Rais wa serikali ya mpito nchini
Misri ametangaza kuwa uchaguzi utafanyika mwaka ujao katika juhudi zake
za kutuliza maandamano na hali ya taharuki nchini humo.
Tangazo hilo limetolewa wakati mgogoro ukizidi
kati ya jeshi na wafuasi wa rais aliyepinduliwa Mohammed Morsi karibu na
kambi ya jeshi mjini Cairo ambako zaidi ya watu 50 waliuawa hapo jana
wakati wa mapigano na wanajeshi.Hii inakuja wakati ambapo watu 51 wamethibitishwa kuuawa mjini Cairo.
Chama cha Muslim Brotherhood kinasema kuwa wanachama wake walipigwa risasi wakati walipokuwa wanakesha nje ya makano ambapo Morsi anazuiliwa, lakini jeshi linasema liliwafyatulia risasi kwani waandamanaji nao walikuwa wamejihami.
Rais Morsi, aliyekuwa rais wa kiisilamu na wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, aliondolewa mamlakani na jeshi wiki jana baada ya maandamano makubwa ya kumpinga kufanyika.
Wafuasi wake wanatuhumu jeshi kwa kufanya mapinduzi, lakini wapinzani wake wanasema hatua hiyo ni mwendelezo wa mapinduzi yaliyomwondoa mamlakani aliyekuwa rais Hosni Mubarak mwaka 2011.
Bwana Mansour alitoa amri hiyo Jumatatu jioni.
Amri hiyo inasema kuwa jopo la kufanyia katiba
marekebisho ambalo lilifutwa kazi wiki jana, litaundwa tena katika
kipindi cha siku 15.Mabadiliko hayo kisha yatapigiwa kura ya maoni. Mchakato utapangwa kufanyika katika muda wa miezi minne.
Baada ya kura ya maoni , uchaguzi wa wabunge huenda ukafanyika mapema mwaka 2014.
Hatimaye uchaguzi utafanyika punde baada ya bunge jipya kuundwa.