Arusha.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, amewasili Arusha na
kupokelewa na ulinzi mkali wa polisi, kuanzia uwanja wa ndege wa Arusha
hadi ofisi yake ya ubunge Arumeru Mashariki.
Nassari
ambaye jana alitarajiwa kupokewa na mamia ya wanachama wa chama hicho,
baadaye angefanya mkutano wa hadhara jimboni kwake, aliwasili saa 6:00
Uwanja wa Ndege Arusha.
Hata
hivyo, polisi ilitangaza kufuta mapokezi na mkutano wake, kwa maelezo
kuwa ni kutekeleza uamuzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec kuzuia
shughuli zozote za kisiasa Arusha hadi kukamilika uchaguzi wa madiwani
Julai 14, mwaka huu.
Kamanda wa
polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alisema wamelazimika kuongeza
ulinzi na kuzuia mapokezi hayo na mkutano, kwani vingekiuka maagizo ya
Nec.
Akizungumza ofisi za Chadema Mkoa wa Arusha jana, Nassari alieleza kushangazwa na ulinzi mkali wa polisi.
“Ulinzi
huu umeanzia Dar es Salaam Airport (uwanja wa ndege), nimeshuka Arusha
hadi sasa polisi wanarandaranda nje ya ofisi hizi,” alisema Nassari.
Pia,
mbunge huyo alieleza kushangazwa na polisi kuweka ulinzi ofisi yake,
huku wananchi wenye shida wakishindwa kuzungumza naye kwa uhuru.
Alisema amerejea Arusha salama na sasa amepona yupo tayari kushiriki kama wakala wa uchaguzi mdogo wa Jumapili.
Akizungumzia
maandalizi ya uchaguzi mdogo, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini,
Aman Golugwa, alisema chama kimewapanga wabunge wake kadhaa kuwa
mawakala.
“Tumeunda vikosi na Godbless Lema (Mbunge Arusha Mjini) atakuwa anaongozwa kikosi cha QS1 hakuna matata,” alisema Golugwa.