Wananchi wa Misri wakitwangana wenyewe kwa wenyewe
Na Flora Martin Mwano
Watu
zaidi ya ishirini na sita wamekufa katika ghasia zinazoendelea kuchacha
nchini Misri baada ya jeshi la nchi hiyo kumuondoa madarakani Mohammad
Morsi ambaye ni Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo.
Wengi waliouawa ni wafuasi wa chama cha Muslim Brotherhood walioshiriki
maandamano ya siku ya ijumaa wakilishinikiza jeshi kumrejesha madarakani
Rais wao aliyekaa madarakani kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee.
Katika
taarifa ya mapema jumamosi hii, wafuasi wa Muslim Brotherhood wameapa
kuzidi kuendesha maandamano ya amani mpaka kiongozi wao atakaporejeshwa.
Morsi
ambaye hajajitokeza kwa umma toka kupinduliwa, amewataka wafuasi wake
kupigania haki yao kwa kiongozi waliyemchagua katika uchaguzi wa
kidemokrasia.
Kwa
upande wake jeshi limesisitiza kufanyika maandamano ya amani pekee
wakati huu ambapo Rais wa mpito Adly Mahmud Mansour, akisema kuwa
uchaguzi Mkuu utafanyika hivi karibuni ili kuwapa nafasi wananchi wa
Misri kuamua ni nani wanayetaka awaongoze.
Taarifa
toka nchini humo zimeeleza kuwa baadhi ya wanachama wa Muslim
Brotherhood sambamba na Bwana Morsi watafikishwa mahakamani siku
jumatatu kusomewa mashtaka ya kukiuka amri ya mahakama.
Tayari
Umoja wa Afrika AU umesitisha uanachama wa Misri katika Umoja huo na
kusema hautambui mapinduzi hayo kwa sababu Morsi alichaguliwa
kidemokrasia baada ya kuondolewa kwa Rais wa zamani Hosni Mubarak.