Waziri wa mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi
Mdahalo
wa kujadili mstakabali wa amani ya taifa ulioandaliwa na Jumuiya ya
Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), umeibua mambo
mazito ambapo washiriki wameinyooshea kidole serikali wakidai ndiye
mchawi wa wananchi.Mdahalo
huo ambao kauli mbiu yake ilikuwa ni Mustakabali wa Amani na Usalama wa
Wananchi wa Taifa Letu kwa Miaka 50 Ijayo, ulifanyika jana katika
Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwashirikisha
wanazuoni, wanasiasa, viongozi wa vyombo mbalimbali vya ulinzi na
serikali.Wachokoza
mada walikuwa ni mhadhiri wa sheria wa chuo hicho, Dk. Onesmo Kyauke
aliyegusia mfumo wa utendaji wa Jeshi la Polisi katika kusimamia amani
ya nchi, Profesa Benadetha Kiliani, mtaalam wa sayansi ya siasa na
utawala kwa umma na mwanahabari nguli na mhadhiri wa Shule Kuu ya
Uandishi wa Habari, Dk. Ayoub Rioba.Katika
mada yake, Dk. Kyauke aliliponda jeshi la polisi linavyokiuka sheria
katika kutekeleza majukumu yake kiasi cha kuruhusu kuingiliwa na
wanasiasa na kuelekezwa jambo la kufanya.Bila
kuuma maneno, mhadhiri huyo alimtaja wazi wazi Naibu Katibu Mkuu wa CCM
(Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, akidai kwa sasa analiendesha jeshi
hilo kwa kuingilia majukumu ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
(DCI) na Mwendesha Mashataka Mkuu (DPP).
Alisema
kuwa mwanasiasa huyo ambaye ni mbunge wa Iramba Magharibi, amekuwa
akiwatuhumu wanasiasa wa vyama vya upinzani kuwa ni magaidi na polisi
wamekuwa wakiwakamata na kuwafungulia mashtaka hayohayo anayosema kada
huyo bila hata kuwa na ushahidi.
Dk.
Kyauke alitolea mfano wa matukio ambayo Nchemba amekuwa akiyafanya kuwa
ni pamoja na lile la kuonyesha ushiriki wa kupanga tukio la ugaidi la
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(CHADEMA), Wilfred Lwakatare.
Tukio
lingine alisema ni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani jijini
Arusha, ambapo kiongozi huyo aliwataka wananchi wa jiji hilo kutochagua
madiwani wa CHADEMA kwa kuwa ni chama cha ugaidi kwa madai kwamba ndio
waliohusika kummwagia tindikali kijana wa CCM kule Igunga.
Kutokana
na matamshi hayo, mhadhiri huyo alisema baadhi ya wanachama wa CHADEMA
waliweza kukamatwa kama njia mojawapo ya kuisaidia polisi; jambo
linalowafanya kama wasomi kujiuliza kuwa Mwigulu siku hizi kawa DCI au
DDP?
Kuhusu
utendaji wa Jeshi la Polisi, alisema ndilo limekuwa chanzo kikubwa cha
uvunjifu wa amani kwa kupoka haki ya Kikatiba ya wananchi kuandamana na
kufanya mikutano huku akitolea mfano wa mauaji yaliyofanywa na jeshi
hilo ya mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, kijijini Nyororo, mkoani
Iringa, wakati wa kuzindua matawi ya CHADEMA.
Katika
mauaji hayo, alisema ushahidi wa wazi umeonyesha namna gani polisi
walivyoshiriki na tume zote zilizoundwa zikamuelekezea kidole Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Iringa na Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini hakuna
hatua zilizochukuliwa hadi leo zaidi ya polisi mwenye cheo kidogo
akitolewa kafara huku mkubwa wake akiendelea kupandishwa cheo.
Pia
alisema kumekuwepo na upendeleo wa jeshi hilo kwa kutetea chama tawala
ikiwemo enzi za IGP Omar Mahita kudai kuwashikilia wanachama wa Chama
cha Wananchi (CUF) na majambia ingawa hadi leo wamekosa uthibitisho
lakini kutokana na uongo huo wameshindwa kumchukulia hatua kiongozi
huyo.
Katika
mapendekezo yake, Kyauke aliitaka polisi kubadili mfumo wake wa kufanya
kazi, na kuhoji kwa nini Tanzania ni dhambi kuandamana huku akimtaka
Waziri Mkuu kufuta kauli yake ya kutaka wananchi kupigwa tu na jeshi
hilo wanapokaidi amri.
Prof.
