Salaam. Siku tatu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuponda mpango wa Chadema
kuanzisha kambi kwa ajili ya mafunzo ya ulinzi kuwalinda viongozi na
wanachama wake, chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimeibuka na
kusema kuwa kinaendelea na mpango huo na kambi hizo zitaanza rasmi wiki
ijayo.
Kimesema hakitishwi na kauli ya Jeshi la Polisi kukionya juu ya
uanzishwaji wa mafunzo hayo, kwamba jeshi hilo linatakiwa kuanza
kukizuia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwanza, kwa maelezo kuwa chama hicho
tawala pia kina kikundi cha ulinzi ‘Green Guards’ ambacho kinafanya
mafunzo ya kijeshi, huku kikitumia silaha za moto.
“CCM
ndiyo wataipeleka nchi hii pabaya, wanawafundisha vijana huku
wakiwabebesha bunduki, wanajenga taifa la aina gani, bunduki ni silaha
ya kivita sasa wanaandaa watu kupigana na nani” alisema Mkurugenzi wa
Organaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira jana wakati
akizungumza na wanahabari huku akionyesha picha za mafunzo ya CCM,
zinazoonyesha vijana wakiwa wamebeba silaha (hata hivyo ni mbao
zilizotengenezwa kwa mfano wa bunduki).
Wakati Chadema wakieleza hayo, CCM kimeshtushwa na taarifa hizo na kueleza kuwa hali hiyo sasa inahatarisha usalama wa nchi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Martin Shigela
alisema ni vyema Chadema kikawaambia wananchi wawalinde, kuliko
kuanzisha mafunzo huku akimtaka Msajili wa Vyama vya siasa nchini, John
Tendwa kulitizama kwa kina suala hilo.
Akifunga Kongamano la Amani lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia
Tanzania (TCD), Dar es Salaam Julai 10, mwaka huu, Rais Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa pia alikosoa kitendo cha Chadema kususia
kongamano hilo alisema, “Sasa hawa kweli wanapenda amani yetu wakati
hawapendi tuzungumze wanataka watu wauane, wapigane.”
Mbali na Rais Kikwete, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, SSP Advera
Senso juzi alikionya chama hicho kuhusu mpango huo akisema kuwa kitendo
cha chama chochote cha siasa kikiwemo Chadema, kuanzisha kikundi cha
kujihami ni kinyume na sheria za nchi na endapo watafanya hivyo hatua za
kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kauli ya jana ya Chadema ni mwendelezo wa ile iliyotolewa na Mwenyekiti
wa chama hicho Freeman Mbowe Julai 9, mwaka huu, ambapo alisema
kimechukua hatua hiyo baada ya Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na
usalama kushindwa kufanyia kazi malalamiko yao kuhusu mauaji, vitisho na
matukio ya kutisha wanayofanyiwa baadhi ya viongozi na wanachama wao.
Katika ufafanuzi wake Kigaila alisema Chadema hakianzishi vikundi vya
kijeshi, bali mafunzo ya kuwafundisha walinzi wa chama hicho ‘Red
Brigade’, jinsi ya kujilinda.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki kwa
raia yeyote kujilinda, Chadema ni taasisi ni haki yetu kuilinda taasisi
yetu ndiyo maana tumesajili kikundi chetu cha ulinzi, sasa nani
anatutisha, tunataka polisi waanze na CCM kwanza ambao katika mafunzo
yao wanafundisha hadi kupiga saluti na kutumia silaha,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yataanza rasmi wiki ijayo, huku akisita kutaja siku
yatakayoanza, wala mikoa yatakayofanyika na kusisitiza kuwa hayo
yatatangazwa wiki ijayo wakati vijana wakienda katika mafunzo.
CHANZO-MWANANCHI.