Balozi Leslie Rowe kutoka ofisi ya Serikali ya Marekani anayeshughulikia mambo ya afya.(Picha na Maktaba).
Na Anna Nkinda – Maelezo
Serikali
ya Marekani kupitia Mpango wa dharula wa kupunguza makali ya VVU na
Ukimwi (PEPFAR) imeipatia Serikali ya Tanzania dola za kimarekani
millioni tatu fedha ambazo zitatumika kuwapima na kuwatibu wanawake
wanaosumbuliwa na matatizo ya saratani ya mfuko wa kizazi.
Hayo
yamesemwa jana na Balozi Leslie Rowe kutoka ofisi ya Serikali ya
Marekani anayeshughulikia mambo ya afya wakati akiongea na watu
mbalimbali walioshiriki mkutano wa wake wa Marais wa Afrika uliofanyika
katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Aidha
Serikali ya Marekani pia imetoa mashine 16 za cryotherapy ambazo
zitatumika kama sehemu ya matibabu kwa ugonjwa wa saratani ya mfuko wa
kizazi katika Hospitali ya Kansa ya Ocean Road.
Balozi
Rowe alisema kuwa upatikanaji na mashine hizo utawasaidia wanawake
wengi ambao wanasumbuliwa na ugonjwa wa Kansa ya shingo ya kizazi
kuweza kupata huduma ya vipimo na matibabu mapema na haraka.
“Kutokana
na maambukizi ya VVU wanawake wengi wako katika hatari kubwa ya kupata
ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti kwa kushirikiana na
PEPFAR tutaendelea kuwaunga mkono utepe wa pink,utepe mwekundu kuokoa
maisha ya wanawake.
Jitihada
za pamoja zinahitajika kwa kushirikiana na vikundi vya kijamii na
kuimarisha miundombinu ili kuhakikisha kuwa tunatoa vipimo na matibabu
ya saratani kwa wakati”, alisema Balozi Rowe.
Akiongea
na waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo Mama
Kikwete aliishukuru Taasisi ya Bush kwa kufanya mkutano huo nchini na
kusema kuwa mambo yaliyojadiliwa ni upatikanaji wa elimu kwa mwanamke,
upatikanaji wa Afya bora na kumuwezesha mwanamke kiuchumi.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) alisema kuwa mwanamke ni mtu muhimu sana katika jamii haijalishi
ana elimu kiasi gani yeye ni mlezi wa familia na ukimwezesha mwanamke
kielimu ni ukombozi mkubwa katika jamii kwani ni rahisi kwake
kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi.
“Miaka
ya nyuma kutokana na baadhi ya watu kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu
ugonjwa wa Ukimwi waliweza kuamini kuwa mtu akiwa na maambukizi ya ya
VVU amerogwa lakini hivi sasa baada ya watu kupata elimu wkamekuwa na
uelewa mkubwa.
“Ukimwezesha
mwanamke kielimu na kiuchumi anakuwa na uhuru wa kufanya mambo yake
bila ya kutegemea msaada kutoka kwa mme wake ninachowaomba wanawake
wenzangu mfanye kazi kwa bidii kwani mwanamke akiwa na kipato cha
kutosha hawezi kudharaulika”, alisema Mama Kikwete.
Alisema
kuwa zamani wanawake wasiokuwa na kazi walikuwa wanaitwa magoli kipa
ingawa walikuwa na kazi kubwa ya kuangalia familia na jamii ikasahau
kuwa wanawake ndiyo wazalishaji mali. Pia aliwaomba wanawake wasiogope
kuchangamkia fursa zinazopatikana na wasiache kumuunga mkono mwenzao
pale anapoomba nafasi ya kupata fursa hizi kwani wakiwa pamoja
wanaweza.
Katika
mkutano huo pia Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa zamani wa
Marekani George Bush walitambulisha rasmi Utepe wa Pinki , Utepe
mwekundu ambayo ni alliance inayofanya kazi ya kupambana na kansa ya
saratani ya mfuko wa kizazi na saratani ya matiti katika nchi za Kusini
mwa jangwa la Sahara na Amerika ya Kusini.
Tanzania
ni nchi ya tatu Barani Afrika kutambulisha Utepe wa Pinki , Utepe
mwekundu alliance nchi zingine ni Zambia na Botswana.
Mkutano
huo wa siku mbili uliomalizika jana uliandaliwa na Taasisi ya Rais
mstaafu wa Marekani George Bush na kuhudhuriwa na baadhi ya wake Wa
Marais wa Afrika na Mke wa Waziri mkuu mstaafu Wa Uingereza Cherie
Blair.