Blogger Widgets

Social Icons

Pages

Saturday, July 20, 2013

Serikali kutambua raia wake kupitia taarifa za DNA.

IMG_0286 
  IMG_1512 
Mkemia kutoka Vinasaba kutoka Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali(GCLA) Fidelis Segumba(kulia) akiwaeleza waandishi wa habari juu ya matumizi ya Teknolojia ya Vinasaba vya Binadamu leo Jijini Dar es Salaam kushoto ni Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Makosa ya Jinai Biologia na Vinasaba kutoka kutoka ofisi hiyo Bi. Gloria Machuve.
PICHA ZOTE NA FRANK MVUNGI

……………………………………………….

Na Fatma Salum – MAELEZO
Serikali kupitia ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ina mpango wa kuanzisha utaratibu wa kutambua raia wake kupitia taarifa za vipimo vya vinasaba vya binadamu maarufu kama DNA.

Akifafanua mpango huo katika mkutano wa waandishi wa habari na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Makosa ya Jinai Biolojia na Vinasaba Gloria Machuve amesema kupitia mfumo wa taarifa za vinasaba utaiwezesha serikali kutambua raia wake na wahamiaji wasio raia kutokana na taarifa zao kutokuwepo kwenye mfumo huo.

Bi Machuve ameeleza kuwa mpango huo ukikamilika watanzania wataweza kupimwa vinasaba vyao na taarifa zao zitawekwa kwenye mfumo rasmi wa taarifa (Database) hivyo kurahisisha shughuli za uhamiaji ikiwemo utoaji wa pasipoti na vitambulisho vya uraia.

Aidha mfumo huo utarahisisha utambuzi wa viungo vya miili ya watanzania wanaofariki kwenye majanga kama moto na ajali za vyombo vya usafiri wakiwa nje ya nchi kwani taarifa za vinasaba vyao zitakuwepo kwenye mfumo hivyo zitaoanishwa na majibu ya vinasaba vya viungo hivyo na hatimaye serikali kupata miili ya raia wake.

Pia Bi Machuve ameongeza kuwa kupitia mfumo huo utoaji wa vyeti vya kuzaliwa utaambatana na taarifa kamili za vinasaba vya wazazi  hivyo kurahisisha watu kupata vyeti vyenye majina ya wazazi wao halali.

Naye Mkemia kutoka Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Fidelis Segumba amesema kuwa mfumo huo pia utasaidia kupunguza tatizo la kubadilishwa watoto hospitalini kwani utawezesha kutambua mama halali wa mtoto aliyezaliwa.

Segumba amesema faida nyingine za mfumo huo ni pamoja na utambuzi wa viungo vya watu wenye ulemavu ngozi , kuondoa tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kutambua wahalifu husika wa makosa ya ubakaji.

Ili kufanikisha mpango huo Segumba amesema serikali inabidi kuongeza wataalamu na kuongeza fedha kwa ajili ya kununulia mitambo mingi ya kufanyia kazi hiyo.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...