Serikali ya
Malawi imesema itaendelea na mazungumzo na Tanzania kuhusu mpaka licha
ya kuwa viongozi wa Tanzania hawaelewi mipaka ndiyo maana wanapigania
kuwa wao ni sehemu ya ziwa. Waziri
wa Habari wa Malawi, Moses Kunkuyu alisema wiki iliyopita alipohojiwa
na Shirika la Utangazaji la Malawi (MBC) akisema viongozi wote wa
Tanzania wanadhani wanamiliki Ziwa Malawi (Nyasa) lakini watakuja
kubaini baadaye kuwa hawana hata tone la umiliki.
Msemaji
huyo wa Serikali, alisema wanakubali kwenda kwenye meza ya majadiliano
ya Tanzania na Malawi kwani kufanya hivyo wanataka kuwaeleza ukweli
kuhusu ziwa hilo kwani hawaelewi ukweli wake.
“Viwango vya
uelewa kwa kitu chochote vinatofautiana. Tawala za Tanzania zilikuja
zikaondoka, mawazo ya kumiliki Ziwa Malawi wanayo lakini itafikia hatua
wataamini kuwa ni Ziwa la Malawi.
“Tunataka
kutafuta utatuzi wa hili. Sisi tunafahamu kuwa wanapiga kelele tu lakini
hawana wanachomiliki katika Ziwa Malawi na baada ya kukamilisha
majadiliano, hakuna atakayekuja kuleta hoja nyingine,” alisema Kunkuyu
akikaririwa na gazeti la Nyasa Times.
Itakumbukwa,
Julai 29 mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Benard Membe alitoa tamko la Serikali kuitaka Malawi kuacha
mara moja mpango wake wa kutafuta mafuta na shughuli nyingine katika
ziwa hilo.
Hata hivyo,
Kankuyu alisema kuwa Malawi itaendelea kutafuta mafuta ziwani kama
kawaida na mengine ya maendeleo yatafanyika kwa kuwa yote yako chini ya
milki ya Malawi. Rais wa zamani wa Msumbiji, Joachim Chissano ndiye
aliyepewa jukumu la usuluhishi wa mgogoro huo.
“Sisi kama
Serikali tuna mipango yetu ya maendeleo na hakuna nchi inayoweza
kutuamrisha kwa kile tunachotaka kukifanya kwa hiyo kwa maendeleo ya
kilimo, madini na utafutaji mafuta utafanyika kama ulivyopangwa,”
alisema Kunkuyu ambaye nchi yake imepewa leseni ya utafutaji mafuta na
Kampuni ya Uingereza ya Surestream.
Chanzo - Mwananchi