Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
likiwa bado halijatangaza rasmi majina ya wapiganaji wake waliofariki
huko Sudan, askari polisi aliyeko huko ameeleza chanzo na mazingira ya
tukio hilo.
Wapiganaji saba na wengine 14 walijeruhiwa Jumamosi iliyopita.
Gazeti hili limepata majina ya askari hao
waliofariki kutoka vyanzo tofauti lakini limeshindwa kuwataja leo kwa
kuwa JWTZ kupitia kwa msemaji wake, Kanali Kapambala Mgawe limesisitiza
kuwa haliwezi kutangaza majina hayo hadi litakapowasiliana na jamaa za
askari waliofariki.
Tukio lilivyotokea
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, askari
polisi huyo anayefanya kazi katika Mji wa Nyala uliopo Darfur, alisema
mauaji hayo yalitokea wakati askari hao walipokuwa wakifuatilia magari
yao yaliyokuwa yameporwa na kundi mojawapo la waasi.
Usalama katika Mji wa Nyala ambao ndiyo mkubwa
zaidi katika eneo la Darfur, umekuwa mdogo katika siku za hivi karibuni.
“Wale wanajeshi walikuwa doria ya kawaida, ila kama wiki moja iliyopita
waasi walivamia tena doria ya wanajeshi wetu na kupora magari manne
bila kuua mtu.
“Siku ya mauaji hayo wanajeshi wetu wakiwa tena
katika doria waliyaona yale magari yaliyoporwa kwa mbali yamepaki,
waliyafuatilia, walipokaribia kumbe ulikuwa mtego, wakashambuliwa,”
alisema askari huyo na kuongeza: “Mauaji hayo yametokea takriban
kilometa 70 kutoka katika kambi niliyopo mimi, lakini wote tupo eneo la
kusini na hiyo kambi ya Korabeche inaongozwa na jeshi letu.”
Tofauti na chanzo chetu cha habari huko Darfur,
Kanali Mgawe alisema wanajeshi hao walishambuliwa walipokuwa kwenye
msafara wa kusindikiza walinzi wa amani.
Makundi yanayopambana
Askari huyo aliyeko Darfur alisema: “Makundi
yanayopambana huku yapo mengi ila makubwa yapo kama matano. Kuna moja
linaitwa Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan (SPLA), ambalo limegawanyika
katika makundi mawili pia kuna mengine kama JEM, Janjaweed na
mengineyo.”
Akizungumzia mshtuko walioupata baada ya mauaji
hayo, askari huyo alisema wafanyakazi wote wanaohusika na ulinzi wa
amani wamepatwa na ganzi... “Huku kwa kweli hali imekuwa chungu, tangu
askari hao wauawe hali haitabiriki kabisa, tupo nje hapa (hospitali
walimohifadhiwa), tunasubiri uhakika.”
“Hawa jamaa (waasi), wamesheheni silaha na wana
vifaa vya kisasa kiasi kwamba hata ndugu zetu walizidiwa kutokana na
wenzao kuwa na silaha nzito.