Kilian kwa upande wake, alisema mpaka sasa bado kiini cha uvunjifu wa
amani hakijagundulika na badala yake pande zote zimekuwa zikirushiana
mpira ikiwemo serikali, wananchi na wanasiasa.
Alizitaja
sababu zinazochangia matukio hayo kuwa ni pamoja na hali ya upinzani
kuja juu hivyo chama tawala kinajihami kutokana na mabadiliko hayo,
kuongezeka kwa kiwango cha umaskini na mfumo wa kiliberali ambao
umechangia matabaka na uhuru wa kutoa maoni tofauti na enzi za ujamaa.
Naye Dk.
Rioba alisema suala la amani sio la kuombewa kanisani au msikitini bali
ni la kisayansi zaidi na kudai kwamba wanasiasa wamekuwa wakijidanganya
pale wanapowahimiza watu kuliombea taifa liwe na amani.
Pia Rioba
alikanusha vyombo vya habari kuwa vimekuwa vikichangia kuharibu amani
na badala yake alivifananisha vyombo hivyo na bunduki ambapo kama
isipotumiwa kamwe haiwezi kuharibu amani.
Akifafanua
hili alisema vyombo vya habari vitaharibu amani endapo tu wanasiasa
watavitumia na kuitaka jamii ielewe kwamba vyombo hivyo vina dhima kubwa
kama mlinzi wa taifa na ndio maana wakati mwingine vinapendekezwa kuwa
NGO’s ili viweze kufanya kazi kwa uhuru zaidi.
Katibu
Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa alisema mchawi wa hayo yote ni
serikali, huku akinukuu ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora iliyomtuhumu aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael
Kamuhanda, na Msajili wa Vyama vya Siasa. Akisema amani sio suala la
kuhubiriwa au kujadiliwa bali ni matokeo ya utekelezaji wa haki
mbalimbali.
Slaa pia
alilalamikia vitendo vya ukatili vilivyofanywa Mtwara na vyombo vya dola
dhidi ya wananchi, huku akimnyooshea kidole Brigedia Elia Athanas
aliyekuwa amemwakilisha Mkuu wa Majeshi.
“Jeshi
letu lilikuwa linaheshimika sana, lakini siku za hivi karibuni
linaelekea kupoteza heshima yake kwa jamii, tukirejea mfano katika
uchaguzi mkuu uliopita ambapo mnadhimu wa jeshi, Abdulrahman Shimbo,
alivyotoa kauli yenye utata, jeshi linaingiaje kwenye siasa wakati suala
la uchaguzi ni suala la kiraia?” alihoji.
Hoja ya
Dk. Slaa kuhusu utendaji wa jeshi la wananchi mkoani Mtwara ilipingwa
kwa haraka na Brigedia Athanas akisema: “Naomba kuweka wazi kuwa jeshi
letu liko Mtwara, lina adabu na vitendo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa ni
vya propaganda tu kama alivyosema Dk. Slaa.”
Licha ya
kiongozi huyo kujitetea, mchangiaji aliyefuata, Julius Mtatiro ambaye ni
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), alithibitisha kuwa wanajeshi
wanabaka na walitenda vitendo vya kikatili dhidi ya raia na viongozi wa
chama hicho akiwemo mkurugenzi wao, Shaweji Mketo.
Mwakilishi
wa NCCR Mageuzi, Faustine Sungura, alisema chama hicho hakiko tayari
kufanya maandamano bali kinapambana kwa nguvu ya hoja na kwamba
wataendelea kutumia nguvu ya hoja.
Akihitimisha
kongamano hilo, Wazri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema
kuwa kati ya mambo ambayo yanampa changamoto ni amani ya nchi hii.
“Tulirithi nchi ikiwa na amani, hivyo tuna deni la kurithisha nchi hii ikiwa ya amani katika kizazi kijacho.
Dk.
Nchimbi alikemea suala la udini, akiwatahadharisha Watanzania kuwa
wasiingie katika vurugu na wasikubali kugawanywa kwa sababu ya dini zao.
“Tukiingia
katika vurugu za dini hatutapona, Wakristo na Waislam wote tukatae
kugawanywa kwa kutumia misingi ya udini kwa manufaa ya Tanzania ya sasa
na kizazi kijacho.
Waziri
Nchimbi huku akimtambua Dk. Slaa, alisema wanasiasa wote wana wajibu wa
kuwatumikia wananchi, “Suala la amani sio suala la Chama cha Mapinduzi
peke yake, ni suala la wanasiasa wote wa chama tawala na wapinzani
kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma, na kuvumiliana kisiasa ndiko
kunaleta amani.