Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba |
Mwandishi Wetu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu Rasimu ya Katiba
iliyotolewa hivi karibuni katika lugha Kiingereza na Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) na kusema rasimu hiyo haitoi tafsiri sahihi ya
maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal Juni 3 mwaka huu (2013).
Rasimu hiyo iliyotolewa na LHRC ambayo inasambazwa kupitia njia
mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, pia inatumika katika mikutano na
warsha mbalimbali zinazojadili kwa lengo la kutoa maoni kuhusu Rasimu
iliyotolewa na Tume.
“Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapenda kuwafahamisha wananchi na wadau
wengine kuwa Rasimu hiyo ya Katiba katika lugha ya kiingereza
iliyoandaliwa na LHRC haitoi tafsiri sahihi ya maudhui ya Rasimu ya
Katiba iliyotolewa na Tume katika lugha ya Kiswahili na hivyo kupotosha
umma kuhusu maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni,”
amesema Katibu wa Tume hiyo, Bw. Assaa Rashid katika taarifa yake kwa
Vyombo vya Habari leo (Julai 9, 2013).
Bw. Asaa amewataka wananchi kuendelea kusoma na kutoa maoni kuhusu
Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika
lugha ya Kiswahili ambayo amesema imesambazwa kwa wananchi, taasisi,
jumuiya na taasisi mbalimbali. Rasimu hiyo pia inapatikana katika tovuti
ya Tume (www.katiba.go.tz) na kutolewa bure katika Ofisi za Tume
zilizopo Dar es Salaam na Zanzibar.
Aidha, Tume hiyo imesema iliandaa Rasimu ya Katiba katika lugha ya
Kiswahili ili kuwawezesha wananchi ambao wengi wao wanajua kusoma na
kuandika kwa lugha ya Kiswahili kuelewa maudhui ya Rasimu hiyo.
Katika taarifa yake, Tume imewataka wadau wote wanaotaka kutafsiri
Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume kuwasiliana na Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ina
Wataalamu wa Uandishi wa Sheria (Legislative Drafters).