwa Askari Mpelelezi
liliyeelekezwa kuwa anahusika na kesi ya Ludovick aliyetajwa kwa jina
moja la Chuki hakuwepo bali lilipewa namba ya simu yake ya kiganjani na
alipotafutwa, naye alikana kuhusika na suala hilo na kuelekeza atafutwe
askari polisi aliyetajwa kwa jina la Lukwamba Sanga.
Alipopigiwa
Sanga na kuulizwa kuhusu sakata hilo, kwanza alikiri kuwa yeye ndiye
mpelelezi wa kesi hiyo na kueleza kuwa ni kweli Ludovick alifungua RB
katika kituo cha Polisi cha Kigogo lakini hakuwa tayari kutoa namba ya
RB hiyo.
Alieleza
kuwa mwenye mamlaka ya kutoa namba hiyo ni Mkuu wa Upelelezi wa Kituo
ambaye hata hivyo hakupatikana, lakini ofisa mwingine kituoni hapo
alieleza kuwa namba hiyo inaweza kutolewa kwa idhini ya Kamanda wa Mkoa
wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela.
Kamanda
Kenyela alipotafutwa, alisema anahitaji muda kuipata namba hiyo, kwa
sababu ana majukumu mengi hivyo atafutwe baadaye. Lakini alipotafutwa
tena simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.
Hata alipopigiwa simu tena jana iliita mfululizo pasipo majibu.
Wachambuzi
wa masuala ya saikolojia wanadai dalili zinaonyesha kuwapo kwa
uwezekano wa Ludovick kushiriki tukio la kutekwa na kupigwa kwa Mhariri
Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.
Wanasema
ni kawaida kuwa watu wanaojihusha na matukio ya aina hii, baada ya
kuyatekeleza huchanganyikiwa, hivyo hata kitendo cha Ludovick kukimbilia
kuandika katika mtandao wa ‘facebook’ kuwa naye alitekwa kinaweza
kuchukuliwa katika mtizamo huo.
Maswali ya kujiuliza
Ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja
sasa baada ya kuvamiwa na kuteswa kwa Kibanda na siku chache baadaye
kukamatwa kwa Ludovick akihusishwa na tuhuma za kupanga ugaidi, yapo
maswali mengi miongoni mwa jamii ambayo hayajapata majibu kuhusu matukio
hayo.
Swali
kubwa linaloumiza vichwa vya wengi hivi sasa ni namna ambavyo Ludovick
alifanikiwa kujipenyeza na kufanikiwa kujenga mtandao wa masiliano ya
simu za mkononi na katika mitandao ya kijamii na Wahariri mbalimbali wa
Vyombo vya Habari.
Tayari
Wahariri wawili, Deodatus Balile na Ansbert Ngurumo, wamekwishatajwa
kuwa na mawasiliano ya muda mrefu na Ludovick na kwamba kuna baadhi ya
taarifa muhimu za waandishi na wahariri ambazo Ludovick alikuwa
akizipata kupitia mawasilino yake hayo.
Kutajwa
kwa wahariri hao kuwa washirika wa karibu kimawasiliano na Ludovick,
kuliibua hisia kuwa Wahariri hao, waliingizwa katika mtandao wa Ludovick
na kuanza kufanya kazi zake pasipo wao wenyewe kujua au wakiwa na
ufahamu huo.
Lakini
pia wadadisi wa mambo wamekuwa wakihoji nguo za Ludovick zilipo baada
ya kile kinachodaiwa kuwa tukio hilo la kudai kutekwa ni feki.
Hali
kadhalika hatua ya Ludovick baada ya kuachana na Mjegwa na kupanda
bajaji iliyokuwa na watu wawili kisha akakaa katikati kwa nauli ya
shilingi mia tano huku akiwa na pesa taslimu shilingi 35,000, begi lenye
laptop toshiba kubwa, chaja yake, kamera ndogo ya digital na USB yake,
modem ya zantel na card reader, jambo linaloonyesha kuwa alikuwa na
uwezo wa kuchukua usafiri salama zaidi.
Aidha,
mkanganyiko wa maelezo ya Ludovick na yale yaliyotolewa na Mjengwa
ambako yeye (Ludovick) alidai kupewa gari na polisi kumpeleka hotelini
kwa Maggid, huku Maggid akidai alifika hapo kwa usafiri wa teksi, nayo
yanazidi kuacha swali gumu la kupata ukweli wa sakata hili zima.
Kuhusishwa
kwake na tukio la Kibanda Siku na wakati ambao Kibanda alitekwa na
kuteswa, Ludovick naye alidai kutekwa na majambazi akiwa eneo la Sinza,
jirani na mahali ilipo ofisi ya Kibanda. Ludovick alidai kutekwa na watu
wasiojulikana majira ya saa tano usiku siku ya Jumanne ya Machi 5,
mwaka huu, ambapo watekaji wake walimnyang’anya vitu vyake mbalimbali na
kumvua nguo zote pamoja na kuchukua simu zake mbili.
Ingawa
katika uchunguzi wake gazeti hili liliambiwa kuwa simu yake iliendelea
kutumika katika maeneo ya mnara wa Sinza karibu na ofisi anakofanyia
kazi Kibanda siku mbili mara baada tukio la kuteswa kwa Mhariri huyo.
Pamoja na hilo, siku mbili kabla Kibanda hajatekwa, anadaiwa kufanya
mawasiliano na kiongozi mmoja mkubwa wa chama cha siasa.
Ahusishwa na video ya Lwakatare
Yuko mikononi mwa sheria na
alishafikishwa Mahakamani pamoja na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, kutokana
na mipango ya kudhuru watu, wakiwemo waandishi wa habari pamoja na
suala la ugaidi.
Inaelezwa
kuwa watu hao wamekuwa karibu kwa muda mrefu ambapo wote ni wenyeji wa
Mkoa wa Kagera, na kwa mujibu wa watu wa karibu na mahusiano yao,
walisema kuwa Ludovick amepata kumsaidia kufanya kampeni za kuwania
ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini mwaka 2000.
Ludovick ni nani?
Ludovick, mbali na kuwa na
ukaribu na Lwakatare, pia alikuwa mtu wa karibu na Mjengwa, akimsaidia
katika shughuli za blog yake, pamoja na wahariri mbalimbali wa habari.
Ludovick pia wapo wanaomtambua kama mtu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Mjengwa
pia aliwahi kukiri kutofahamu kazi halisi aliyokuwa akiifanya Ludovick
mtaani, lakini katika maelezo yake aliyoandika kupitia kwenye mtandao wa
Jamii Forum, Mjengwa alisema anamfahamu Ludovick tangu akiwa Chuo Kikuu
(DUCE) na kwamba ni mmoja wa Watanzania wengi waliomfahamu kupitia kazi
zake magazetini.