.jpg)
MBUNGE wa
Mwibara, Kangi Lugola (CCM) amefichua siri ya sababu ya Kamati ya
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwaweka kitimoto yeye na Mbunge wa
Ludewa, Deo Filikunjombe.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Lugola alisema sababu ya
kibano alichopata ndani ya CCM ni kutokana na kauli aliyotoa hivi
karibuni mkoani Iringa ya kumuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu,
Edward Lowassa.
“Wabunge
wa CCM tunaoikosoa serikali na kuzigomea bajeti tuko wengi, kwanini
ndani ya kikao wametubana mimi na Deo tu? Mimi nadhani ile ziara
tuliyoifanya hivi karibuni kumsindikiza Lowassa mkoani Iringa ndiyo
imeleta shida yote hii,” alisema.
Mbunge
huyo machachari bungeni, alisema pamoja na maneno na vitisho
alivyotolewa ndani ya kikao hicho na baadhi ya mawaziri na wabunge
wenzake wa CCM, kamwe hawezi kuogopa.
Alisema
hatua ya kutaka kunyamazishana, hakubaliani nayo bali anaendelea na kasi
yake ya kuibana serikali pale anapoona dhahiri kwamba inakosea.
“Mimi
siogopi maneno, hata kifo chenyewe pia sikiogopi. Nitasimamia ukweli,
CCM ni chama changu na serikali ni yangu na naitakia mema ndiyo maana
nipo tayari kufa kwa kusimamia ukweli huo,” alisema.
Hivi karibuni Lowassa aliambatana na wabunge hao mkoani Iringa ambako alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa kanisa na kituo cha redio cha Overcomers Power Centre (OPC) mjini Iringa.
Katika hafla hiyo alitunukiwa tuzo maalumu kutokana na jitihada zake za kuitumikia na kuisaida jamii nchini.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Lugola aliwashangaa watu wanaowalaumu wanasiasa kwa
kuingia makanisani na kusema kuwa kazi wanazozifanya hazina tofauti na
za viongozi wa dini.
Lugola alifananisha matukio yaliyomkuta Lowassa sawa na matatizo yaliyomkuta Bwaba Yesu wakati alipokuwa anahubiri duniani.
Alimmwagia
sifa Lowassa kuwa licha ya maneno mengi yanayosemwa juu yake, lakini
bado ameendelea kuitumikia jamii kupitia siasa na shughuli za kidini.
Alisema
kuwa kama ilivyokuwa kwa Yesu ambaye alipigwa na kunyanyaswa na kuyaacha
yote kwa Mungu, Lowassa naye aliandamwa na waliomzushia kesi kiasi cha
kuamua kujiuzulu uwaziri mkuu.
“Mnakumbuka
kuwa waliomchukia Yesu walimfungulia mashtaka ya uongo wakamfikisha
mbele ya pilato. Walipoambiwa watoe ushahidi wakashindwa, lakini
wakapiga kelele asulubiwe. Yesu alipigwa, akatemewa mate, lakini yeye
akasema ‘ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke lakini si kama nitakavyo
mimi bali mapenzi ya Mungu yatimizwe’.
“Vivyo
hivyo Edward, aliposakamwa sana aliamua kujiuzulu uwaziri mkuu...lakini
tunajua kuwa Yesu, baada ya kuuawa, alifufuka na kuinuliwa. Naomba
kanisa liendelee kumuombea Lowassa ili naye ainuliwe juu katika nchi
yetu ya Tanzania,” alisema Lugola.
Filikunjombe
naye alimwaga sifa kwa Lowassa akimtaka kutokatishwa tamaa na maneno
yanayosemwa, na kuongeza kuwa siku zote mti wenye matunda ndio unaopigwa
mawe.
Wiki
iliyopita katika kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM, Lugola na
Filikunjombe walisutwa kutokana na mwenendo wa kuikosoa serikali na
kuwashambulia mawaziri.
Mbunge aliyewawashia moto wabunge hao ni Said Nkumba wa Sikonge ambaye alihoji mwenendo wao.
Mbele ya
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mkumba alisema kuwa wabunge hao wanatumika na
CHADEMA na kuwataka waamue kama wanabaki CCM au la.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi, huku mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde akitolea mfano wake.
Naibu
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Adam Malima naye alimbana Lugola
ataje majina ya mawaziri alioliambia Bunge kwamba wanauza unga.