Msanii nyota wa muziki wa asili, Saida Karoli ambaye alivumishiwa kifo
hivi karibuni anatarajiwa kujitokeza hadharani kwa mara ya kwanza
kufanya maonyesho maalum ya kudumisha amani yatakayofanyika mkoani
Tabora.
Karoli aliyewahi kutamba na nyimbo mbalimbali kama 'Chambua kama
Karanga' na nyingine atafanya onyesho la kwanza kesho Jumamosi katika
shamrashamra za kusherehekea sikukuu ya Sabasaba mjini Igunga na
kutambulisha nyimbo zake mpya kwa mashabiki wa mji huo.
Kwa mujibu wa mratibu wa maonyesho hayo, Livenus Madaraka, onyesho la
pili la mwanadada huyo litafanyika Julai 9 katika mji wa Nzega,
akiwadhihirishia mashabiki wake kwamba yu hai na anaendeleza 'makamuzi'
kama kawaida.
Mratibu huyo alisema amewataka wale ambao bado hawajaamini kama Saida
Karoli anadunda wajitokeze katika maonyesho hayo ambapo msanii huyo
ameahidi kufanya makubwa katika kuwapa burudani mwanzo mwisho.
"Mwenyewe
ameahidi kukata kiu ya mashabiki wake kwa kuwapa burudani kabambe na
kuzitambulisha nyimbo zake mpya na zile za zamani zilizompatia umaarufu
mkubwa ndani na nje ya Tanzania," alisema Madaraka.