Baadhi ya majeruhi wahanga wa ajali ya Basi la Sumry iliyotokea Sitalike katika mto Iku Julai 5, 2013 majira ya saa 7:30 usiku |
Mganga mkuu wa wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi, Dr Emanuely Kamgobe akifafanua jinsi walivyoweza kumudu kuwahudumia wahanga wa ajali |
Basi la Sumry lenye namba T909AZT mara baada ya kuondolewa mtoni Sitalike maarufu kama nyumba ya VibokoJulai 5, 2013 : NA http://www.sumiampanda.blogspot.com |
Kijidaraja chembamba kinachodaiwa kusababisha ajali tisa tangu Januari 2013 hadi Juni 2013 |
KATIKA hali isiyo ya kawaida basi la kampuni ya Sumry limetumbukia mtoni
na kuuwa watu tisa na kujeruhi abiria wapatao hamsini na tatu katika mto Iku
uliopo katika kijiji cha Sitalike wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa sita usiku kuamkia Julai 5, 2013
basi hilo lilipokuwa likitokea mjini Sumbawanga kuelekea Mpanda mkoani Katavi
likiwa na abiri waliokuwa wametoka Mbeya.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Katavi Emanuely Nnley alisema jana kuwa
ajali hiyo ilihusisha basi aina ya Nissan Diesel lenye namba T909 AZT mali ya
kampuni ya Sumry lililokuwa likiendesha na dereva aliyetajwa kwa jina na
Stephano Chimane maarufu kwa jina la Ntungu.
Alisema basi hilo lilipofika katika daraja hilo lenye kona kali na
mteremko dereva wake alishindwa kulimudu na kulenga daraja hali iliyosababisha
tairi za nyuma kupanda juu ya ukingo na kudumbukia mtoni ambapo dereva wa basi
hilo aliweza kutoka na kukimbilia kusikojulikana.
Alifafanua kuwa juhudi za uokoaji zilianza kufanyika usiku huo huo ambapo
majeruhi 53 waliokolewa na maiti tisa za wanaume watatu na wanawake watano na
motto mmoja wa kike ziliopolewa katika maji.
Alisema hali ya majeruhi inaendelea vizuri isipokuwa majeruhi watatu
walikimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Rukwa kwa matibabu zaidi na kufafanua
kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kuliongoza gari, ubovu
wa gari na wembamba wa daraja.
Akizungumza na gazeti hili Afisa Mwandamizi wa SUMATRA mikoa ya Rukwa na
Katavi, David Chiragi alisema basi hilo lilikuwa limeiba njia kwani leseni yake
inaliruhusu basi hilo kufanya safari za Sumbawanga Kirando na siyo Sumbawanga
Mpanda kwa mujibu wa leseni iliyotolewa mwezi Juni mwaka huu.
Alisema hata upana wa daraja ilipotkea ajali hiyo ni mdogo sana ambapo
vipimo vinaonesha daraja hilo lina upana wa mita 3.5 (tatu na nusu) tu wakati
basi lina upana wa mita nne na nusu hivyo kujenga mazingira ya ugumu wa dereva
kulenga daraja inapotokea msukosuko wa aina yoyote hasa wakati wa usiku na
hivyo kuwataka wakala wa barabara mkoani Katavi kuangalia namna ya kupanua
daraja hilo na kuboresha eneo hilo.
Alisema katika kipindi cha Januari hadi July 2013 zaidi ya ajali tisa
zimetokea katika daraja hilo zikihusisha magari makubwa saba na madogo mawili
kutokana na madereva kushindwa kumudu magari yao na kulenga daraja
hilo.
Alisema pia basi hilo lina makosa ya kutembea nje ya ratiba, kuiba njia
na kuzidisha abiria hivyo ofisi yake imechukua hatua ya kuvunja safari za
mabasi ya kampuni ya Sumry za mchana na badala yake mabasi yote yataondoka
Sumbawanga na Mpanda majira ya asubuhi pekee.
Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo wakiongea kwa tabu katika hospitali ya
wilaya ya Mpanda jana walisema kuwa dereva wa basi hilo alikuwa akiendesha kwa
mwendo wa taratibu sana tangu mwanzo wa safari hali iliyowapa shaka kuwa huenda
alikuwa hajui kueondesha magari au basi hilo lilikuwa na hitilafu kwani
waliondoka mjini sumbawanga majira ya saa kumi na moja jioni na kufika eneo
hilo saa saba na nusu usiku tofauti na mwendo wa kawaida ambapo walitakiwa
kufika saa nne usiku eneo hilo.
Kondakta wa basi lililopata ajali alisema kuwa dereva huyo alikuwa mgeni
wa njia pia alikuwa hajazoea kuendesha mabasi aina ya Nissan Diesel hali
iliyomlazimu kumuelekeza njia wakati wote wa safari lakini ilipofika eneo la
mteremko wa mto Sitalike Iku alimueleza kuwa mbele kuna daraja jembamba na kona
kali dereva huyo alibadili gia ikagoma na kuanza kuporomoka hadi mtoni.
Mkuu wa mkoa wa Katavi Dr Rajabu Rutengwe alitoa rambi rambi kwa wafiwa
wote na kuwapa pole wahanga wa ajali hiyo mbaya kutokea tangu mkoa huo uanze.