BAADA
ya kukamatwa na dawa za kulevya nchini Afrika Kusini, msanii
anayeshiriki katika video za wasanii wa muziki wa bongo fleva, Agnes
Jerald 'Masogange' na mwenzake Melisa Edward, ukweli umeibainika kwamba
dawa walizokamatwa nazo ni za kutengenezea dawa za kulevya, ambazo
hazipatikani nchini na hazina matumizi yoyote.
Kupitia
taarifa rasmi zilionesha kuwa, Chemical bashirifu ndiyo aina ya dawa
walizokamatwa nazo nchini humo, ambapo wasanii hao walikamatwa nchini
Afrika Kusini wakitokea Tanzania.
Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam leo Kamishina wa Tume ya
Kuratibu na Kuthibiti Dawa za Kulevya nchini, Christopher Shekiondo
alisema kwamba kwa mujibu wa sheria za nchi, dawa walizokamatwanazo
wasichana hao zinatumika kutengenezea dawa za kulevya, ambapo adhabu yao
ni sawa na mtu aliyekamatwa na dawa za kulevya.
Wasichana hao walikamatwa Julai 5, mwaka huu nchini humo wakiwa
shehena ya dawa za kulevya zenye thamani ya sh. bilioni 6.8 wakitokea
Tanzania.
Shekiondo alisema dawa walizokamatwa nazo hazitumiki moja kwa moja
kama dawa, bali zinatumika kutengenezea dawa za kulevya hivyo kwa mujibu
wa sheria, adhabu zao zinakwenda sambamba na waliokamtwa na dawa za
kulevya.
"Dawa hizo hazitumiki moja kwa moja bali zinatumika kutengenezea dawa
za kulevya, hivyo kama taarifa tulizopata ni sahihi juu ya aina ya dawa
walizokamatwa nazo na dawa hizi hazitumiki sana nchini, bali zinatumika
Afrika Kusini, Asia pamoja na Ulaya," alisema Shekiondo.
Alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, mtu anayekamatwa na dawa hizo
mara nyingi hukumbwa na adhabu ya kuhukumiwa miaka 20 au kifungo cha
maisha.
Akielezea kuhusu wasichana hao wawili kupanda kizimbana juzi,
Kamishina huyo aliweka wazi kuwa hadi sasa hawajapata taarifa zozote
rasmi, zaidi ya kupokea zile za awali za kushikiriwa na Jeshi la Polisi
Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi.
Kamishina huyo alisema inaonesha Watanzania wengi wamekamatwa na dawa
za kulevya nchini Brazil ambao idadi yao inafikia 109, ambapo wengi wao
wameshahukumiwa.
Alisema watu hao wamekamtwa nchini humo, wakiwa na dawa aina ya
cocain kwa ajili ya kusafirisha nchi nyingine, huku baadhi yao
wamehukumiwa kunyongwa pamoja na kifungo cha maisha, ingawa idadi kamili
ya watu hao bado haijafika rasmi.
"Tumepokea taarifa jumla ya Watanzania 109 wamekamtwa nchini Brazil,
ingawa bado tunasubiri kujua ni wangapi waliohukumiwa kifo, pamoja na
kifungo cha maisha," alisema Shekiondo.
Aliongezea kuwa baadhi ya nchi nyingine, ambazo Watanzania
wanakamatwa na dawa hizo za kulevya wakiwa wanasafirisha ni China vijana
34, Kenya 30, Pakistani 16, Falme za Kiarabu ikiwemo Dubai 14, pamoja
na nchi nyingine kama Japan, Argentina, Msumbiji, Afrika Kusini, Ureno,
pamoja na Uingereza.
Akizungumzia hukumu ambazo zimeshatolewa baadhi ya nchi walizokamatwa
Watanzania hao,, Kamishina huyo alisema Brazil ambayo ndiyo Watanzania
wengi wamekamatwa idadi kamili, bado hawajapata ingawa Kenya tayari wapo
waliohukumiwa kifungo cha maisha, huku wengine wakiwa wamehukumiwa
kifungo cha miaka 20 hadi 40, nchi China wapo waliohukumiwa kifo na
kifungo cha maisha.
Shekiondo alisema Tanzania kwa sasa inajulikana kama ni njia ya kusafirisha dawa hizo.
Alisema kuna baadhi ya watu wanatumia maji kusafirisha dawa hizo,
yaani meli, jahazi pamoja na mitumbwi, hivyo wana mikakati ya kutoa
elimu kwa jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya.