Christopher Shekiondo |
Dawa
za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya
Sh. bilioni 6.8 zimekamatwa nchini Afrika Kusini wakati zikisafirishwa
kutoka Tanzania.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka nchini humo, wanawake wawili
walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Oriver Tambo uliopo
eneo la Kempton Park siku ya Ijumaa wiki iliyopita wakitokea Tanzania.
Wanawake
hao walikamatwa wakiwa na mabegi sita ambayo yalipokaguliwa yalikutwa
na kilo 150 za dawa hizo ambazo pia zinajulikana kama ‘Tik’.
Baada ya kukamatwa na dawa hizo wanawake hao walikabidhiwa polisi.
Mwenyekiti
wa Tume ya Kuthibiti Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo,
alipotafutwa alisema hajapata taarifa hizo na aliahidi kufuatilia.
"Sijapata taarifa za tukio hilo lakini nitafuatilia kujua kama kweli wanawake walitoka Tanzania," alisema Shekiondo.
Hivi
karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika taarifa yake ilisomwa kwa
niaba yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi, mjini Dodoma, katika maadhimisho ya kitaifa ya
‘Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani’ alisema tatizo la dawa
hizo ni janga la kitaifa hivi sasa nchini.
Alisema
kumekuwa na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara
haramu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi
cha miaka mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa
kujihusisha na dawa hizo.
Endelea kusoma habari hii kwa kubofya hapa chini
Pia
alisema katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika nchi za
Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, kuharibu taswira ya nchi na
kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti magumu
wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
Alisema
mwaka huu pekee kumekuwa na ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya katika
eneo la kimataifa la Bahari ya Hindi karibu na Tanzania.
Pinda alisema hivi sasa mikate, maandazi na askrimu zinazouzwa kwenye shule za msingi, zinawekwa dawa za kulevya.
Alisema
vitendo hivyo vinafanya vijana wengi wa shule za msingi na hata
sekondari kuwa na tabia za ajabu, ikiwamo kuingia darasani wakiwa na
kiatu kimoja mguuni, mkufu wenye nyembe na kidani chenye nyembe kifuani.
CHANZO: NIPASHE