MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinapinga mfumo wa
serikali tatu usiingizwe katika Katiba mpya kwa vile kinajua kwamba
huo ndio utakuwa mwisho wa utawala wake. Mbowe alitoa kauli hiyo katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Chipukizi mjini Tabora
na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi. Alisema kuwa CCM inakwepa
kuzungumzia suala la serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kwa kuhofia kwamba vyama pinzani vitatwaa ushindi
katika ujaguzi mkuu ujao.
CCM
inaogopa serikali tatu kwa sababu inajua Zanzibar ni mali ya Chama cha
Wananchi (CUF) na Tanganyika itakuwa ya CHADEMA; yenyewe itakuwa wapi?”
alihoji. Mbowe alifafanua kuwa mfumo wa serikali mbili umekuwa manufaa
kwa Wazanzibar kwani Watanganyika wengi wakienda kwao hawana uhuru wa
kumiliki mali tofauti na ilivyo wao wakija bara wanamiliki kila kitu
sawa na Watanzania wengine. “Tanganyika tupewe uhuru wetu kama
Wazanzibari, wana bendera yao, wimbo wa taifa, rais wao na Bunge lao,”
alisema. Mbowe pia aliwatahadharisha wananchi juu ya hujuma
wanazofanyiwa na serikali iliyo madarakani ikiwemo kulipia kodi ya
umiliki wa laini ya simu za mikononi.
Alisema kuwa serikali ya CCM ilifuta kodi mbalimbali kwa ajili ya
kumhadaa mwananchi ili aweze kuipigia kura lakini hivi sasa zimerejeshwa
kwa mlango wa nyuma ikiwemo hiyo ya simu na ile inayowataka wananchi
kununua visimbuzi ndipo waweze kupata mawasiliano ya runinga zao. Mbowe
ambaye yuko kwenye ziara ya kawaida kwa ajili ya kuimarisha chama,
alisema kuwa kuanzia Agosti 4 chama hicho kitafanya ziara ya kutembelea
mikoa yote nchini na kukutana na wananchi ili kuzungumza na kujadili nao
wanataka Katiba iwe na muundo gani. Katiika hatua nyingine wananchi
wamelaani vikali kauli iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
CCM, Nape Nnauye, kwamba wanaotaka serikali tatu ni wazee ambao
wanagojea kifo.
Source: Tanzania Daima