Navi
Pillay Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameutaka
utawala wa Kizayuni wa Israel kuufanyia mabadiliko mswada wa sheria
ambao ikiwa utatekelezwa utasababisha kuporwa kwa ardhi katika eneo la
Negev na hivyo kupelekea watu takribani 40,000 kutoka jamii ya Bedouin
kutimuliwa kutoka kwenye ardhi ya mababu zao.
Pillay
anasema kuwa 'watu wa jamii ya Bedouin wana haki sawa ya kumiliki mali,
nyumba na kupata huduma za umma kama jamii nyingine yeyote ile ya
Israel'. Pillay alielezea masikikitiko yake kuwa bado utawala wa Israel
unaendelea kuwalazimu watu wenye asili ya Kiarabu kuhama makwao hata
baada ya kulizungumzia suala hilo alipofanya ziara Israel miaka miwili
iliyopita. Pillay ameongeza kuwa ikiwa mswada huo utakuwa sheria
utachochea kubomolewa kwa makao ya jamii hiyo na kuwalazimu watu hao
kuhama makwao hatua ambayo itawanyima haki yao ya kumiliki ardhi.